BAADA ya kiungo mkabaji, Baraka Majogoro kuachana na Chippa United ya Afrika ya Kusini, mabosi wa Namungo na KMC aliyowahi kuichezea zimeonyesha nia ya kumhitaji, huku ikielezwa miamba hiyo inachuana kwa ajili ya kuipata saini yake.
Taarifa ambazo Mwanaspoti ilizozipata, zinaeleza KMC na Namungo zote kwa pamoja zimeonyesha nia ya kumhitaji na jambo kubwa linaloendelea kwa sasa ni kukubaliana masilahi binafsi, ili achague ni timu gani kati ya hizo atacheza msimu ujao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula alisema hadi sasa hakuna kinachoendelea kwa sababu tayari wameachia benchi la ufundi lifanye kazi yake, hivyo wao viongozi wanachosubiria ni mapendekezo yaliyopo.
“Sisi tulishamaliza usajili kitambo kwa sababu tulishakamilisha mahitaji yote ambayo yalipendekezwa na benchi letu la ufundi chini ya Kocha Adam Mbwana Mubesh aliyekuwa anashirikiana na Kocha Mkuu, Marcio Maximo,” alisema Mwakasungula.
Hata hivyo, licha ya kauli ya Mwakasungula, ila Mwanaspoti linatambua uongozi wa timu hiyo unapambana na menejimenti ya Majogoro ili kuipata saini yake na hii ni baada ya mabosi wa Namungo wanaomhitaji pia kurudi nyuma kiaina.
Mmoja wa kiongozi wa Namungo, aliliambia Mwanaspoti huenda wakajitoa katika vita ya kuiwania saini ya nyota huyo, baada ya usumbufu anaoendelea kuuonyesha, ingawa ni kweli wako katika mazungumzo kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi.
Nyota huyo wa zamani wa Tanzania Prisons, Ndanda, Polisi Tanzania na Mtibwa Sugar kwa sasa yupo huru baada ya kuachana na Chippa United aliyojiunga nayo Agosti 4, 2023, akitokea KMC inayoonyesha nia ya kumrejesha tena kikosini.