CHAN 2024: Sudan, Algeria vita ilikuwa kati

WANAUME 22 kutoka Sudan na Algeria, walizimwagilia vizuri nyasi za Uwanja wa Amaan Complex, visiwani Zanzibar katika mchezo wa robo fainali wa michuano ya CHAN uliopigwa juzi.

Katika mchezo huo ambao dakika 120 zilimalizika kwa timu zote kutoshana nguvu ya kufungana bao 1-1, vita kubwa ilionekana eneo la kati ambalo kwa kiasi kikubwa liliamua mechi hiyo kumalizika sare.

Sudan ambayo ilikuwa inacheza robo fainali yake ya nne, ilisonga mbele baada ya kushinda penalti 3-2 dhidi ya Algeria ambayo ilionekana kutawala vyema mchezo huo.

Vilevile hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Algeria kupoteza mchezo wa robo katika mara zote ilizowahi kufika hatua hiyo.

Hapa chini tumekuwekea uchambuzi juu ya dakika zote 120 za mchezo huo.

SUDA 01


Moja ya maeneo Sudan ilifanikiwa kuikamata Algeria ilikuwa ni eneo la kiungo na Salah Eldini muda mwingi alikuwa akikimbia nyuma ya viungo wa Algeria sehemu ambayo alikuwa akipokea mipira, pia alikuwa akifika kwa wakati mara zote ambazo viungo wa Algeria walikuwa na mpira.

Hiyo ilisababisha muda mwingi Algeria kushambulia kutokea pembeni kwa Mohamed Halaima upande wa kushoto pamoja na Mohamed Khacef waliokuwa wanabadilika kuwa mawinga au mabeki wa pembeni katika mfumo wa 3-5-2.

Licha ya kushambulia kutokea pembeni, bado Algeria haikufanikiwa katika mipango yao hali iliyosababisha kocha Madjid Bougherra wa Algeria kumtoa Bilel Boukerchaoui na kumuingiza Mehd Merghem ambaye alipoingia alikuwa akishambulia zaidi kupitia pembeni mahali ambako kocha wao aliona panaweza kuwapatia chochote.

SUDA 03


Ubora wa eneo lao la kiungo ulichagizwa sana na Eldin pamoja na Abdelrazig Taha na hata kocha wa Algeria katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi alikiri ndiyo walikuwa wakimpa changamoto sana.

Hata hivyo, kwa bahati mbaya Eldin alipata majeraha ya kichwa na baade akafungwa bandeji lakini bado ilishindikana kuendelea.

Kutoka kwa Eldini ilikuwa kama anguko kwa Sudan kwani uwepo wake kwanza ulikuwa ukisaidia kusimama kama kiungo wa chini kuzuia mashambulizi, pia alikuwa akipanda kutengeneza mashambulizi pamoja na kuhakikisha viungo wa Algeria hawapati utulivu wanapokuwa na mpira mguuni.

Algeria ilitumia mwanya wa kukosekana kwa Eldini vizuri na ikawa inashambulia kwa vipindi pamoja na kupokezana na Sudan.

Kocha wa Sudan, James Appiah baada ya mechi alikiri wazi kuumia kwa Eldin ilikuwa pigo kwa timu yake.

“Uliona Eldin alipoumia, eneo letu la kiungo halikuwa kama vile lilivyokuwa awali, tulipoteza mipira kwa kiasi kikubwa, Algeria pia ilipata utulivu kwenye eneo la kiungo.”

SUDA 04


Licha ya ukweli safu zote za ushambuliaji hazikuonyesha ubora mkubwa sana, pia nafasi chache ambazo washambuliaji wa timu zote  walizipata hazikuzaa matunda kutokana na ubora ambao makipa wote waliuonyesha.

Mohamed Alnour kwa upande wa Sudan aliokoa zaidi ya hatari nne zilizoonekana kuwa mabao.

Vivyo hivyo, kwa kipa wa Algeria, Zakaria Bouhalfaya mikono yake ilifanya kazi ya ziada kuhakikisha timu inabakia katika sehemu salama hadi dakika 120 zinamalizika.

Hata hivyo, mwisho wa mechi Alnour aliibuka mchezaji bora wa mchezo na kuwa shujaa mbele ya Zakaria.

Baada ya kupata bao la kusawazisha wana fainali hawa wa fainali zilizopita waliendelea kushambulia zaidi lakini ilikuwa ni kupitia pembeni hasa kushoto kwa Meghreb.

Changamoto kubwa ilikuwa ni idadi ndogo ya washambuliaji wao katika eneo la mwisho.

Aimen Mahious pamoja na Abdennour Belhocini hawakuwa wakifanya mikimbio ya kuingia kwenye boksi, muda wote walikuwa mbele ya mabeki wawili wa kati wa Sudan na mara chache ambazo walikuwa wakiingia walikuwa wakichelewa.

