Ligi Kuu Zanzibar kuanza Septemba 20

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), limetangaza kwamba, Ligi Kuu Soka Zanzibar (ZPL) msimu wa 2025-2026 inatarajiwa kuanza Septemba 20, 2025.

Ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 ambapo 12 za Unguja na 4 kutoka Pemba huku bingwa mtetezi ikiwa Mlandege FC, inatarajiwa kufikia tamati Mei 31, 2026.

Wakati ligi ikianza Septemba 20, mchezo wa Ngao ya Jamii kuashiria kufunguliwa kwa msimu wa 2025-2026 visiwani hapa, utachezwa Septemba 13 kati ya bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2024-2025, Mlandege na bingwa wa Kombe la FA, KMKM.

Katika ligi hiyo, timu ya New King itashiriki kwa mara ya kwanza kufuatia kupanda daraja, huku Polisi ikirejea baada ya kushuka misimu miwili iliyopita. Zingine zilizopanda ni New Stone Town na Fufuni zikitokea kisiwani Pemba.

Msimu uliopita ilishuhudiwa timu nne zikishuka daraja ambazo ni New City, Mwenge, Tekeleza na Inter Zanzibar. Wakati huohuo, Mwembe Makumbi na Junguni zikiendelea na safari katika ligi hiyo kufuatia kupanda daraja na kubaki ikiziacha Tekeleza na InterZanzibar zikishuka.

Timu 12 za Unguja zitakazoshiriki ligi hiyo ni Mlandege, KVZ, Mafunzo, Mwembe Makumbi, JKU, Uhamiaji, Zimamoto, Malindi, KMKM, Kipanga, Polisi na New King.

Zinazotokea Pemba ni Junguni United, Chipukizi United, Stone Town na Fufuni.