HADITHI: Bomu Mkononi (Mwisho) | Mwanaspoti

“SASA nitapata wapi huduma hizi?”

Musa aliponiuliza hivyo nikanyamaza kimya. Baada ya muda kidogo nikamwambia:

“Ungekuwa na ndugu yako mwanaume angekusaidia. Mimi mwanamke inakuwa ni taabu kuwa kwenye wodi hii ya wanaume.”

Musa alitoa pesa kutoka kwenye begi lake alilokuwa ameliweka mchangoni mwa kitanda chake.

“Hizi pesa utatumia,” akaniambia.

Nilitaka nimuachie lakini nikaona nizichukue, angeweza kuniuliza nimepata wapi pesa za kutumia.

“Asante,” nikamwambia.

“Hii miguu itaniweka kitandani kwa muda mrefu,” Musa aliniambia kwa kusikitika na kuongeza:

“Huu mguu mmoja umevunjika sehemu mbili na unaniuma sana.”

“Upi? Huu uliofungwa bendeji ngumu au ulioning’inizwa?”

“Huu ulioning’inizwa.”

“Umeambiwa utakaa kwa muda gani hapa?”

“Sijaambiwa lakini nahisi nitachukua muda mrefu.”

Nikajisema kimoyo moyo, kama Musa ataendelea kuwepo hapo hospitalini kwa muda mrefu inaweza kugundulika kuwa ni mume wangu.

“Baadaye utamuita ndugu yako aje akuhudumie hapa,” nikamwambia.

“Nimeshakuelewa, ndiyo nilikuwa nafikiria ndugu yangu yupi nimuite. Hadi sasa hakuna ndugu yeyote aliyefika hapa.”

“Basi kaniletee chai.”

“Nitapata wapi chupa?”

“Tena itabidi kesho uje na chupa ikae hapa. Kwa leo nitaazima kwa mwenzangu yeyote.”

Musa akaazima chupa kwa majeruhi mwenzake aliyekuwa amepakana naye.

“Ninunulie vikombe viwili vya chai ya maziwa.”

“Ulihitaji chai na kitafunio gani?”

“Vitumbua au chapati.”

Nikaondoka kwenda kumnunulia chai. Nilinunua vikombe viwili vya chai ya maziwa na vitumbua vinne nikampelekea.

Nilimsubiri anywe chai. Alipomaliza nilikwenda kuosha kikombe nikakirudisha kwa mwenyewe, kisha nikamuaga Musa.

“Utahitaji chakula mchana?” nikamuuliza.

“Mchana nitajinunulia hapa hapa. Wewe niletee jioni.”

“Naweza hata kumuagiza muuguzi, watu wako wengi.”

“Na hapo jioni ungependa chakula gani?”

“Niletee ndizi kwa nyama.”

Kutoka siku ile nikawa nimepata kibarua cha kwenda Muhimbili kila siku asubuhi na jioni kumhudumia Musa. Siku zikapita. Kila baada ya siku tatu nilikuwa naenda Ilala kwa Sele kisha napitia Kimara kwa Musa.

Chakula nilichokuwa nampelekea Musa nilikuwa nakipika nyumbani kwa Mustafa, na Mustafa ndiye aliyekuwa anakinunua bila kujua kuwa alikuwa akimnunulia chakula mume mwenzake.

Baada ya kupita wiki mbili nilipata msaidizi. Mdogo wake Musa aliyekuwa akiishi Chanika akachukua nafasi yangu. Yeye naye alianza kumhudumia kaka yake. Kwa hiyo kulikuwa na siku ambazo nilipumzika kwenda hospitali.

Kulikuwa na siku moja nikamdanganya Mustafa kwa kumuaga safari ya kwenda Tanga kumjulia hali shangazi yangu. Mustafa alinikubalia akanipa nauli ya kwenda Tanga na kurudi.

Nilipoondoka nyumbani nilikwenda Ilala kwa Sele. Nikalala kwa siku mbili huku nikimpigia simu Mustafa nikijifanya niko Tanga.

Pia sikumsahau Musa. Na yeye nilimpigia nikamwambia kuwa nilishindwa kwenda kumjulia hali kwa sababu nilikuwa naumwa.

“Una nini?” akaniuliza kwa wasiwasi.

“Nafikiri ni malaria. Kichwa kinaniuma na mwili pia unauma.”

“Umekwenda hospitali?”

“Sijakwenda, nimemeza dawa tu.”

“Basi pumzika, mdogo wangu yuko atanisaidia.”

“Nikiona sipati nafuu nitakwenda hospitali.”

“Sawa. Rama hajambo?”

“Hajambo, anakusalimia.”

Rama sikuwa naye, nilimuacha Mbezi. Ikabidi niseme uongo mwingine.

“Rama yuko nje na wenzake wanacheza,” nikamwambia.

“Utakapokuja uje naye.”

“Nikipata nafuu nitakuja naye kesho.”

Baada ya kuzungumza hayo na Musa nikakata simu.

Wakati huo Sele alikuwa bado yuko Marerani. Sikutaka kupitisha muda mrefu bila kufika pale nyumbani kwake ili nisimtie wasiwasi yule mtumishi wetu.

Baada ya siku mbili niliondoka, nikaenda kituo cha mabasi cha Mbezi ambako nilimpigia simu Mustafa.

“Niko kituo cha mabasi cha Mbezi naomba uje unichukue,” nilimwambia Mustafa baada ya kupokea simu.

“Ndio umerudi kutoka Tanga?” Mustafa akaniuliza.

“Ndio, tumewasili muda huu.”

“Mbona hukunijulisha kuwa unakuja?”

“Nilijisahau, njoo bwana nakusubiri.”

“Usinisubiri, tafuta usafiri mwingine uende nyumbani.”

“Ke! Kwanini unaniambia hivyo?”

“Mimi niko Bagamoyo kwa mama, nitarudi jioni.”

“Vipi hali yake, hajambo?”

“Hajambo, nilikuja kumsalimia tu.”

“Sawa, basi nitachukua teksi niende nyumbani.”

“Chukua tu, mimi nitarudi jioni.”

Badala ya teksi nilikodi bodaboda iliyonipeleka nyumbani kwa Mustafa.

Nilipata hisia kuwa hata yule mtumishi wetu wa hapo Mbezi alikuwa hanielewi, sema alishindwa kuniuliza kuhusiana na nyendo zangu.

Lakini kama hakuwa akinielewa, hilo sikulijali. Nilichojali ni kuwa asitoe siri yangu kwa Mustafa. Hilo ndilo lililonifanya nijipendekeze naye sana ili anione kama dada yake au kama rafiki yake.

Jioni ya siku ile nilimchukua Rama nikaenda naye Muhimbili. Musa alipomuona alifurahi sana, akazungumza naye kwa muda mrefu. Alikuwepo pia shemeji yangu, mdogo wake Musa ambaye alikuwa akinisaidia kumletea chakula Musa pamoja na kumhudumia asubuhi na jioni.

“Unajisikiaje kuumwa?” Musa aliniuliza baada ya kuzungumza na Rama.

“Leo sijambo kidogo, ndiyo maana nimeweza kuja.”

“Yule kaka yako ameshaondoka?”

Musa aliniuliza hivyo akimaanisha Mustafa.

“Yule si yuko Tanga, anakuja mara moja moja tu,” nikamdanganya.

“Kwa hiyo amesharudi Tanga?”

“Ndio maana sijamuona tena.”

“Ameniambia atakuja siku hizi hizi, akija kama bado utakuwa hospitali atakuja kukusalimia.”

Musa akanipa pesa za matumizi.

“Jana waliniletea mshahara wangu,” akaniambia.

“Sasa si ungenipa nikakuwekee nyumbani?”

“Hapa hospitali nitatumia nini? Hizi pesa ndizo zinazonisaidia, nikitaka kitu naagiza.”

“Basi nipe nitakazotumia mimi na mtoto.”

“Ndio hizo nilizokupa, au ni kidogo?”

Nilitaka nimwambie ni kidogo lakini niliona aibu kwa vile mdogo wake alikuwa yuko karibu.

Tukaendelea kuzungumza hadi muda wa kutazama wagonjwa ulipoisha, nilimuaga Musa na mdogo wake nikaondoka na mwanangu.

Rama alikuwa bado mdogo, hakuwa akijua kilichokuwa kinaendelea. Lakini niligundua kuwa alikuwa anatatizika kumjua baba yake halisi kati ya Mustafa na Musa. Kutokana na ule utoto wake alikuwa anashindwa kuuliza.

Tukarudi nyumbani Mbezi. Mustafa alikuwa hajarudi. Nikampigia simu.

“Uko wapi baba Rama?” nikamuuliza alipopokea simu.

“Si nilikwambia niko Bagamoyo.”

“Uko Bagamoyo hadi muda huu?”

“Hivi sasa ndio narudi.”

“Unapenda kusafiri usiku!”

“Mbona nitafika mapema tu.”

Wakati ule nazungumza na Mustafa kwenye simu nikaona simu ya Sele inataka kuingia. Nikaagana na Mustafa na kukata simu. Ndipo nilipopokea simu iliyokuwa inatoka kwa Sele.

Sele aliniuliza hali. Nikamwambia naendelea vizuri.

“Na wewe unaendeleaje huko?” nikamuuliza.

“Huku bado tunapambana lakini matumaini yapo.”

“Unatarajia kuja lini huku?”

“Siwezi kuwaachia hawa kwa sasa, kama wakitoa mzigo mimi sipo itakuwa imekula kwangu.”

“Kazi hizi za madini si za kuaminiana. Unaweza kulizwa mchana kweupe!”

“Kwa hiyo hutakuja hivi karibuni?”

Sikuwa nimemuuliza hivyo kimapenzi, nilimuuliza ili nijue kama atarudi hivi karibuni ili nijiandae kwa kazi ya kulea waume watatu, mmoja akiwa mgonjwa hospitali ya Muhimbili.

Nilipojua kuwa Sele hakuwa na mpango wa kuja hivi karibuni nikashukuru. Niliagana naye kwenye simu na kutoka chumbani nilimokuwa nikizungumza naye.

Juma lile lile nikapata taarifa ya msiba iliyonihuzunisha sana. Shangazi yangu kipenzi aliyekuwa akiugua huko Tanga, ahadi yake iliwadia. Nilipigiwa simu nikajulishwa kuwa shangazi yangu alikuwa amefariki dunia alfajiri. Nilipigiwa simu hiyo saa moja asubuhi.

NILIAMBIWA kwamba mazishi yatakuwa saa kumi jioni baada ya sala ya alasiri.

