AWALI ilielezwa kiungo raia wa Uganda, Khalid Aucho alikuwa mbioni kumfuata swahiba wake, Kennedy Musonda huko Israel alikoenda kucheza soka la kulipwa baada ya kumaliza mkataba na Yanga, lakini mwamba huyo alibadilisha gia angani.
Aucho aliyeitumikia Yanga kwa misimu minne mfululizo, alimaliza mkataba na Yanga mwishoni mwa msimu uliopita na ilidaiwa alikuwa tayari kumfuata Musonda, huku akihusishwa pia na Simba, lakini ghafla aliamua kutua Singida Black Stars inayonolewa na Miguel Gamondi.
Inadaiwa kiungo huyo nyota wa kimataifa wa Uganda, alisainishwa mkataba wa miaka miwili ili kuitumikia timu hiyo inayojiandaa na michuano ya Kombe la Kagame 2025 itakayofanyika jijini Dar es Salaam kati ya Septemba 2-15 na hivi unavyosoma tayari ameanza rasmi kazi kikosini.
Aucho ni kati ya wachezaji wapya w Singida wanaoendelea kujifua kwa ajuili ya maandalizi ya msimu ujao wa mashindano ikiwamo Kombe la Kagame 2025 inayotarajiwa kuanza Septemba 2-15, jijini Dar es Salaam, timu hiyo ikiwa moja ya zitakazoshriki.
Singida Black Stars imepata nafasi ya kushiriki Kagame Cup baada ya wakongwe Simba na Yanga kujitoa kutokana na kubanwa na ratiba.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Singida Black Stars kimeliambia Mwanaspoti, Aucho ameshaanza kujifua na timu hiyo ambayo imeweka kambi Arusha na mapema wiki ijayo itakuwa Dar es Salaam.
“Aucho yupo kambini na ameanza mazoezi kujiweka tayari na michuano iliyo mbele ambayo mapema mwezi ujao watashiriki Kagame michuano hiyo itakuwa sehemu ya maandalizi kwa ajili ya michuano msimu mpya na michuano ya kimataifa,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Kuwahi kujiunga kwa kiungo huyo kumeongeza hari ya ushindani na ubora ndani ya kikosi kilichonchini ya kocha mwenye uzoefu wa ligi akiiwa na mafanikio makubwa ndani na kimataifa.”
Mtoa taarifa huyo alisema michuano ya Kagame pia itakuwa sehemu ya utambulisho wa wachezaji wao wapya baada ya kuhairishwa kwa tamasha la Singida Big Day lililokuwa limepangwa kufanyika Septemba 6.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa habari wa Singida, Hussein Massanza alisema kuhairishwa kwa tamasha la Singida Black Stars imetokana na ratiba ngumu iliyo mbele yao.
“Tunawaomba radhi wana Arusha ambao walikuwa wana shahuku kubwa kuiona Singida Black Stars lakini tumesitisha kutokana na ufinyu wa ratiba tuna matukio mengi mwezi ujao tunathibitisha tukio hilo rasmi,” alisema Massanza na kuongeza;
“Singida Black Stars ni kati ya timu zitakazoshiriki Kagame Cup tunawaomba radhi wana Arusha kutokana na ufinyu wa ratiba tunaenda kujiimarisha zaidi katika mashindano tuliyoalikwa kuanzia Septemba 2 ndio sababu ya ufinyu wa ratiba.”
Massanza alisema sasa watatoa taarifa juu ua namna gani watatangaza kikosi chao kipya cha msimu ujao baada ya kuhairishwa kwa tamasha lao ambalo ndio mahususi kwa kutangaza kikosi chao kipya kwa kila msimu.