‘Kuwarudisha vijana kundini, kibarua kinachomsubiri Kihongosi’

Dodoma. Siku moja baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kumtangaza aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenan Kihongosi kuwa Katibu wa Itikadi, Siasa, Uenezi na Mafunzo, watu mbalimbali wametaja jukumu kubwa linalomsubiri.

Hata hivyo, wachambuzi wa mambo wamemtaja kuwa chaguo sahihi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 29, 2025 ukizingatia hakuwa sehemu ya mchakato wa upitishaji majina ya wagombea ubunge, hivyo hawezi kuwa na upande.

Kihongosi amechukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Amos Makalla ambaye naye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Moja ya kazi inayotajwa kumsubiri ni mkakati wa kurudisha mawasiliano ya chama kwa kundi la vijana ambayo kwa kiasi kikubwa yalianza kupotea.

Mbali na mawasiliano hayo kupitia mitandao ya kijamii, Kihongosi anapaswa kuwa namba moja kwenye majukwaa kutokana na mabosi wake Katibu Mkuu wa CCM na Naibu wake kuwa na umri unaoonyesha mwendo wa mchakamchaka kwao utakuwa mgumu.

Kihongosi aliteuliwa Juni 25, 2025 kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha akitokea Simiyu ambako alikuwa mkuu wa mkoa huo.

Hata hivyo, Arusha inakuwa kete ya kutokea kwa Kihongosi ambaye aliwahi pia kuhudumu kama mwenyekiti vijana wa CCM Mkoa wa Iringa ambako nyota yake ilianzia kung’ara.

Akimzungumzia Kihongosi, Mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja amemtaja kama chaguo sahihi kwa wakati huu kulingana na hali ya kisiasa nchini.

Mgeja amesema Kihongosi haendi kujifunza jambo jipya ndani ya Sekretarieti kwa sababu alishahudumu kwenye nafasi hiyo.

Amesema kwa kipindi hiki nafasi ya mwenezi inahitaji kiongozi kijana mwenye maono ambaye anaweza kufanya siasa za mchakamchaka zisizohitaji kupoa.

“Huyu mtu namfahamu, niseme kwamba chama hakijakosea kumpa nafasi hiyo maana anaweza na atatufaa sana kwa wakati huu,” amesema Mgeja.

Hata hivyo, amesema kazi itakuwa ngumu kama hatapewa ushirikiano na makundi ya wanaCCM hasa vijana.

Kada wa CCM, Livingston Lusinde amesema kabla ya yote, Mwenezi huyo anapaswa kuamsha kundi la vijana ili wasimame imara na wawe tayari kujitokeza katika kipindi cha kampeni na hata siku ya kupiga kura.

Lusinde, maarufu ‘Kibajaji’ amesema kwa sasa CCM imefikia pazuri na mkakati uliowekwa na Sekretarieti ulionyesha uimara lakini mvuto wa kundi la vijana unatakiwa uongeze nguvu kubwa.

“Siku zote jeshi lenye amshaamsha wakati mwingine huwa linashinda vita hata kabla ya kuingia katika uwanja wa mapambano, huyu naamini atatuvusha kwenye kundi la vijana,” amesema Kibajaji.

Amefafanua kundi la vijana kuanzia majukwaani na kwenye mitandao ya kijamii linahitaji kuamshwa kazi anayoamini inawezekana kwa mwenezi huyu mpya.

Kuhusu majukwaa ya vyama vingine, anamtaja Kihongosi kama jasiri wasiye na mashaka naye kwamba anaweza kukabiliana na mikikimikiki yote kutoka kwa watu tofautitofauti.

Katibu Mkuu wa chama cha UMD, Moshi Kigundula amesema hakuna jipya ambalo atakuja kuongoza Kihongosi kutokana na ukweli kuwa chama hicho kimefika mwisho katika kufikiri.

“Katibu amesema kundi walilolilenga CCM ni vijana, lakini wanasahau kuwa sera zao zimefikia mwisho na hawawezi kuaminika hata wakichagua malaika,” amesema Kigundula.