Nililia sana nilipopata taarifa ile. Nililia mpaka Mustafa alinihurumia kwani wakati napigiwa simu nilikuwa naye.

“Nyamaza, usilie sana. Utapata homa bure,” Mustafa alinambia.

Kilichonitia huzuni ni kuwa baba yangu na mama yangu walikuwa wameshakufa, shangazi yangu ndiye aliyekuwa kila kitu kwangu. Isitoshe sikuwa nimekwenda kumjulia hali siku za karibuni, zaidi ya kumdanganya Mustafa kuwa nimekwenda Tanga, kumbe nilikuwa hapo hapo Dar kwa Sele.

“Wamekwambia mazishi ni saa ngapi?” Mustafa akaniuliza.

“Atazikwa saa kumi jioni. Mimi nitakwenda hii asubuhi. Sijui nitapata basi gani?”

“Tutakwenda sote na gari ndogo. Wewe jiandae, mimi nakwenda kujaza mafuta.”

Mustafa alipoondoka na mimi niliondoka. Nilikodi teksi nikaenda Kimara kwa Musa. Nilimwambia mfanyakazi wetu kuwa nimefiwa na shangazi yangu Tanga.

“Oh pole dada, amekufa hii leo?”

“Amekufa alfajiri ya leo, atazikwa saa kumi jioni.”

“Sasa utawahi mazishi?”

“Nitawahi, nimekuja kukuachia nyumba. Nitakuwa huko kwa siku saba.”

Nilitoa shilingi elfu hamsini nikampa.

“Utatumia kidogo dogo mpaka nitakaporudi. Kumbuka baba Rama yuko hospitali. Nitamwambia kama atakuwa na tatizo akupigie simu.”

Ndipo nilipompigia simu Musa na kumjulisha kuhusu msiba wa shangazi yangu.

Musa alikuwa akimjua vizuri shangazi yangu kwani ndiye aliyesimamia shughuli zote za ndoa yetu.

Musa aliposikia kwamba shangazi amekufa alisikitika sana.

“Sasa itabidi uende peke yako, mimi sitaweza,” Musa akaniambia.

“Wewe baki tu, nitaenda peke yangu.”

“Unatarajia kuondoka saa ngapi?”

“Muda huu huu tu. Kama utakuwa na tatizo la nyumbani utampigia simu Mage, nimeshamwambia.”

“Sawa. Utarudi lini?”

“Tutafahamishana kwenye simu.”

Baada ya kuzungumza na Musa nilimuaga Mage nikaondoka pale nyumbani na kwenda Ilala kwa Sele.

Nilipofika nilimpigia simu Sele na kumjulisha kuwa nimefiwa na shangazi yangu.

“Na hivi ninaondoka, ninakwenda Tanga. Mazishi yatakuwa saa kumi jioni,” nilimwambia.

“Pole sana mke wangu, tatizo limetokea mimi niko huku lakini nitajitahidi nifike hata kama ni kesho.”

“Wewe endelea tu na kazi yako, utakuja kuhani siku nyingine.”

“Sasa wape taarifa nyumbani, mwambie Rukia (mdogo wake) aje akae hapo nyumbani mpaka utakaporudi.”

Nilipokata simu nilimfahamisha mtumishi wetu hali halisi, nikamwambia kuwa wifi yangu Rukia atakuja kukaa pale nyumbani mpaka nitakaporudi.

Baada ya hapo nikatoka nikaenda nyumbani kwa kina Sele. Niliwapa taarifa ya msiba kisha nikamwambia Rukia mdogo wake Sele aende akakae nyumbani kwetu hadi nitakaporudi.

Wakati natoka kwa kina Sele Mustafa akanipigia simu.

“Umekwenda wapi?” akaniuliza.

“Ninakuja, nimekuja kuwaarifu ndugu na jamaa.”

“Sasa njoo, nimeshajaza mafuta.”

Nikapanda tena teksi hadi Mbezi. Nilimkuta Mustafa akinisubiri.

“Sasa unywe chai tuondoke, safari ni ndefu.”

“Nitakwenda kunywa huko huko.”

“Hapana, kunywa kidogo. Sidhani kama tukifika huko utapata nafasi ya kunywa chai. Mimi nimeshakunywa.”

Nikanywa chai kidogo kisha nikachukua nguo na vitu nilivyotaka kuchukua, tukaondoka. Rama tulimuacha na mtumishi kwa vile Mustafa alipanga kurudi kesho yake.

Tulifika Tanga saa nane mchana.

Tukakuta msafara uliokuwa ukielekea kijijini kwetu kwa ajili ya mazishi.

Kijiji chetu kiko katika barabara ya kuelekea wilaya ya Pangani. Kiko mwendo wa kilometa ishirini kutoka Tanga mjini. Kwa vile tuliambiwa kuwa matanga yangekuwa pale pale nyumbani, tulikubaliana na Mustafa kuwa yeye ndiye aende akazike, mimi nibaki kutokana na taratibu zetu za Kiislamu, wanawake hawaendi makaburini.

Mustafa akajiunga na ule msafara wa kwenda mazishini, mimi aliniacha pale nyumbani pamoja na wanawake wenzangu.

Hapo msibani nilikutana na ndugu zangu wa Tanga pamoja na shangazi zangu wengine. Nilitambulishwa pia kwa ndugu zangu niliokuwa siwajui.

Msafara wa mazishi ulirudi saa kumi na moja na nusu jioni. Kulikuwa na ndugu wengine wa kiume waliokuwa wamekwenda kuzika, nikakutana nao. Niliwatambulisha kwa mume wangu Mustafa. Kuna baadhi ya ndugu zangu ambao walihudhuria harusi yangu nilipoolewa na Musa wakadhani yule alikuwa ni Musa.

Kwa vile kulikuwa na watu wengi kwenye msiba huo, mimi nilibaki kwa wanawake wenzangu tukishughulika na kazi ya kupika. Mustafa alikwenda kukaa na wanaume wenzake lakini kila mara nilikuwa natoka nje na kuzungumza naye.

Ilipofika usiku alikula chakula pamoja na wenzake waliokuwepo kwenye msiba. Baada ya chakula aliniambia atakwenda kukodi chumba cha gesti ili aweze kuoga na kubadili nguo kwani pale nyumbani asingeweza kuoga kutokana na hekaheka iliyokuwepo.

Akanipakia kwenye gari, nikampeleka katika gesti iliyokuwa mtaa wa pili. Akachukua chumba.

“Ina maana utalala hapa?” nikamuuliza.

“Itabidi nilale hapa, sasa pale nitalala wapi?”

“Si ulale barazani na wenzako?”

“Hapana, sikuzoea, nitalala hapa.”

“Ndugu zangu wakijua umelala gesti nitalaumiwa.”

“Si wameona tumeondoka pamoja.”

“Unajua nitafanyaje, nikishaoga nitakurudisha halafu nitaondoka kwa wakati wangu bila kukuaga. Gari nitaliacha palepale. Wakiona gari watajua nipo.”

“Halafu asubuhi utakuja saa ngapi?”

“Nitakuja mapema tu.”

“Sawa, basi fanya hivyo.”

Mustafa baada ya kuoga na kubadili nguo tulirudi tena msibani. Nikamuacha nje na wenzake. Ilipofika saa nne usiku nilitoka nje kumuangalia. Nilikuta gari lipo lakini mwenyewe sikumuona. Nikampigia simu.

“Umeshaondoka?” nikamuuliza.

“Nimeondoka dakika chache tu zilizopita.”

“Ndio, nafika sasa hapa gesti.”

Ilipofika saa tano usiku Sele akanipigia simu.

“Vipi mmeshazika?” akaniuliza.

“Tumezika tangu saa kumi, mbona hukunipigia mapema kuniuliza?”

“Nilijua hatutasikizana, ingekuwa ni vilio tu. Nikaona nikuache.”

“Ah! Mambo yamekwisha. Tumeshashukuru.”

“Haya, nitakupigia kesho asubuhi.”

“Tumepangisha vyumba huku, niko na wenzangu.”

“Angalia sana huko Sele, nasikia ukimwi ni mwingi sana!”

“Kumbe una mashaka na mimi mke wangu.”

“La, sina shaka yoyote. Nakuhadharisha tu.”

“Tuwasiliane hapo kesho.”

Baada ya kuzungumza na Sele nikatafuta mahali pa kulala. Nyumba ilikuwa imejaa ndugu na jamaa. Hakukuwa na nafasi vyumbani wala ukumbini. Watu walikuwa wametandika chini.

Nilipata nafasi katika nyumba ya jirani yetu ambako nililala barazani na wanawake wenzangu.

Niliamka saa kumi na mbili asubuhi nikarudi ndani na kuanza kushughulika na kazi.

Mustafa alikuja saa mbili asubuhi akanipigia simu kunifahamisha kuwa yuko barazani. Alikunywa chai na wenzake, baadaye nilimfuata na kuzungumza naye.

“Utaondoka saa ngapi?” nikamuuliza katika mazungumzo yetu.

“Nitaondoka saa nane.”

“Mimi nitabaki huku hadi matanga yaishe.”

“Ni siku saba kuanzia leo.”

Baada ya hapo nikarudi ndani. Niliendelea na kazi hadi saa sita. Ilikuwa ni baada ya chakula cha mchana kutolewa nikashitukia Sele akinipigia simu. Nikaenda pembeni na kupokea simu yake.

“Niko Tanga,” akaniambia na kunishitua.

“Unasemaje?” nikamuuliza kwa kutaharuki.

“Nimekwambia niko Tanga, nimeondoka Arusha asubuhi.”

“Mbona hukuniambia kuwa unakuja?”

“Ni wazo ambalo nililipata asubuhi, nimeona ni jambo jema nije ingawa sikuwahi mazishi lakini angalau nifike tu kuliko kuacha msiba uishe.”

“Kama ungeniambia kuwa unakuja ningekwambia acha tu, kwa sababu kama ni kuzika tumeshazika na wewe una kazi zako huko.”

“Sasa nimeshakuja niko hapa stendi ya Tanga. Naomba unielekeze mtaa mnaoishi.”

Kwa kweli Sele alikuwa amenichanganya akili yangu. Sikutarajia kabisa kuwa angekuja. Na kama angeniambia wakati wa asubuhi kuwa anakuja Tanga ningemzuia asije.

SEHEMU YA 33
NIKAJIULIZA ningefanyaje wakati Mustafa alikuwa pale?

Badala ya kujilaumu kwa ulaghai wangu wa kudanganya wanaume, nilijikuta nikimlaumu Sele kimoyomoyo.

“Huyu mtu ni mpumbavu kweli, kama alitaka kuja si angeniambia asubuhi?”

