Haya hapa yanayomsubiri Dk Migiro ofisi ya Katibu Mkuu

Dodoma/Dar. Wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kikimtangaza Balozi Dk Asha-Rose Migiro kuwa Katibu Mkuu wake mpya, wadau mbalimbali wametaja majukumu makubwa yanayomsubiri kiongozi huyo, likiwamo la kuirejesha imani ya chama hicho kwa wanachama na wananchi wasio wanachama.

Miongoni mwa mambo yanayobainishwa kama kibarua kikubwa kwa Dk Migiro ni namna ya kwenda sambamba na kasi ya siasa za sasa, ambazo kwa kiasi kikubwa zinatawaliwa na nguvu na ushawishi wa vijana.

Aidha, wadau wa kidiplomasia kwa upande wao wanasema uteuzi huo ni sawasawa na CCM “kulamba dume,” wakieleza kuwa uzoefu wa Dk Migiro katika uongozi na diplomasia, unampa nafasi ya kipekee ya kukiongoza chama hicho katika mazingira ya kisiasa yanayobadilika kwa kasi kubwa.

Katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma Agosti 23, 2025 chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, wajumbe walimpendekeza  Dk Migiro kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Uteuzi huo umefanyika kufuatia aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk Emmanuel Nchimbi, kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Rais Samia katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano, Oktoba 29, mwaka huu.

Dk Migiro anarejea tena katika Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM, safari hii akiwa Mtendaji Mkuu wa chama, baada ya awali kuhudumu kama Katibu wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa.

Kibarua cha Dk Migiro hiki hapa

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumapili Agosti 24, 2025, mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Ali Makame amesema jukumu la Dk Migiro kwa sasa ni kuhakikisha chama chake kinarejea kushika dola na kurejesha imani ya chama hicho kwa wanachama wake pamoja na wasiokuwa wanachama.

“Faida kubwa anayopata Dk Migiro kuiongoza CCM ni misingi imara iliyotengezwa awali na chama chake ambayo itamuwezesha kukiongoza kwa ufanisi na kushirikiana na watu wengine,” amesema Profesa Makame.

Aidha, mchambuzi huyo amebainisha kuwa Dk Migiro anashikilia wadhifa huu wakati ambao CCM inapaswa kujibu hoja na sio kuikosoa Serikali.

Amesema ingawa katibu mkuu huyo mpya ana uzoefu mkubwa ndani na nje ya nchi, uteuzi wake umekuja katika kipindi ambacho vyama vya siasa bado vinajijenga.

Hivyo, changamoto kubwa ni kipindi cha uchaguzi, ambapo tayari chama chake kimeshateua wagombea mbalimbali wa nafasi ya ubunge n udiwani.

“Hiki ni kipindi ambacho uzoefu wake wa kidiplomasia unahitajika, kwa sababu mifumo ya chama na uchaguzi mkuu inabadilika kwa kasi. Ndani ya chama, Dk Migiro atahitajika kukijenga chama kinachopaswa kusaidia maendeleo ya Taifa na wananchi,” amesema Profesa Makame.

Akiunga mkono hoja za mchambuzi wa awali,  Profesa Mohamed Bakari mchambuzi pia wa masuala ya siasa ameiambia Mwananchi kuwa majukumu yanayomsubiri Dk Migiro itategemeana na dhamira ya waliomteua kushika nafasi hiyo, huku akimpa pole na hongera kwa uteuzi huo.

Profesa Bakari amempa pole kiongozi huyo akisema amepokea majukumu makubwa wakati ambapo sura ya siasa za Tanzania na hali ya demokrasia haipo katika hali nzuri.

“Hakuna historia inayoonyesha kama ni mchafu kisiasa, sijui kama atakuja kufanya siasa achafuke kama walivyochafuka wengine au ameteuliwa kuja kukikomboa chama kwa kuanzisha mwelekeo mpya wa siasa za CCM,” amesema mchambuzi huyo.

Akimzungumzia mtangulizi wake, Dk Emanuel Nchimbi, Profesa Bakari amesema alijitahidi kulinda heshima yake kwenye majukumu hayo kutokana na kujizuia kuzungumza mara kwa mara, akisema kuwa Dk Migiro pia anaweza kufuata nyayo hizo ili asichafue jina lake kwa siasa za majukwaani.

