Mabula aendelea alipoishia Azerbaijan | Mwanaspoti

KIUNGO wa Shamakhi FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Azerbaijan, Alphonce Mabula amesema ligi ya nchi hiyo imeanza kwa kasi na mechi ya kwanza walitoka sare ya 1-1.

Mabula ambaye alijiunga na Shamakhi kwa nusu msimu akitokea FK Spartak Subotica ya Ligi Kuu Serbia alikocheza kwa misimu miwili, alisema tofauti na msimu uliopita, msimu huu karibu timu zote zimejiandaa kuonyesha ushindani kwani mechi ya kwanza waliyotoka sare imeonyesha hilo.

Aliongeza, kutokana na ubora wa ligi hiyo, baadhi ya timu zimesajili wachezaji kutoka ligi kubwa kama Ufaransa.

“Ni kupambana tu, maana hata kwenye timu wameongeza wachezaji wakubwa. Ukilegea basi kupata nafasi ndiyo basi tena. Tulicheza mechi ngumu sana wiki iliyopita na timu kubwa,” alisema na kuongeza:

“Timu iko vizuri kwangu kama mchezaji. Mbali na malengo ya timu, binafsi nataka kuendelea kuonyesha ubora na niendelee nilipoishia msimu uliopita.”

Msimu uliopita alicheza nusu msimu kwenye mechi 17, akifunga mabao matatu na kuisaidia Shamakhi kumaliza nafasi ya saba kati ya 10 zilizoshiriki ligi hiyo.