Hapo stendi aliposema yupo, unapita mitaa miwili tu unatokea katika mtaa ilipo nyumba yetu.

“Sasa hili ni balaa!” Nikajiambia kwa dhati.

“Mishi mbona uko kimya?” Sele akaniuliza.

Nikazinduka kutoka kwenye mawazo yangu.

“Ndio, nafikiria jinsi ya kukuelekeza,” nikamwambia.

“Ni mbali sana na hapa stendi?”

“Si mbali, ni mtaa wa tatu tu kutoka stendi.”

“Kama upo Barabara ya Pangani, njoo hadi barabara ya tisa upande wa kaskazini.”

“Hii stendi iko barabara ya ngapi?”

“Stendi inachukua barabara mbili; barabara ya kumi na moja na ya kumi na mbili. Wewe rudi barabara ya tisa.”

“Sawa, ngoja niitafute barabara ya tisa.”

“Kuna vibao vimeandikwa namba za barabara viko pembeni mwa barabara.”

“Sasa njoo hadi barabara ya tisa ukate kushoto.”

“Subiri nigeuze gari.”

Baada ya sekunde chache sauti ya Sele ikasikika:

“Nimeshafika barabara ya tisa.”

“Kata kushoto kwako.”

“Kuna nyumba imefungwa turubai nje, ni nyumba ya tatu baada ya kona.”

Sele akakata simu. Nilikuwa uani nikatoka nje haraka, nikaliona gari la Sele likifunga breki nyuma ya gari la Mustafa.

Nilitamani Mustafa awe ameshaondoka.

Nikatupa macho kila upande kumtazama Mustafa, sikumuona. Nikashuka barazani na kulifuata gari la Sele.

Sele aliponiona alifungua mlango wa gari na kushuka.

“Habari za safari?” nikamuuliza huku macho yangu yakitazama huku na huko.

“Safari ilikuwa njema, habari za hapa?”

Nilihisi miguu yangu inatetemeka. Hivyo ndivyo ninavyokuwa nikikumbwa na changamoto kali—miguu hunitetemeka ingawa mara nyingi si rahisi mtu kutambua.

“Nzuri, nyumbani kwetu ndio hapa.”

“Nimepaona. Poleni sana.”

Nikamkaribisha Sele bila kupenda. Tuliingia hadi chumbani alikokaa shangazi yangu mkubwa, kikongwe ambaye mara nyingi hakutoka chumbani.

“Kaa kwenye kiti,” nikamwambia.

Sele akakaa na kumuamkia shangazi:

“Marahaba, hujambo baba?” shangazi akamjibu.

“Sijambo, habari za hapa?”

“Kwanza ngoja nikuweke sawa mume wangu. Huyo si bibi yako, ni shangazi—dada yake marehemu,” nikamwambia Sele.

“Shangazi, huyu ni mume wangu,” nikamwambia, kwa kuwa tangu nifike na Mustafa sikuwahi kumtambulisha kwake. Nilikuwa nimemtambulisha kwa ndugu wengine tu tuliowakuta nje.

“Hata ukinionesha macho, yenyewe hayaoni. Yana kiza kitupu. Tunasubiri wakati tu,” shangazi akasema kisha akaniuliza:

“Ndiyo mume wako wa huko Dar?”

“Karibu sana mkwe wangu.”

“Asante. Poleni sana kwa msiba uliotokea.”

“Tumeshapoa baba, hiyo ni njia ya kila mtu. Hakuna atakayebaki.”

“Ni kweli shangazi. Mbele yake nyuma yetu.”

“Umeshakula?” nikamuuliza Sele.

Akatingisha kichwa: “Sijakula bado.”

“Ngoja nikuletee chakula humu humu chumbani.”

Nikatoka kumuandalia chakula. Lakini akilini mwangu nilikuwa nawaza nini kitatokea nikikutana na Mustafa.

Baada ya kumletea chakula, nikakaa naye pale chumbani. Alikuwa anakula huku tukizungumza.

“Ni vizuri umekuja, lakini kama ungenitaarifu mapema kuwa unataka kuja ningekuzuia,” nikamwambia Sele.

“Mawazo ya kuja huku yalinijia ghafla tu asubuhi, na wenzangu walinishauri nije angalau kuwapa pole.”

“Nilizingatia maelezo yako kwamba isingekuwa vizuri kazi iendelee Marerani bila wewe. Nikaona bora uendelee tu, kwa sababu kama ni kuzika tumeshazika jana.”

“Ni kweli, lakini bado naona nimefanya vizuri kuja.”

“Nisingependa wenzako waharibu kazi. Unajua umepoteza gharama nyingi.”

“Kama utaweza kurudi leo, ingekuwa bora. Hapa hakuna cha kukuweka. Tumeshazika, sasa ni matanga ya ndugu wa karibu tu. Wengine wote wameshaondoka.”

“Naweza kuondoka saa kumi jioni, ili kesho niwe machimboni.”

Ghafla simu yangu ikaita. Nilipoangalia, ilikuwa namba ya Mustafa. Nilihisi kuondoka nipokee pembeni, lakini nikajiuliza Sele atafikiria nini? Pia nikiiacha bila kupokea, naye atafikiri nini?

Kwa vile simu ilikuwa ikiendelea kuita na Sele akiisikia, nikaona bora niipokee pale pale.

“Uko wapi?” Mustafa akauliza.

“Niko ndani, nina kazi kidogo. Kuna wakati nilitoka sikukuona.”

“Nilikuwa nimezunguka mtaa wa tatu kuangalia stendi yenu. Sasa nimesharudi.”

“Subiri nakuja,” nikamkatiza, nikihofia Sele asishuku kwa maneno mengi.

“Sele kaka ananiita hapo nje, ngoja nimsikilize. Wewe endelea kula,” nikamwambia Sele.

Nikainuka na kutoka nje. Nilimkuta Mustafa ameketi barazani. Alipoona nimefika, aliinuka tukasogea kando ya gari yake.

“Naona muda unakaribia,” akaniambia.

“Hata mimi nilitaka kukupigia simu nikwambie.”

“Labda unipeleke ndani nikawaage kabisa wenyeji, kisha nianze safari.”

“Si unaona mishemishe zilizopo? Sijui utaenda kumuaga nani. Wewe funga safari tu, mimi nitakuaga. Subiri nikuletee begi lako.”

Nikamuacha Mustafa na kuingia ndani. Begi lake lilikuwa chumbani kule alikokuwa Sele.

Nilipoingia, Sele alikuwa ameshakula.

“Umeshamaliza kula?” nikamuuliza.

“Ngoja nimpe kaka begi lake, nakuja sasa hivi,” nikamwambia, nikachukua begi la Mustafa na kutoka.

Nilipokuwa nikimkabidhi Mustafa begi na kuagana naye, Sele akatoka nje akatukuta tumesimama kando ya gari.

Nilishtuka kidogo, lakini sikuonesha hofu. Kwa haraka nikamwambia Mustafa:

“Nilikuwa nazungumza na kaka, naona amenifuata huku nje.”

“Ni kaka yako?” Mustafa akauliza.

“Ni mmoja wa kaka zangu, anaishi Arusha.”

Baada ya kumwambia hivyo, nikamtazama Sele.

“Bado una mazungumzo?”

“Namaliza sasa hivi. Njoo umsalimie shemeji yako,” nikamwambia.

Sele akaja kumsalimia Mustafa. Kila mmoja akamuita mwenzake shemeji.

“Poleni sana jamani,” Sele akamwambia Mustafa.

Niliona hapo Sele anaweza kuharibu mambo, maana Mustafa angejiuliza: tuliofiwa ni sisi, kwa nini Sele anampa pole yeye?

Nikatabasamu na nikavunga:

“Unajua, ndio amekuja muda huu kutoka Arusha. Yeye hakuwahi kushiriki mazishi.”

“Ahaa, kumbe anaishi Arusha?” Mustafa akauliza.

“Yupo kikazi Arusha. Kwa bahati mbaya alipata taarifa jana, hakuweza kufika. Ndio maana kafika leo.”

“Na nyinyi nawapa pole vile vile,” Mustafa akamwambia Sele, akijua sisi ndio wafiwa.

“Nashukuru, tumeshapoa,” nikajibu haraka, kisha nikamgeukia Sele.

“Una mazungumzo na mimi?”

“Hapana, endeleeni tu. Mimi napumzika hapa nje.”

“Usijali, namalizana naye sasa hivi.”

Sele akatupisha, akaenda kuketi barazani.

“Basi wewe nenda, wala huna haja ya kuaga mtu. Waswahili hawa wanaweza kukuweka. Wakija kuniuliza nitawaambia umeshaondoka,” nikamwambia Mustafa.

“Sawa. Kwa hiyo mtamaliza matanga baada ya siku saba?”

“Ndio, natumaini itakuwa hivyo.”

Mustafa akafungua mlango wa gari lake na kujipakia.

“Basi utanisalimu shemeji.”

“Nitamsalimu. Safari njema, uende ufike salama.”

Hadi Mustafa anawasha gari na kuondoka, nguo yangu ya ndani ilikuwa imetota kwa jasho.

Zile dakika chache za kuwakutanisha Sele na Mustafa zilikuwa kama dakika za moto. Nilishukuru sana Mustafa alipoondoka salama na hakukutokea tatizo lolote.

SEHEMU YA 34
NILISIMAMA kwa sekunde kadhaa huku nikilitazama gari la Mustafa likikata kona kuelekea Barabara ya Pangani.

Ndipo nilipourudisha uso wangu kwa Sele. Muda ule nilianza kufikiria kwamba haikuwa lazima Sele aondoke siku ile, angeweza kulala na kuondoka kesho yake kwani mume mwenzake niliyekuwa namuhofia alikuwa ameshaondoka.

Nikaenda pale alipokuwa ameketi nikaketi naye.

“Kaka yako anakwenda wapi?” Sele akaniuliza.

“Ana safari zake mwenyewe, sijui anakwenda wapi.”

“Kumbe una kaka wengi!”

“Sana. Hawa watu wote unawaona ni ndugu zangu, ama ni kaka zangu au baba zangu wadogo. Umenielewa?”

Sele akanikubalia kwa kichwa.

“Yule kaka aliyeondoka ni mwana wa shangazi, mama yake ni yule shangazi uliyesalimiana naye kule chumbani,” nikamdanganya.

“Kwa hiyo huku Tanga una ndugu wengi kuliko Dar.”

“Ni kwa sababu huku ndiko tunakotoka. Mimi ni Mdigo wa Tanga. Mama yangu ndiye Muarusha.”