Profesa huyo amesema Dk Migiro anaweza kufuata nyayo za aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula ambaye alijitenga na siasa chafu.

“Kuna namna anaweza kujiepusha na siasa za majukwaani akafanya kazi za utendaji zaidi kama ilivyokuwa kwa mzee Mangula, japo namhurumia katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na siasa chafu na kudorora kwa demokrasia kwenye mfumo wa vyama vingi,” amesema profesa huyo.

Majukumu mengine yanaomsubiri  Dk Migiro yameelezwa na Mhadhiri wa vyuo vya Diplomasia, Dk Elifuraha Ole Lalkaita ambaye amesema uteuzi wa msomi huyo ni hatua ambayo ameiona kama CCM kimelamba dume.

Dk Ole Lalkaita ametaja faida tatu kubwa zinazotarajiwa kutokana na uteuzi wa Dk Migiro kwamba akifanya vema, atasaidia kupandisha hadhi ya chama chake kwenye anga za kimataifa.

Pili, diplomasia yake itasaidia kuweka mlengo sawa wa mawazo ndani na nje ya Tanzania. Na la tatu, Dk Migiro amesema ni mtu mwenye utulivu ambaye hana malengo binafsi, bali amejitolea kwa ujenzi wa diplomasia na amani.

Mwanadiplomasia huyo ameongeza kuwa anaamini Dk Migiro si mtu wa tamaa wala kufanya mambo kwa kukurupuka.

Akizungumzia hoja ya kufanya kazi na watu wa kada tofauti, Dk Ole Lalkaita amesema haoni kama kuna changamoto, “Nina imani Dk Migiro kama mtendaji mkuu, atakuwa mwalimu mzuri kwa wale walio chini yake na watalazimika kuiga mtindo wake wa utendaji kazi ambao ni chanya.”

Kwa upande wake, Deus Kibamba amesema hana mashaka na uwezo wa Balozi Migiro, akibainisha kuwa amefanya naye kazi nyingi na kwa sehemu kubwa alikuwa mfano wa kuigwa.

Moja ya kazi aliyoitaja Kibamba ni kuhusiana na uandishi wa Dira ya Taifa, ambayo walishirikiana naye tangu mwanzoni mwa mwaka jana.

Hata hivyo, Kibamba amesema anaamini CCM imepata mtu sahihi kwa wakati sahihi.

“Ila najua atakutana na siasa za mchakamchaka, lakini zinazohitaji akili sana. Huyu mama anaweza kuhimili yote na waliompa nafasi hawatajuta,” amesema Kibamba.

Kada wa Chaumma, Kayumbo Kabutali, amempa pole Dk Migiro akibainisha kuwa nafasi aliyopewa haihitaji diplomasia pekee, bali vitendo zaidi.

Kabutali amesema siasa za majukwaani katika kipindi hiki ni tofauti na zile alizozifahamu Dk Migiro na hakuna jukwaa la siasa linalohitaji itifaki pekee.

Ameongeza kuwa atapaswa kuendana na kasi ya vijana ambao wamechukua siasa za sasa. “Sina shida na uadilifu na uzoefu wake, isipokuwa kizazi cha Gen Z lazima akubaliane nacho; hawa ni maji ya moto, dakika mbili wanabadilika, ukija na diplomasia zako utakwama,” amesema Kabutali.

Mmoja wa wateule wa ubunge ambaye aliomba hifadhi ya jina lake, amesema kuwa nafasi hiyo ya Dk Migiro inaweza kumpa changamoto mitandaoni na kuharibu heshima yake.

Mteule huyo amemuelezea Dk Migiro kuwa ni mtu mtulivu ambaye angeweza kumaliza utumishi wake na kubaki kuwa mshauri wa masuala yote yanayohusiana na chama na Serikali, kuliko huku alikotumbukizwa.

“Binafsi sikutarajia kama chama changu kingempatia huyu mama nafasi hiyo hasa katika nyakati hizi za siasa za mitandaoni. Vijana wamevurugwa, dakika moja tu, wanakuharibia  CV  (wasifu) yako, nasema hivi kwa kuwa tunayaona, daktari simuoni katika mikikimikiki hii, ila muda ni mwalimu,” amesema.