Dar es Salaam. Nyenzo za kidijitali kama vile simu za mkononi, vishikwambi, programu na mifumo ya takwimu, zimesaidia upatikanaji wa huduma za afya kwa urahisi zaidi, kwa gharama nafuu na kwa usawa nchini.
Mafanikio hayo yamejidhihirisha wazi, baada ya idadi ya wanaofariki wakati wa ujauzito na kujifungua kushuka kutoka 556 kati ya kila wanawake 100,000 mwaka 2016 hadi 104 mwaka 2022.
Hili liliwezekana baada ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii, wauguzi na madaktari waliopo pembezoni katika baadhi ya maeneo, kutumia simu za mkononi na vishikwambi kurahisisha utoaji huduma kwa kundi hilo.
Ingawa hili ni ongezeko kubwa la mafanikio, bado ni juu ya lengo la kimataifa la vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000, jambo linaloonyesha kwamba ubunifu zaidi unahitajika.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu kuhusu ujio wa Mkutano wa 12 wa Afya Tanzania (Tanzania Health Summit), rais wa Taasisi ya Afya Tanzania Health Summit (THS), Dk Omary Chillo amesema Serikali, asasi zisizo za kiserikali, watafiti na wabunifu wa teknolojia wanashirikiana kuunda suluhisho jipya.
Amesema suluhisho hilo ni kuanzia ujumbe wa simu kwa akina mama unaokumbusha tarehe za kliniki, hadi dashibodi za kidijitali, zinazosaidia hospitali kuepuka uhaba wa dawa.
Kwa mujibu wa Dk Chillo, hadithi za mafanikio haya na nyingine nyingi zitatolewa na wabunifu 2,000 wakati wa mkutano huo, utakaofanyika Oktoba Mosi hadi 3, 2025, jijini Dar es Salaam, zikionyesha jinsi afya kidijitali inavyoweza kuokoa maisha na kuileta nchi karibu na lengo la afya kwa wote.
“Mfano wenye nguvu ni matumizi ya ujumbe wa simu kwa akina mama. Kwa mfano, mradi wa Mama-Bora huko Zanzibar hutuma SMS zenye ushauri kwa wajawazito, na kuwasaidia wengi kuhudhuria kliniki na kuwachanja watoto wao,” amesema.
Ametaja ubunifu mwingine ni Tunza Afya chatbot ya WhatsApp ambayo tayari inasaidia akina mama wapya 59,000 kwa ushauri rafiki kuhusu ujauzito, malezi ya mtoto na dalili za hatari.
“Katika miezi miwili tu ya 2025, mamia ya wazazi waliripoti kuwa chatbot imewasaidia kutambua dalili za hatari katika ujauzito na maradhi ya utotoni. Vifaa hivi vimeonyesha jinsi simu za mkononi zinavyoweza kuwafikia akina mama popote walipo, kuboresha maarifa ya afya na kuokoa maisha kwa gharama ndogo,” amesema Dk Chillo.
Amesema vifaa vya kidijitali havisaidii wagonjwa tu bali pia vinaimarisha mfumo mzima wa afya.
“Kwa mfano, katika maeneo ya majaribio, wahudumu wa afya walitumia dashibodi mpya za takwimu zaidi ya mara 2,500 ndani ya miezi sita pekee kupanga huduma vizuri, na kusaidia kliniki kujua dawa na watumishi wanapohitajika zaidi.”
Dk Chillo amesema, katika kliniki 10 za majaribio, kukagua akiba ya dawa kila mwezi kulipunguza ziada zisizo za lazima za dawa kutoka asilimia 35 hadi asilimia 28, jambo lililoleta upungufu mdogo wa dawa na matumizi bora ya fedha.
Wataalamu wa ndani pia waliunda mfumo wa kitaifa wa takwimu za afya unaounganisha rekodi za hospitali, maabara na famasia, hivyo kuondoa dosari za kurudia faili na kufanya huduma iwe ya haraka na rahisi zaidi.
Kwenye upande wa afya ya mama na mtoto, amesema zana mpya za akili mnemba (AI) zimekuwa mkombozi. Mradi mmoja uliopitia rekodi 300,000 za wajawazito uliweza kutabiri matatizo ya presha ya juu kwa usahihi wa asilimia 95, na kusaidia madaktari kuchukua hatua mapema.
Dk Chillo amesema chombo kingine, kiitwacho Sevia, kinawasaidia wauguzi kugundua saratani ya shingo ya kizazi kwa kutumia simu janja. Tayari kimeweza kuchunguza wanawake zaidi ya 30,000 katika kliniki 248 na ni sahihi kwa asilimia 98 sawa na wataalamu bingwa.
“Mafanikio haya yana maana kwamba magonjwa yanagunduliwa mapema, matibabu yanatolewa kwa wakati, na maisha yanaokolewa kwa gharama nafuu zaidi,” amesema.
Ametaja vifaa vipya vya kidijitali vinabadilisha jinsi huduma za wanawake na akina mama zinavyotolewa Tanzania.
Dk Chillo amesema siyo ubunifu wa teknolojia ya juu pekee unasaidia, “Huko Geita, wajawazito sasa wanahudhuria kliniki kwa makundi badala ya kwenda peke yao, na hii imeongeza uelewa, msaada na mahudhurio yao, huku pia ikipunguza gharama.”
“Huko Zanzibar, mpango wa Jamii ni Afya uliwapa watoa huduma ngazi ya jamii kompyuta mpakato zenye programu ya afya. Ndani ya mwaka mmoja pekee, walifikia wanawake 100,000 na watoto 400,000, na kusaidia wazazi kuboresha malezi ya watoto kutoka asilimia 75 hadi asilimia 91, na hata kupunguza taarifa za unyanyasaji wa watoto.”
Dk Chillo ametolea mfano Dar es Salaam, kampuni changa iitwayo Capelex ilizindua programu ya famasia mtandaoni inayoruhusu wagonjwa kupakia dawa walizoandikiwa na kuzungumza na wafamasia. Ndani ya miezi michache, ilishughulikia usambazaji wa dawa 300, mashauriano ya mtandaoni 420, na kupata kuridhika kwa watumiaji kwa asilimia 88.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania MAT, Dk Mugisha Nkoronko akisema zama za mawe zilipita, sasa ni zama za kidijiti, ambapo teknolojia inatumika kuratibu kazi na kuongeza ufanisi unaochochea tija kwenye kazi na maendeleo.
Amesema zama hizi zinatumia sayansi ya takwimu kujenga mifumo.
“Katika sekta ya afya Tehama kwa aina zake inasaidia vitu vingi sana. Kwa mfano mfumo wa huduma za afya (electronic health management system) unaongoza Itami wa huduma za tiba, unaharakisha utoaji wa huduma, unaboresha usalama wa huduma, mfumo unaotumia intaneti.
“Kwa kutumia teknolojia ya akili Mnemba (AI) inasaidia kuongeza ufanisi na usalama wa ugunduzi wa magonjwa, na kuboresha tiba,” amesema.
Dk Mugisha ametaja matumizi mengine ni kusaidia ufuatiliaji wa magonjwa, kusaidia rufaa za wagonjwa, na upashanaji habari katika jamii.