“Na wewe umeshabihiana sana na marehemu mama yako.”

“Lakini Mishi, mji wenu ni mtulivu. Nimeupenda sana.” Sele akabadili mazungumzo.

“Kama utapenda lala Tanga uondoke kesho,” nikamwambia.

“Hapana, nimeshapanga kuondoka leo kama tulivyokubaliana. Sitaweza kulala hapa.”

Niliendelea kuzungumza na Sele hapo barazani hadi saa kumi, muda ambao Sele alikuwa amepanga kuondoka.

Nilikwenda naye chumbani kwa shangazi nikamwambia amuage yeye tu. Shangazi aliposikia mume wangu anaondoka alimuuliza:

“Kumbe unaondoka leo?”

“Naondoka leo kwa sababu ya kazi. Kuna kazi zinaningoja huko Arusha,” Sele akamjibu.

“Mimi nilidhani unakwenda Dar.”

“Tunaishi Dar lakini kwa sasa niko Arusha kutokana na kazi zangu.”

“Basi uende salama mwanangu.”

“Asante shangazi, na wewe ukae salama.”

Baada ya Sele kuagana na shangazi nilitoka naye nikamsindikiza hadi lilipokuwa gari lake, akajipakia na kuondoka.

Nilijua walikuwepo watu waliokuwa wakijiuliza maswali kuhusu Sele na Mustafa lakini walishindwa kuniuliza Sele ni nani na Mustafa ni nani, kwani wote kwa nyakati tofauti niliwatambulisha kama waume zangu jambo ambalo liliwapa utata baadhi ya ndugu zangu.

Nilikaa Tanga kwa siku saba. Wakati wote nilikuwa nikiwasiliana na Musa aliyekuwa hospitalini na pia nilikuwa nikiwasiliana na Mustafa na Sele.

Baada ya kumaliza matanga nilirudi Dar. Nilifikia nyumbani kwa Musa ambako nilipanga nilale kwa siku moja kabla ya kwenda kwa Mustafa.

Usiku wake nilimpigia simu Musa na kumjulisha kuwa nilikuwa nimesharudi.

“Hawajambo watu wote?” akaniuliza.

“Hawajambo, wanakusalimia. Na wewe unaendeleaje?”

“Naendelea vizuri. Huu mguu wa pili nimeshavalishwa bendeji ngumu.”

“Nitakuja kukujulia hali kesho.”

“Utakuja asubuhi au jioni?”

“Nitakuja jioni, asubuhi nitakuwa na kazi ya kufanya usafi hapa nyumbani pamoja na kufua nguo.”

“Ukija jioni utanikaangia kuku wa kienyeji uniletee.”

Baada ya kuzungumza na Musa, Sele naye alinipigia simu nikamwambia bado niko Tanga.

“Natarajia kuondoka kesho.”

“Meshamaliza matanga?”

“Tumemaliza leo. Shughuli zinaendeleaje huko?”

“Zinaendelea vizuri. Kwa kweli tumefanikiwa kidogo.”

“Ukipata pesa uweke benki.”

“Mimi nakusanya tu madini ninayopata, siuzi huku.”

“Utakwenda kuuza wapi?”

“Nitakwenda kuyauza Sauzi. Kule nitapata bei nzuri.”

“Jitahidi mume wangu, karibuni tutapata mtoto, atahitaji kupata elimu bora.”

“Nimekuelewa mke wangu.”

Baada ya kuzungumza na Sele nikaenda kuoga. Kwa vile Mustafa hakunipigia kuniuliza chochote na mimi sikumpigia. Nilikuwa nimeshapanga kama atapiga na kuniuliza nimwambie nitaondoka kesho kurudi Dar. Sikutaka ajue kuwa nimesharudi.

Asubuhi kulipokucha ndipo Mustafa aliponipigia.

“Bado uko Tanga hadi leo?” akaniuliza.

“Ndio, napanda basi, nakuja Dar,” nikamwambia.

“Na mimi naenda Bagamoyo, mama yangu anaumwa.”

“Kwa hiyo sitakukuta?”

“Hutanikuta lakini nitarudi jioni.”

“Sawa. Jioni nitakwenda hospitali kumtembelea kaka.”

“Loh! Yule bwana nimemsahau kabisa. Tangu siku ile tulipokwenda pamoja sijakwenda tena. Sijui atanielewaje!”

“Yeye anajua uko Tanga na mimi. Usiwe na wasiwasi.”

“Sawa. Mwambie tulikuwa Tanga, asije akanielewa vibaya.”

Saa saba mchana nikaibukia Mbezi nyumbani kwa Mustafa nikijifanya ndio ninatoka Tanga.

Nilikuwa nimepitia sokoni ambako nilinunua kuku aliyekuwa ameshachinjwa kabisa.

Mtumishi wetu akaniambia kuwa baba Rama amekwenda Bagamoyo pamoja na Rama.

Nikamwambia nimeshawasiliana naye kwenye simu. Nikampa yule kuku amtengeze na kumkaanga.

“Mkaange vizuri, nataka kumpelekea kaka yangu hospitali, aliniagiza nikienda nimpelkee kuku,” nikamwambia.

Wakati msichana huyo akimshughulikia yule kuku, nilitoa baadhi ya nguo zangu nilizokuwa nikivaa kwenye msiba na kuzifua. Nilipomaliza niliingia chumbani nikajilaza kidogo.

Ilipofika saa tisa mtumishi alinibishia mlango. Nilikuwa nimepitiwa na usingizi. Nikakumbuka nilikuwa na safari ya kwenda Muhimbili.

Niliamka nikafungua mlango na kumuuliza msichana huyo:

“Umeshamkaanga yule kuku?”

“Tayari. Si uliniambia unataka kwenda hospitali?”

“Ndio. Nilipitiwa na usingizi kidogo. Muweke kwenye chombo kisha ukiweke kwenye mfuko. Najitayarisha nitoke.”

Nikarudi chumbani na kujiandaa.

Nusu saa baadaye nilikuwa nimeshaoga na kuvaa. Nikatoka na mfuko wangu na kwenda kutafuta usafiri.

Nilipofika Muhimbili nilimkuta Musa akiwa na baadhi ya jamaa na marafiki zake. Yule mdogo wake aliyekuwa akimhudumia alinipokea ule mfuko na kuuweka kwenye kabati lililokuwa kando ya kitanda cha Musa.

Tulisalimiana tukaulizana hali, nikapewa pole nyingi kutokana na msiba uliotokea. Hata hivyo nililaumiwa kwa kutowapa taarifa ya msiba jamaa zake Musa.

Musa akanitetea kuwa nilichanganyikiwa baada ya kupata taarifa ile.

“Kwa vile aliniambia mimi na mimi niliwambia imetosha,” akawambia.

Japo Musa hakufahamu, ukweli ni kuwa niliacha kwa makusudi kuwapa taarifa ya kifo cha shangazi yangu jamaa zake hao kwa vile na wao wangetaka kwenda kuzika. Na kama wangekwenda wangeweza kugundua uhusiano wangu na Mustafa pamoja na Sele.

Musa akanijulisha kuwa hali yake inaendelea vizuri ingawa aliambiwa angeendelea kukaa hospitali kwa muda zaidi hadi mifupa yake itakapoanza kuunga.

“Kuendelea kukaa hospitali si tatizo, tatizo letu upone,” nikamwambia.

“Kazini kwangu ndio kutakuwa na matatizo, si unajua hizi kazi za watu binafsi.”

“Una maana ukikaa hospitali kwa muda mrefu utafukuzwa kazi?”

“Unaona ajabu, wanaweza kunifukuza. Na hata kama hawatanifukuza wanaweza kunilipa nusu mshahara.”

“Kwani si uliumia ukiwa kazini?”

“Ndio. Nilipata ajali nikiwa Zambia.”

“Wana haki ya kukutibu mpaka upone na pia wana haki ya kukulipa mshahara wako kamili uweze kujikimu.”

“Unafikiri hizo sheria zinafuatwa?”

“Lakini hizo sheria zipo.”

“Najua kuwa zipo lakini hazifuatwi.”

“Wakija kufukuza kazi au kukupa nusu mshahara kwa sababu tu umekaa hospitali kwa muda mrefu nitakwenda kufungua mashitaka mahakamani kwa niaba yako, na hapo ndio tutaona sheria zinafuatwa au hazifuatwi.”

“Sijawahi kuona watu wale wakishitakiwa.”

“Ni kwa sababu nyinyi wenyewe hamna muamko na hamjiamini.”

Jamaa zake Musa waliniunga mkono katika mazungumzo yangu wakasema nilichosema kilikuwa sawa.

Mazungumzo yetu yaliendelea hadi muda wa kutazama wagonjwa ulipoisha. Jamaa zake Musa waliondoka na kutuacha mimi na Musa. Musa akanipa pesa za matumizi. Akanipa pia pesa nyingine niende nikamuwekee nyumbani. Aliniambia zilikuwa pesa alizokuwa akipewa na madereva wenzake pamoja na marafiki waliokuwa wanakwenda kumjulia hali.

“Ukija kesho niletee bukta moja na fulana,” Musa akaniambia.

“Fulana yoyote tu, nataka nibadili hii niliyovaa.”

Nilipoondoka hapo hospitali nilirudi Mbezi. Kwa vile nilishamwambia Mage, mtumishi wangu wa Kimara, kuwa sitalala Kimara, sikuwa na haja ya kurudi tena Kimara.

Mustafa alirudi usiku pamoja na Rama. Akaniambia mama yake alikuwa amepata nafuu kidogo.

SEHEMU YA 35
“KWANI anasumbuliwa na nini?” Nilimuuliza.

“Kwa kweli ni uzee tu, maungo yameshachoka. Maradhi hayamuendei mbali.”

“Nitatafuta siku niende nikamsalimie.”

Baada ya hapo Mustafa aliniuliza habari za Tanga. Nikamwambia ni nzuri.

“Nitakwenda tena kwenye arubaini.”

“Sawa, ila mimi nitakuwa sipo.”

“Nafikiri nitakuwa China.”

“Unatarajia kuondoka lini?”

“Mama yangu atakapopata nafuu nitaondoka.”

“Inshallah Mungu atampa nafuu.”

Siku iliyofuata niliamka saa kumi na moja na nusu alfajiri. Nikamwambia Mustafa kuwa ninakwenda Muhimbili kumjulia hali kaka.

Baada ya kuoga na kuvaa ilikuwa saa kumi na mbili na nusu. Nikaenda Kimara kuchukua fulana aliyoniagiza Musa kisha nikaenda Muhimbili. Sikumchukulia chai kwa sababu mdogo wake ndiye aliyekuwa amechukua jukumu hilo tangu nilipoondoka kwenda Tanga.