Hii ilisababisha krosi na mipira mingi ya Algeria iliyofika katika boksi la Sudan kukosa uhatari kwa sababu haikuwa inachezewa katika lango la Sudan, pia hata ilipokuwa hapo washambuliaji wa kumalizia hawakuwa eneo husika kwa muda sahihi.

SUDA 06


Kocha wa Sudan, James Appiah baada ya mchezo alisema:”Ilikuwa ni mechi nzuri kwetu, jambo la kwanza lililokuwa kwenye vichwa vyetu ilikuwa ni kuwaheshimu kwanza Algeria, tulifahamu hatutoweza kwenda na kupishana nao moja kwa moja ilitakiwa tuwe na mpango mkakati ikiwa tutashindwa kupata matokeo katika dakika za kawaida. Tulijua penalti hazina mwenyewe, hivyo kupitia huko tungekuwa na nafasi ya kufanya kitu.”

“Tulipata tabu katika eneo letu la kati baada ya kuumia kwa Eldin lakini siku zote lazima uwe na mbinu tofauti tofauti kuhakikisha unapambana na kila hali. Niliungana na hii timu siku tatu kabla ya mashindano na kwa hiki wanachokifanya kwangu ni jambo kubwa sana, niwapongeze kwa kujitoa.”

“Najua mechi ijayo itakuwa ngumu lakini tutajaribu kupambana kadri inavyowezekana kuhakikisha tunasonga mbele.”

SUDA 05


SUDA 05

Kwa upande wake kocha wa Algeria alisema:

“Niseme nashukuru Mungu kwa matokeo haya, wachezaji wangu walipambana sana. Sudan ilikuwa na wachezaji wazuri sana katika eneo lao la kiungo hususan, namba 15 na namba nane, walifanya viungo wetu wasipande muda mwingi wa mchezo kiasi cha mchezaji kama Bilal Boukerchaoui kulazimika kushuka sana, alikuwa anashindwa kukaa kwenye eneo lake na muda mwingi alishuka chini kwa ajili ya kwenda kuchukua mipira.”

“Hiyo ilisababisha tupotee kabisa katika eneo la kati ndiyo maana tukachukua jukumu la kumtoa na kumwingiza Mehdi Meghreb.”

“Tulikuwa na muda mchache wa kujiandaa na kufika hapa Zanzibar, lakini hicho hakiwezi kuwa kisingizio. Yote kwa yote, hakuna wa kumlaumu.  Wachezaji wangu walicheza na kujitoa kwa asilimia mia.”

SUDA 02


2. Imeruhusu mabao mawili tu hadi sasa katika michuano hii(katika dakika 120).

3. Imecheza robo fainali yake ya nne na haijawahi kupoteza hatua hii, ilishinda mbele ya Niger kupitia penalti mwaka 2011  na  ikatoa Zambia kwa bao  1-0 mwaka 2018 pamoja na leo dhidi ya Algeria.

4. Itaenda kucheza nusu fainali kwa mara ya tatu baada ya kufanya hivyo mwaka 2011 na 2018.

5. Katika mechi za mtoano imeshinda mara nne na kufungwa mara tatu kati ya mechi saba.

6. Mechi pekee iliyoshindwa kufunga bao tangu ianze kushiriki michuano hii ilikuwa ni nusu fainali dhidi ya Nigeria mwaka 2018.

7. Imeshinda mechi yake ya pili kati ya saba zilizopita ilizocheza katika michuano yote.

1. Baada ya mechi ya leo inakuwa imetoka sare kwenye mechi nne zilizopita (katika dakika 90) ndiyo rekodi yao ya kucheza mechi nyingi zaidi bila ushindi kwenye muda wa kawaida.

2. Hii inakuwa ni mechi yao ya kwanza kupoteza katika mechi  11 mfululizo.

3. Kichapo cha mwisho kwenye michuano hii kilikuwa dhidi ya Sudan kwenye mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu mwaka 2011 na leo imechapwa tena.

4. Haikuwa imeruhusu bao katika mechi nane kati ya 10  zilizopita.

5. Ilikuwa ni robo fainali yao ya tatu; Mbili zilizopita  ilishinda zote dhidi ya Afrika Kusini mwaka 2011, dhidi ya Ivory Coast mwaka 2022).

6. Kabla ya mchezo huu, haikuwahi akupoteza robo fainali kwenye michuano hii, ilikuwa imeshinda zote na bila kuruhusu bao.

7. Hii ni mara ya kwanza Algeria kutolewa mapema kwenye michuano ya CHAN katika mara zote ilizoshiriki.

8. Katika mechi saba za mtoano ilizocheza kwenye michuano hii imeshinda tatu na kufungwa nne.

9. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Algeria kufika hadi hatua ya changamoto ya mikwaju ya penalti katika mechi ya mtoano ya michuano ya CHAN, mara zote ilikuwa ikimaliza ndani ya dakika 90.