Mavunde ataka viongozi waombewe | Mwananchi

Dodoma. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amewataka Watanzania kuwaombea viongozi wa nchi kuelekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.

‎Uchaguzi mkuu wa kuwapata Rais, wabunge na madiwani unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

‎Mavunde ametoa kauli hiyo leo Jumapili Agosti 24, 2025 jijini Dodoma kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Petro (St. Peter) lililopo Kisasa Kata ya Dodoma Makulu.

‎Amesema Watanzania wote bila kujali dini zao watumie nyumba za ibada kumwomba Mungu ili aendelee kudumisha amani nchini, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

‎Amesema amani iliyopo ndiyo inasababisha watu wanakusanyika makanisani na misikitini kumwabudu Mungu hivyo ni wajibu wao kuwaombea viongozi ili uchaguzi uwe wa amani.

‎”Kuna mataifa ambayo hawana amani na hivyo hawana hata muda wa kuabudu kama sisi tulivyo hapa leo. Tuendelee kuwaombea viongozi wetu ili nchi iendelee kuwa na amani na uchaguzi mkuu upite salama,” amesema Mavunde.

‎Aidha amewaomba waumini wa Kanisa la Anglikana kutenda matendo mema ikiwemo kuchangia ujenzi wa makanisa kwani, hata wasipokuwepo sadaka zao zitaendelea kukumbukwa na vizazi vijavyo kwa kujitoa kwao.

‎Kwa upande wake Mchungaji wa kanisa hilo, Dickson Jackson amemshukuru Mungu kwa kanisa hilo kupata hati baada ya kufuatilia kwa takribani miaka 20.

‎Amesema baada ya kufuatilia hati ya kiwanja cha kujenga kanisa hilo kwa muda mrefu wamefanikiwa kuipata Februari 2025 na hivyo wameanza kazi ya kulijenga.

‎Amesema kutokana na mgogoro wa ardhi uliokuwepo kati yao na mwekezaji kanisa halikuweza kufanya maendeleo yoyote lakini kwa sasa wameanza ujenzi wa kanisa hilo ambalo litakuwa kubwa na la kisasa.

‎”Eneo la kanisa lilikuwa na ukubwa wa takriban ekari tisa lakini baada ya kukaa na viongozi wa Serikali, kanisa lilikubali kuachilia ekari  tano kwa ajili ya matumizi ya kijamii na kubakiwa na ekari nne ambazo tutazitumia kwa ajili ya maendeleo ya kanisa,” amesema Mchungaji Jackson na kuongeza kuwa,

‎”Kanisa limechagua kuwa na amani na jamii inayotuzunguka kama Biblia inavyotutaka.”

‎Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi, mipango na fedha wa kanisa hilo, Gayo Mhila amesema lengo la harambee hiyo ni kukusanya Sh350 milioni kwa kipindi cha miezi mitatu kwa ajili ya kuweka msingi wa kanisa hilo ambalo wanatarajia likamilike ndani ya miaka miwili.