Nilizungumza na Musa hadi muda wa kutazama wagonjwa ulipoisha, nikamuaga na kuondoka.

Niliendelea kwenda Muhimbili kumjulia hali Musa hadi arobaini ya shangazi yangu ilipowadia, nikaenda Tanga. Safari hii nilimchukua mwanangu Rama kwa vile Mustafa naye alikuwa na safari ya kwenda China.

Nilikaa Tanga siku tatu, nikarudi Dar. Siku ile narudi, Sele naye alikuja Dar. Ikabidi nibaki Ilala kwa Sele.

Sele alinionesha mfuko uliokuwa na madini wakati tumekaa sebuleni tukizungumza.

“Mbona kidogo sana?” Nikamuuliza.

“Haya si kidogo, unadhani yangejaa kapu nzima?”

“Si ndio utapata pesa nyingi.”

“Unajua haya ni kiasi gani?”

“Ni pesa nyingi pia. Nikienda Sauzi naweza kupata pesa yenye thamani ya shilingi milioni mia tatu kwa pesa za Kitanzania.”

“Madini haya tu, upate pesa zote hizo?”

“Kumbe ni biashara nzuri sana!”

“Ndiyo maana niliamua kujiingiza katika biashara hii kwa sababu inalipa. Unapoteza pesa kuajiri watu lakini mwisho wa siku unaweza kupata pesa nzuri.”

“Unatarajia kwenda lini huko Sauzi?”

“Ndiyo nimekuja kwa ajili ya safari hiyo. Labda kesho kutwa naweza kuondoka.”

“Hizo pesa ukizipata utazifanyia nini, mume wangu?”

“Na mimi utanipa kidogo?”

“Nitakupa, mke wangu.”

Sele aliponiambia hivyo nilifurahi kwa kujua angenipa pesa nzuri na mimi ningeweza kubuni biashara yangu badala ya kutegemea kupewa pesa na waume.

“Ukienda huko utakaa muda gani?”

“Kama wiki mbili hivi.”

Baada ya siku ile, siku ya tatu yake Sele akaondoka kwenda Afrika Kusini kuuza madini yake.

Katika siku hizo tatu nilizokuwa na Sele sikwenda Muhimbili, na wala sikumfahamisha Musa kuwa nilisharudi kutoka Tanga. Ila nilikuwa nikiwasiliana na Mage, mtumishi wetu tuliyeacha nyumbani.

Siku alipoondoka Sele nikaenda Mbezi. Nililala siku mbili, siku ya tatu yake nikaondoka kwenda Kimara nikajifanya ndiyo natoka Tanga. Nilipofika nilishangaa kukuta mfanyakazi wetu amemleta mdogo wake.

Nikajua ile tabia ya kumuachia nyumba imemfanya ajione kama yeye ndiye mwenye nyumba kiasi cha kuamua kumleta mdogo wake bila hata kutujulisha.

Lakini nilipomuuliza huyo msichana ni nani, akanijibu:

“Nimemleta kutoka kijijini kwetu, ni mdogo wangu.”

“Kwa hiyo amekuja kukusalimia au amekuja kwa ajili gani?”

“Amekuja nikae naye hapa nyumbani, mimi naogopa kukaa peke yangu.”

“Siku zote si unakaa peke yako, mbona hujaniambia kama unaogopa?”

“Sijakwambia tu, lakini naogopa kulala peke yangu.”

“Si kuna mlinzi nje.”

Mage akanyamaza kimya, lakini baadaye akapata jibu.

“Nataka mwenzangu wa kunichangamsha kwa maana niko peke yangu humu ndani.”

Maneno yake, ingawa yalikuwa ya kutunga, yalikuwa na ukweli wake.

Sikumgombeza wala kumlaumu, isipokuwa nilimwambia:

“Mimi nilidhani amekuja kutafuta kazi.”

“Akipata kazi atakwenda kufanya.”

“Mbona sikuelewi, Mage!”

“Kama akipata kazi atakwenda kufanya, wewe si utakuwa umesharudi.”

Maneno hayo yakaishia hapo hapo. Yule msichana aliyeletwa nilimuacha aendelee kukaa pale nyumbani. Mimi mwenyewe nilihisi wakiwa wawili ni bora kwa vile yule msichana wa pili sitamlipa.

Jioni ya siku ile nikaenda Muhimbili na mwanangu Rama kumjulia hali Musa.

Musa akafurahi kumuona Rama kwa mara nyingine. Akazungumza naye kisha akaniuliza:

“Nimerudi leo mchana.”

“Hawajambo, wanakusalimia.”

“Nashukuru kupata salamu zao. Mimi kwa sasa naendelea vizuri.”

“Umeambiwa utatoka lini?”

“Wameniambia wataniruhusu nirudi nyumbani lakini sijajua ni lini.”

“Bora urudi nyumbani, hizi safari za kuja huku kila siku zinachosha.”

Maneno yangu yalikuwa kinyume na mtazamo wangu. Mimi nilikuwa ninataka aendelee kukaa kule hospitali hadi apone kabisa, kwani akirudi nyumbani atakuwa amenibana.

Lakini sikuweza kumueleza ukweli huo, nikajifanya nafurahia akirudi nyumbani.

Kulikuwa na kitu ambacho sikukijua au nilikipuuzia, lakini kilikuwa kama moshi unaoficha moto.

Kitendo kile cha kuwa na waume watatu kilikuwa kinambabaisha mwanangu Rama kiasi cha kutomjua baba yake halisi ni nani. Kwa sababu ya akili za kitoto alikosa uwezo wa kuuliza, lakini kadiri alivyokuwa anakuwa, udadisi uliendelea kumjaa.

Laiti kama ningejua mawazo yake, ningemwambia kwa siri kuwa baba yako ni fulani ili kumuondolea wasiwasi, ingawa kwa upande mwingine sikutaka ajue siri yangu.

Nilikuwa na hakika kwamba Rama atakapokuwa mkubwa mwenye akili zake nitakuwa nimeshaachana na Musa na Mustafa, na ningemuonesha baba yake halisi.

Tarajio langu lilikuwa kuwa mume ambaye ningedumu naye angekuwa Sele, kwa vile Sele alikuwa mchumba wangu wa kwanza na ndiye mwanaume aliyenianza. Si unajua mwanaume wako wa kwanza si rahisi kumsahau, na hata mkiachana, ukimuona tu moyo unashituka na kumbukumbu za maumivu zinakujia.

Waswahili wana msemo wao: Hakuna marefu yasiyo na ncha, na kila lenye mwanzo halitakosa kuwa na mwisho wake.

Baada ya wiki mbili Sele alirudi kutoka Afrika Kusini. Akanipa karibu shilingi milioni tano ili nianzishe biashara.

Musa naye akaruhusiwa kutoka hospitali, akawa anajiuguza nyumbani. Ikanibidi nihamie Kimara. Wakati huo Sele alikuwa ameshakwenda Marerani.

Hatukukaa sana, Mustafa akarudi kutoka China. Kutokana na ujanja wangu niliweza kumdanganya Musa na kwenda kulala Mbezi kwa Mustafa.

Ikapita miaka mingine miwili. Wanaume hao hawakuweza kujuana kabisa. Rama sasa alikuwa mkubwa na nilikuwa natarajia kumpeleka shule ya chekechea, lakini sikuwa nimeamua nimpeleke shule ipi. Sele alikuwa akiendelea na shughuli zake za Marerani, na Musa alikuwa ameshaanza kazi yake ya udereva baada ya miguu yake kupona. Mustafa naye alikuwa akiendelea na safari zake za China na India.

Kwa vile watu hao hawakuwa jijini kwa wakati mmoja, mara kwa mara wanakuwa safarini, ilinipa nafasi ya kuendelea kuishi kwa kila mmoja bila mwingine kujua kinachoendelea.

Siku moja ambayo sitaisahau maishani mwangu, waume zangu wawili Musa na Mustafa walikuwa jijini. Sele alikuwa ameondoka jana yake kwenda Marerani.

Baada ya Sele kuondoka, nikahamia Kimara kwa Musa ambaye alinipigia simu kunijulisha kuwa alikuwa ameshaingia jijini kutoka Burundi.

Musa alipokuja nyumbani alinikuta nikiwa na mwanangu Rama. Baada ya kumpokea Musa begi lake, Musa aliketi sebuleni na kuanza kuzungumza na Rama.

“Rama, mbona huniamkii baba yako?” Musa alimuuliza Rama.

Rama akabetua mabega yake.

“Wewe si baba yangu.” Rama akamjibu.

“Baba yako ni nani?” Musa akamuuliza.

“Baba yangu yuko Mbezi, anaitwa Mustafa.”

“Kumbe una baba mwingine huko Mbezi?”

“Wewe ukiondoka, sisi tunakwenda Mbezi na mama. Baba yangu ana gari na nyumba yetu ni nzuri kuliko hii.”

Maneno yale yalimshangaza Musa. Mimi nilijifanya nacheka-cheka, lakini niligundua kuwa nilikuwa nimefanya kosa kubwa kumuamini huyo mtoto na kumuonesha vitendo vyangu vya kuangaika kwa wanaume wakati alikuwa ameshakuwa na akili.

“Huyo naye ajiropokea maneno tu kama mwehu,” nikasema ili kumfanya Musa asiyatie maanani yale maneno.

Lakini Musa tayari alikuwa ameshapata shaka.

“Unasema nikiondoka mnakwenda kwa baba yako mwingine, mnalala huko?” Akaendelea kumuuliza.

SEHEMU YA 36
RAMA akamkubalia kwa kichwa. Mimi nikajifanya naendelea kucheka, lakini uso wangu ulikuwa umeshafadhaika.

“Baba yangu ameniambia atanipeleka shule ya chekechea.” Rama akazidi kumchanganya.

“Huyu mtoto haropoki kama unavyosema wewe, naona anazungumza kitu ambacho ana hakika nacho. Kuna baba yake mwingine huko Mbezi.”

“We baba Rama! Na wewe washika maneno ya mtoto asiye na akili,” nikamwambia Musa nikijifanya nimeyapuuza yale maneno.

“Anazungumza maneno ya maana, lazima niyashike, labda ana baba yake mwingine.”

“We Rama njoo hapa,” nikamuita Rama kwa ukali.

Rama akaja pale nilipokuwa nimeketi.

“Unamwambiaje baba yako?”

“Kule Mbezi tunakokwenda kila siku unaniambia yule baba unayelala naye ni baba yangu. Kule Ilala pia tunaenda kulala unaniambia yule baba ni baba yangu. Sasa baba yangu ni nani?”

