UONGOZI wa Fountain Gate uko katika mazungumzo ya kumsajili aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa JKT Tanzania, Ismail Aziz Kader, hivyo kuzipiku timu za Mbeya City, Tanzania Prisons na Pamba Jiji ambazo zote zilionyesha kumuhitaji.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa kikosi hicho, zimeliambia Mwanaspoti, Kader amekubaliana maslahi binafsi na tayari amepewa mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia timu hiyo kwa msimu wa 2025-26, hivyo hadi sasa kilichobakia ni kusaini.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Fountain Gate, Wendo Makau alisema msimu ujao wanataka kufanya mambo makubwa zaidi tofauti na uliopita, hivyo hadi sasa kuna majina ya nyota wapya ambao wanaendelea na mazungumzo nao na watayaweka wazi.
“Kilichotokea msimu wa 2024-2025 hatutaki kukiona kikitokea tena kwa 2025-2026, ni kweli tumefanya usajili mkubwa ambao tunaamini utatusaidia, tumezingatia ubora wa wachezaji katika kuwachagua na muda ukifika tutawatangaza,” alisema Wendo.
Wendo alisema msimu uliopita wa 2024-2025, umekuwa ni kipimo sahihi kwao cha kujifunza kutokana na makosa yaliyojitokeza hivyo, presha waliyopitia ya kuinusuru timu hiyo hawataki ijirudie, ndio maana wanataka kukisuka tena upya kikosi hicho.
Nyota huyo aliyewahi kuichezea pia Azam FC, amekubali kujiunga na Fountain Gate baada ya kupewa ofa nono tofauti na zile za Mbeya City, Tanzania Prisons na Pamba Jiji, ambazo zilionyesha nia ya kumuhitaji kabla ya kuzidiwa ujanja wa kifedha.