Rama akazidi kuchafua. Maneno yake yalinitia hasira, nikampiga kibao.

“We huna adabu kweli!”

“Usimpige mtoto, mimi naamini anachosema ni kweli. Mimi ninakuwa safarini kwa muda mrefu, inawezekana umepata bwana mwingine,” Musa akaniambia wazi.

“Yaani mume wangu, mtu mzima na akili yako unashika maneno ya kipumbavu ya mtoto…!”

“Huo utu uzima wangu ndio unaonifanya niyashike hayo maneno unayosema ni ya kipumbavu. Mtoto mdogo hawezi kubuni maneno ya namna hii, lazima yatakuwa na ukweli fulani.”

Rama alikuwa amejishika shavu baada ya kumpiga kibao. Hakuwa akilia kwa sababu alishajua kuwa alichofanya kilikuwa kimeshachafua hali ya hewa.

“Una maana kwamba mimi nina bwana mwingine kwa mujibu wa maelezo ya mwanao?”

“Inawezekana. Mtoto hawezi kuniambia kuwa mimi si baba yake wakati mimi najua ni mwanangu.”

“Baba Rama, usinichafue, wewe unamuona huyu Rama ana akili? Si anaweza kujiropokea tu?”

Musa akanyanyuka alipokuwa ameketi. Nikamuona anaelekea jikoni huku maneno yakimtoka midomoni.

“Ukweli utajulikana tu.”

Sikujua alikuwa anakwenda wapi. Nikanyanyuka kumfuata. Nikamuona akiingia jikoni ambako Mage alikuwa anapika.

Na mimi nikamfuata huko. Nilimkuta ameshika mkono Mage.

“Mage, hebu niambie ukweli, huyu mke wangu analala hapa nyumbani kila siku wakati nikiwa sipo?” Akamuuliza Mage kwa ukali.

“Niambie ukweli, usiponiambia nitakupiga!”

“Siku nyingine anakuwa halali,” Mage akasema.

“Wewe huna adabu kweli, unasema silali hapa nakwenda kulala kwa baba yako!” Nikamuuliza Mage kwa jazba.

“Hebu nyamaza nimalize maswali yangu,” Musa akaniambia huku akinizuia kwa mkono mmoja ili nisimsogelee Mage.

“Anakwenda kulala wapi?” Musa akaendelea kumuuliza Mage.

“Ni lini na lini amekuwa akilala nje?”

Musa akageuza uso wake na kunitazama. Hivi sasa uso wake ulikuwa umebadilika, si mzaha.

“Mtoto hawezi kusema uongo. Amenema kitu anachokiona na kukijua,” akaniambia.

“Huyo msichana ni mbeya, ana lake analolitala na atalipata. Nimeshamuona anataka kunikosea heshima…” Nikaondoka kule jikoni huku nikiendelea kufoka peke yangu nikimlaumu Mage kwa maneno aliyomwambia Musa.

Musa akanifuata na kuniambia,

“Isiwe shida, ukweli utafahamika tu. Kama mtoto wako ni muongo au Mage ni mbeya, tutajua.”

“Twende, Rama,” akamwambia Rama na kutoka naye.

Sikujua walikwenda wapi. Niliinuka na kwenda kuwachungulia kwenye dirisha, nikaona wanapanda teksi na kuondoka. Walikokuwa wanakwenda kilikuwa kitandawili.

Nikaondoka kwenye dirisha na kumfuata Mage jikoni.

“We Mage, huo umbeya wako utakupa faida gani?” Nikamuuliza nikiwa na hasira.

“Kama mimi nikiachwa, unadhani wewe utaendelea kukaa humu ndani?”

“Baba Rama, kaniambia nisipomwambia atanipiga,” Mage akajitetea.

“We mpumbavu sana, huna akili. Kuna siku nilikuaga hapa nikakwambia kuwa nakwenda kwa wanaume?”

“Sasa kwanini unamwambia nalala nje?”

Mage akanyamaza. Akili yangu ilikuwa ikinituma nimpige vibao, lakini niliogopa. Mwili wake ulikuwa mkakamavu na alionesha wazi kuwa alikuwa na nguvu. Kama angeamua kupigana na mimi, ni mimi ningeumizwa, si yeye.

Nikabaki kumtazama Mage kwa hasira.

“Kama ulikuwa unamtaka Musa leo, nitakuachia ulale naye,” nikamwambia kisha nikatoka mle jikoni nikaingia chumbani.

Nilikusanya baadhi ya nguo zangu na vitu vyangu vya maana na kuvitia kwenye begi. Niliona hali ya hewa ilikuwa imeshachafuka pale nyumbani. Nilitoka na begi langu, nikakodi teksi na kwenda Ilala kwa Sele.

Nilipofika niliweka begi langu, nikajilaza kitandani na kuanza kuitafakari ile hali iliyokuwa imetokea. Sikujua Musa alikuwa amekwenda wapi na yule mwanangu. Upande mmoja wa akili yangu nilihisi kwamba alikuwa amekwenda kwa jamaa zake kunishitakia, na yule mtoto alimchukua ili akayaseme yale maneno, ndugu zake wayasikie.

Nilipoteza kama saa mbili hivi kuwaza na kuwazua, kisha nikatoka tena kurudi Kimara. Nilishaamua kama Musa ataamua kunipa talaka, itakuwa sawa. Kama ataamua kunisamehe pia itakuwa sawa.

Nilipofika Kimara, sikukaa sana, Musa akarudi akiwa na yule mtoto.

“Nilikwambia kuwa ukweli utafahamika na umeshafahamika,” akaniambia kwa hasira.

“Kupimwa. Mimi na Rama tumepima kipimo cha DNA. Kama alivyosema Rama, imegundulika si mwanangu!”

Aliposema hivyo, Musa alinitolea macho. Nikajua kuwa atanipiga.

“Kama si mwanao, ni mwana wa nani?” Nikamuuliza.

“Ndio, utanitajia wewe, huyo Mustafa aliyemtaja Rama ni nani?”

“Mimi simjui, muulize huyo Rama aliyekwambia. Mimi najua ni mwanao.”

“Mimi sikujua kama wewe mwanamke ni mshenzi kiasi hiki. Kumbe mimi nikienda safari, wewe unakwenda kulala kwa wanaume. Leo mwanao mwenyewe anakuumbua.”

Nikanyamaza kimya nikiwa nimefura. Nilijua kama nitajibu Musa, angeweza kunipiga.

Simu yangu ikaita. Nilikuwa nimeiweka kwenye kochi nilipoketi. Nikaishika na kutazama namba iliyokuwa inapiga. Ilikuwa na jina la M, nikajua alikuwa Mustafa.

Sikupokea ile simu, nikairudisha kwenye kochi. Nilijilaumu kwanini sikuwa nimeizima.

Simu ilendelea kuita. Nikawa namtazama Musa.

“Pokea simu, usinitazame mimi,” Musa akaniambia kwa kunisuta. Vile nilivyoacha kuipokea, alishashuku kwamba ilikuwa simu ya mwanaume wangu.

Aliponiambia vile, nikaikata. Kitendo hicho kikazidi kumpa mashaka Musa.

Hakuniambia kitu, ila alipiga hatua za haraka, akapeleka mkono wake akitaka kuichukua ile simu. Akawahi kuishika na mimi nikaishika. Tukawa tunaigombania.

“Achia!” Musa akaniambia kwa hasira.

“Na wewe achia, kwani hii ni simu yako?”

Musa alitumia nguvu, akanisukuma nikaiachia simu, akabaki nayo yeye.

“Unataka simu yangu ya nini?” Nikamuuliza Musa kwa hamaki.

“Nataka kuichunguza.”

“Mbona umehamaki sana, kuna nini kwenye hii simu?”

Sikuwa nikijali kwamba Musa angegundua kuwa Mustafa ni mwanaume wangu. Nilichojali na ambacho sikutaka Musa ajue ni kama nilikuwa na ndoa mimi na Mustafa.

Nilijua kwamba kugundulika kwa jambo hilo kungeniletea matatizo makubwa kwa upande wa Musa na kwa upande wa Mustafa.

“Tafadhali nipe simu yangu,” nikamwambia Musa kwa ukali.

“Sikupi!” Musa akanijibu kibabe.

“Musa, nipe simu yangu!” Nilitumia jina la Musa badala ya la baba Rama kama nilivyozoea kumuita. Si kwa sababu alikuwa amegundua kuwa Rama si mwanawe, bali pia ile heshima yetu ya mke na mume ilikuwa imeshatoweka.

Kama nilikuwa namdanganya kwamba yeye ni baba Rama, sikutaka kumdanganya tena kwa sababu ukweli alishaujua kuwa Rama si mwanawe.

“Nakwambia kwamba simu sitakupa mpaka niichunguze,” Musa akaniambia.

“Lakini ni tabia gani hiyo ya kuchunguza simu za wenzako? Simu si yako ni yangu, unataka uchunguze nini?”

“Sikiliza Musa, kama umenichoka, tafadhali nipe talaka yangu niondoke hapa kwako. Sitaki ugomvi na wewe, wala sitaki tukoseane heshima.”

“Wewe una heshima gani, kama ungekuwa na heshima ungenizalia mtoto wa nje?”

“Wewe huko unakoenda huna wanawake? Mbona mimi sikuulizi. Kuna siku nilikuta kondomu kwenye mfuko wako, mbona sikutaka kugombana na wewe?”

SEHEMU YA 37
KABLA Musa hajanijibu, Mustafa akapiga tena simu. Na simu ilikuwa mikononi mwa Musa.

Nikawaza kwamba nimrukie Musa nipigane naye ili ile simu ianguke chini na kuvunjika. Lakini kama aliyeyagundua, mawazo yangu alirudi kinyume nyume huku akitazama namba iliyokuwa inaita kisha akaipokea.

“Nakwambia Musa, nipe simu yangu mpumbavu wewe!” Nikampandishia huku nikimfuata. Nilikuwa nataka tupigane.

Nilijua kuwa angenipiga kwa sababu yeye ni mwanaume na ana nguvu kuliko mimi, lakini asingeweza kuisikiliza tena ile simu, na nilikuwa nataka ianguke chini ivunjike.

Nilipomsogelea, Musa alinipiga kibao kilichonirudisha nyuma na kunitupa kwenye kochi.

“Wewe nani?” Musa akauliza kwenye simu.

“Kwani wewe unayeniuliza ni nani?” Mustafa akamuuliza. Bila shaka alikuwa ameshangaa kusikia sauti ya kiume.

“Mimi ni mume wa Mishi, na wewe ni nani?”

“Nakwambia mimi ni mume wa Mishi.”

Niliposikia zile sauti zikikoromeana, nikajiambia, “Nimekwisha!”

Nilitamani ardhi ipasuke niingie ndani.

“Mume wa Mishi. Mishi ana mume mwingine zaidi yangu mimi?” Mustafa akauliza.

“Unataka uniambie wewe ni mume wa Mishi, uko wapi?”

“Wewe ndiye Mustafa, baba yake Rama?”

“Huyu Mishi ni mke wako wa ndoa?”

“Ndiyo, nina ndoa naye. Mishi ni mke wangu, nashangaa ninampigia simu unapokea wewe.”

“Kumbe wewe ndiye unayenichukulia mke wangu, umempa mimba na kuzaa mtoto, halafu unaniambia ni mke wako wa ndoa?”

“Yaani unataka kuniambia Mishi ni mke wako wewe?”

“Ndiyo, Mishi ni mke wangu.”

“Tuna karibu miaka saba sasa?”

“Wewe uko wapi hapo?”

“Na Mishi yuko hapo?”

“Nataka kuja kumuona. Tafadhali nielekeze, mko mtaa gani? Ninakuja sasa hivi.”

Musa akamuelekeza mtaa tunaoishi pale Kimara pamoja na kumtajia nambari ya nyumba.

“Nataka uje sasa hivi nionane na wewe.”

Nilipoona siri imefichuka na ingefichuka zaidi watu hao watakapokutana, niliona nikimbie ili niwaache waje wagombane wenyewe.

Nikainuka kwa jazba pale kwenye kochi nilipokuwa nimekaa baada ya kupigwa kibao.

“Unakwenda wapi?” Musa akaniuliza kwa ukali. Alikuwa amepandisha za kikwao. Kifua chake kilikuwa kimevimba na mishipa ya mikono ilikuwa imetokeza.

“Nakwenda zangu kwetu,” nikamjibu, huku nikielekea chumbani.

Musa akaja kusimama mbele yangu.

“Nakwambia huendi popote, utakaa hapa mpaka kieleweke!”

“Utakijua wakati huyo hawara yako atakapofika.”

“Yaani una tamaa kwamba kuna mtu atakuja hapa?”

“Ameniambia anakuja na ninaamini kuwa atakuja.”

“Haya, nisubiri aje, mimi nakwenda zangu.”

“Nisiende vipi? Sasa nisubiri nini hapa?” Nikamuuliza Musa kwa mkazo kama vile niliona swali nililomuuliza lilikuwa la maana sana.

“Huyu mwanamme anasema anakuja na amenihakikishia kuwa wewe ni mke wake, nataka aje tujue wewe ni mke wake kama alivyosema au ni mke wangu?”

“Hivi akitokea mwandawazimu akikwambia mimi ni mke wake basi wewe unakuja juu tu. Sasa akija na kukwambia mimi ni mke wake, utamfanya nini?” Niliendelea na maswali yangu ya kipuuzi.

“Nitamwambia akuchukue mwende zenu.”

“Sasa ukali wa nini?”

“Najua wewe ni hodari sana wa kusema, lakini ninachotaka mimi kaa hapa mpaka huyo mtu aje.”

“Halafu unipe talaka yangu.”

“Haya, mimi nakaa hapa, naomba unipe hiyo simu yangu.”

Nikaenda kukaa kwenye kochi.

“Mbona unapenda tubishane. Simu yako sitaila. Akija huyo mtu, nitakupa simu yako.”

“Sasa ndugu zangu wakinipigia, unataka upokee wewe?”

Musa hakunijibu tena. Akawa anarandaranda pale sebuleni, simu yangu akiwa nayo mkononi. Mage alikuwa amenyamaza kimya jikoni, akisikiliza nikichambana na mume wangu. Hakuthubutu hata kuchungulia kwa kuniona aibu.

Mwanangu Rama, ambaye muda wote alikuwa amesimama akitutazama, alisogea pale nilipokuwa nimeketi akawa ananiangalia.

Bila shaka alikuwa akinionea huruma. Aliona maneno aliyomwambia baba yake ndio yaliyosababisha ugomvi huo. Pengine alikuwa akijilaumu kimoyo moyo.

Hapo sebuleni pakawa kimya kwa karibu saa moja kasorobo. Sikuwa na wasiwasi sana. Nilijua hata kama Mustafa angefika na ingebainika kuwa wote wawili walinioa, hatua ambayo wangechukua ni kuniacha tu.

Kama Musa na Mustafa wataniandikia talaka, nitabaki na mume mmoja ambaye pia alikuwa na uwezo. Kwa hiyo sikujali sana.

Kitu ambacho sikukitaka ni ile aibu na fedheha, lakini kama ndio yameshanifika, niliendelea kujiambia nitavaa uso wa kauzu.

Mara nikasikia gari ikisimama barazani, nikashituka kidogo. Muda huo huo, simu yangu aliyokuwa nayo Musa ikaita.

Musa akatazama namba iliyokuwa inaita kwenye skirini ya simu kisha akaipokea.

“Nazungumza na yule mume mwenzangu au nazungumza na Mishi?” Sauti ya Mustafa ikasikika ikiuliza.

“Unazungumza na mimi.” Musa akamjibu.

“Wewe ndiye uliyepokea simu yangu mara ya kwanza?”

“Nyumba uliyonielekeza nimeshafika lakini sina hakika kama ndiyo hiyo, naomba utoke nje.”

“Ndiye wewe uliyefika na gari?”

Kukawa kimya. Baada ya sekunde chache mlango ukafunguliwa. Mustafa akaingia. Aliingia kibabe kama anayeingia nyumbani kwake. Uso wake ulionesha wazi kuwa aliingia kivita.

Wakati anaingia, macho yake yalishazunguka hapo sebuleni na kutukagua sote tuliokuwepo. Alimuona Musa, aliniona mimi, lakini uso wake huo haukuonesha mshangao kama nilivyotarajia kumuona.

Hakumsemesha kitu Musa, alinifuata mimi kwa hatua kakamavu akaniuliza.

“Umefuata nini hapa?”

“Unamuulizaje yeye, zungumza na mimi niliyekuita?” Musa akamwambia.

Mustafa akamgeukia Musa na kumtazama kwa macho makali.

“Nizungumze na wewe kama nani?”

Nikajua hawa watu wanaweza kupigana.

Nikanyanyuka na kumshika mwanangu.

“Kama mume wa Mishi,” Musa akajibu Mustafa kwa sauti kakamavu.

“Huyu ni mke wako… huyu ni mke wako?”

“Ni mke wangu ndiyo. Kwanini wewe unadai kuwa ni mke wako?”

“Huyu ni mke wangu!” Mustafa akasema kwa kufoka.

Nilimshika mkono mwanangu nikaenda uani. Hakukuwa na aliyenipatiliza. Wote walikuwa wamepandwa na mori.

Nilipofika uani, nikasimama kando ya mlango na kuwachungulia.

Kumbe Mustafa alikuja na hati ya ndoa yetu. Akatia mkono kwenye mfuko wa shati lake na kuitoa.

“Labda uniambie ni hawara yako nitakuelewa, hati ya ndoa yetu hii hapa. Na wewe nioneshe hati yenu.” Mustafa alimwambia huku akimuonesha ile hati.

Nilimuona Musa akiikodolea macho hati hiyo, akaisoma.

“Ngoja na mimi nikuletee hati yangu,” Musa akamwambia na kuelekea chumbani.

Baada ya muda kidogo alitoka akiwa ameshika hati yake.

“Hati yetu hii hapa.”

Alimpa Mustafa ile hati. Mustafa akaichukua na kuisoma. Katika hati zote mbili jina langu lilionekana pamoja na saini yangu.

“Huyu mwanamke ndio atatueleza ukweli.” Mustafa akasema huku akiinua kichwa chake kunitafuta mimi kwa macho. Alipoona sikuwepo, akauliza:

“Amekimbia. We Mishi, njoo hapa!”

Niliposikia hivyo, nilikimbia na mwanangu kuelekea mlango wa nyuma uliokuwa uani.

Niliufungua na kutoka na Rama. Nikaanza kuchapuka kuelekea katika nyumba zingine. Sikuwa na viatu na mwanangu pia alikuwa peku peku. Tulitembea hivyo hivyo hadi mtaa wa pili. Nikaona teksi inapita, nikaisimamisha.

Teksi iliposimama, tukajipakia.

“Tupeleke Ilala, mtaa wa Pangani,” nikamwambia dereva wa teksi.

Teksi ikaondoka kuelekea Ilala. Moyo ulikuwa ukinienda mbio na nilikuwa nimetaharuki. Tukio hili la kufumaniwa na waume wawili nilikuwa nikilitarajia, lakini sikujua kama lingenitokea kipumbavu kama lilivyotokea.

Kwa jinsi fumanizi hili lilivyotokea, kusingekuwa na njia yoyote ya kujitetea zaidi ya kukimbia.

Wale watu wana hasira, wangeweza kuchangia kunipiga na kuniua kabisa, nilijiambia.

TEKSI ilitufikisha Ilala nyumbani kwa Sele. Sikuwa hata na pesa ya kulipia teksi. Nikashuka na mwanangu na kuingia ndani kwenda kuchukua pesa za kulipia teksi.

Mtumishi wangu alinishangaa alivyoona nikiingia na mwanangu bila viatu, lakini alivyoona nilivyokasirika hakuniuliza chochote.

Niliingia chumbani nikafungua kabati na kuchukua pesa ambayo nilitoka nayo nje na kumlipa mwenye teksi.

Nilirudi ndani nikaenda kuoga na kubadili nguo. Nilijiambia nilikuwa nimefanya jambo la maana kuwahi kuhamisha nguo zangu na baadhi ya vitu vyangu.

Sikutarajia tena kurudi kwa Musa wala kwa Mustafa. Nilijihesabu kama tayari nimeshapewa talaka na waume wote wawili.

Nilikuwa na hakika kwamba Musa na Mustafa walinijadili sana na kuniona nilikuwa mwanamke tapeli nisiyefaa, na hapakuwa na shaka yoyote kwamba wote waliamua kuachana na mimi.

Kama waliamua hivyo, ingekuwa nafuu kwangu kwa sababu tayari nilikuwa na mume mwingine niliyekuwa nikimtegemea, ambaye kwa bahati njema alikuwa Marerani.

Kama kulikuwa na kitu kilichonisikitisha, ni ile simu yangu iliyobaki mikononi mwa Musa, ambayo kutokana na sekeseke hili lililotokea, nisingeipata tena. Nilijua Musa asingeweza kunipa tena baada ya kugundua unyama niliowafanyia.

Usiku ule nililala bila kula. Mwanangu ndiye aliyekula kidogo na mtumishi wetu.

Asubuhi, kulipokucha, nikaenda kununua simu nyingine kama ile. Tatizo lilikuwa kuipata ile laini yangu. Nikajiambia isiwe tabu. Niliwaona mawakala wa simu wakanipatia laini nyingine yenye namba ile ile baada ya kuwambia simu yangu imepotea.

Kwa hatua hiyo, nilijua laini aliyobaki nayo Musa isingefanya kazi tena na hivyo asingeweza kunasa taarifa zangu.

Baada ya kupata laini nyingine, nilimpigia Sele. Sele alipopokea simu yangu, aliniuliza:

“Vipi Mishi, mbona napata taarifa za ajabu-ajabu?”

“Taarifa gani?” Nikamuuliza.

“Jana usiku nilikupigia simu, akapokea jamaa mmoja, akaniuliza wewe nani, nikamwambia mimi ni mume wa Mishi…”

Sele alipoanza kuniambia hivyo, moyo wangu ukaanza kwenda mbio; nikajua habari zimeshamfikia Sele.

“Huyo mtu alikuwa nani?” Nikamuuliza.

“Ameniambia eti yeye ni mume wako, na pia ulikuwa umeolewa na mume mwingine, yaani mimi nilikuwa mume wa tatu. Hizi habari zilinishangaza sana.”

“Nikamwambia Mishi ni mke wangu mimi, tulioana hivi karibuni, na kwamba nilikuwa ninajua alikuwa ameolewa na mume mwingine aliyezaa naye mtoto, lakini walishaachana. Akaniambia hujaachwa.”

“Sasa, kama sijaachwa, mbona ninaishi na wewe siku zote?”

“Ameniambia umekuwa ukitumia ujanja wa kuishi na waume wote watatu kwa wakati mmoja; huyu akisafiri unakwenda kwa huyu, na huyu akisafiri unakwenda kwa huyu.”

“Huo ni uongo. Mimi sina mume mwingine zaidi yako; mume niliyekuwa naye alikwishaniacha.”

“Kama alikuacha, huyo mume mwingine ametokeaje?”

“Na yule jamaa unayedai mliachana, aliipataje simu yako? Mimi nilikupigia wewe nikaona anapokea yeye?”

“Sikiliza Sele, jana nilipoteza simu yangu. Sijui niliibiwa au niliitupa sehemu. Sasa, bila shaka huyo aliyeiokota ananifahamu na ndiye huyo aliyezusha uongo huo.”

“Sasa amekurudishia hiyo simu?”

“Hapana. Nimenunua simu nyingine na nimeisajili tena laini yangu.”

“Hivi sasa uko wapi?”

“Niko nyumbani Ilala.”

“Jana niliambiwa ulikuwa Kimara na ulikimbia na mtoto baada ya hao wanaume wawili kukutana.”

“Huo ni uongo mtupu. Mimi niko nyumbani tangu ulipoondoka. Usisikilize maneno yao; hizo ni fitina za kutaka kututenganisha.”

“Unakuja kwa ajili ya huo uongo? Wewe endelea na shughuli zako, bwana.”

Hapo sauti yangu ilikuwa imeshabadilika. Nilijua kama Sele atakuja, sitakuwa na ujanja tena.

“Kama nitakuja nitakjulisha,” Sele akaniambia na kukata simu. Jinsi alivyokata simu ilionesha wazi kwamba ile habari ilikuwa imeshamtia wasiwasi.

Mchana wa siku ile nilishinda bila furaha kutokana na sakata hilo. Tegemeo langu lilikuwa kwa Sele, na nilidhani Sele hatajua. Lakini naye ameshapata habari.

Nilikuwa nikijiambia kama Sele atakuja Dar na kuthibitisha kuwa habari aliyoambiwa ina ukweli, na yeye ataniacha, na hivyo nitabaki bila mume.

Sikuweza kujua mara moja hatima ya yule mwanangu itakuwaje.

Usiku baada ya kula chakula, Sele akanipigia simu akaniuliza:

“Niko nyumbani, ndio kwanza tumemaliza kula chakula.”

“Yule jamaa amenipigia tena, ameniambia kama nilikuoa kweli basi nimeoa mke wa mtu tena si mtu mmoja. Hivi ninavyokwambia, walikuwa wanakutafuta, hawajui uko wapi. Nimemwambia yule jamaa kuwa uko nyumbani kwangu Ilala. Bado, Mishi, unakataa kwamba wakati nakuoa hukuwa mke wa watu?”

“Siwezi kukubali, huo ni uzushi. Mume wangu ni wewe peke yako,” nikamwambia Sele ili kumpa moyo asiamini maneno aliyoelezwa.

Lakini Sele bado alionesha kutokuwa na furaha. Akaniambia:

“Sawa. Mimi nakuja huko.”

Aliposema hivyo, sauti yake ilikuwa ya kinyonge sana.

“Yaani, Sele huniamini tena?” Nikajidai namuuliza kwa kusikitika.

“Sio kwamba sikuamini, bali hii habari imenikosesha furaha.”

“Sasa unataka kufanya nini?”

“Nataka nije ili nionane na huyo mtu anayezizusha hizi habari nimuulize ana maana gani.”

“Haina haja. Tangu unanioa nilijua kulikuwa na watu hawakufurahishwa na uamuzi wetu.”

“Kitu ambacho kinanipa hofu ni kuwa yule mtu anayenieleza habari hizi yuko thabiti sana na anaonekana ana hasira, kitu ambacho kinaonesha maelezo yake yana ukweli fulani.”

“Sasa subiri nije huko; ukweli na uzushi tutaujua huko.”

Sele alipoaniambia hivyo, alikata simu. Nikabaki nimeduwaa. Kwa vyovyote vile, Sele atakuwa ameshabadilika na kuwa upande wa kina Musa, nikajiambia.

Yeye ndiye niliyemtegemea sana. Siku zote nilikuwa nikijiambia bora niachwe na Musa au Mustafa lakini nibaki na Sele. Nilikuwa nikitarajia kuwa iko siku Musa na Mustafa watakuja kung’amua kuwa wanakula shirika. Nilijua kuwa wataniacha na mimi nisingejali kwa sababu ya kumtegemea Sele.

Sasa, Sele niliyekuwa nikimtegemea tayari ameshabadilika. Kweli, siku ya kufa nyani miti yote huteleza!

Kitu ambacho sikupenda kitokee ni Sele kuja Dar kufuatia hizi habari za mimi kuolewa na waume watatu. Nilijua, kama atakuja, kila kitu kitaharibika. Hao waume wakikutana, wanaweza kuniua.

Kama kweli Sele atakuja, niliendelea kujiambia, ni bora nikimbie wasinikute. Lakini nilijiuliza, nitakimbilia wapi ambapo sitaweza kupatikana?

Sana sana, ningekimbilia Tanga kwa shangazi zangu, lakini wanaume wote watatu wanakufahamu. Wanaweza kunifuata huko.

Japokuwa nilikuwa na uhakika kwamba ningeweza kuwakwepa, bado wangeweza kuipeleka kesi kwetu. Aibu yangu itajulikana. Jambo hilo sikutaka litokee.

Usiku wa siku ile, sikulala kwa mawazo. Nilimlaani sana mwanangu kutokana na kitendo chake cha kumwambia Musa maneno yale yaliyosababisha mbivu na mbichi kujulikana.

Lakini kila nilipowaza kwamba mwanangu ndiye chanzo cha yote, moyo wangu ulinisuta kwamba chanzo cha yote ni mimi mwenyewe. Tamaa yangu ndiyo iliyokuwa chanzo cha yote.

Tamaa yangu ndiyo iliyonifanya nikubali kuolewa na Mustafa wakati nikijua kuwa tayari nina mume. Na tamaa yangu hiyo hiyo ndiyo iliyonifanya niolewe tena na Sele huku nikijua kuwa nilishaolewa na waume wawili. Nikajiambia, kama kuna wa kumlaumu, nijilaumu mimi mwenyewe.

Asubuhi, kulipokucha, sikuwa na habari kuwa Sele aliondoka tangu alfajiri kuja Dar bila kunijulisha kuwa yuko njiani.

Alipofika Dar, Sele aliwasiliana na Musa kabla ya kufika nyumbani. Alikwenda nyumbani kwa Musa. Musa akampigia simu Mustafa kumuita. Mustafa alipokwenda, maneno yakazungumzwa.

Nilikuwa niko chumbani, napanga nguo zangu kwenye sanduku, nikasikia watu wanaingia. Sikujua walikuwa kina nani, lakini ghafla nikaona mlango wa chumbani unafunguliwa. Nilipotupa macho, nikamuona Sele. Kusema kweli, nilishituka sana.

“Hebu njoo huku sebuleni,” Sele akaniambia bila hata salamu. Uso wake na sauti yake siku ile havikuwa vya kawaida. Nilipomuona tu, nilimuogopa.

Aliponiambia niende sebuleni, sikujua kama alikuwa amekuja na kina Musa. Nikaacha kupanga nguo, nikatoka.

SEHEMU YA 39
Vile nafika sebuleni, nikamuona Musa na Mustafa wamekaa. Moyo ulinipiga kwa kishindo. Nikajua saa ya kuumbuka ilikuwa imewadia. Ujanja wangu ulikuwa ni wa kukimbia; pale ningekimbia, kwa wapi?

Nilishindwa hata kuwasalimia, nikabaki nimesimama huku nimetahayari.

“Kaa,” Sele akaniambia.

Miguu ilikuwa ikinitetemeka. Nikaenda kwenye kochi na kukaa, lakini nilielekea upande mwingine.

“Haya Mishi, nieleze, unawajua hawa?” Sele akaniuliza huku akinionesha Musa na Mustafa.

“Siwajui,” nikamjibu bila kuwatazama hao watu aliouliza kama nawajua.

“Mimi hunijui?” Musa ndiye aliyeanza kuniuliza.

Niliposema, ‘Mume wangu ni Sele,’ Mustafa akaja juu.

“Wewe mwanamke, ulikuwa na waume wangapi?” akaniuliza kwa hasira.

“Nimeshamtaja mume wangu.”

“We mwanamke shetani kweli kweli…”

Mustafa akasimama kwa hasira akaelezea historia yetu mimi na yeye tangu tulivyokutana hadi tulivyooana na hatimaye kupata mtoto mmoja. Akaonesha na hati ya ndoa yetu.

Musa naye akaeleza kivyake na kuonesha hati ya ndoa yetu.

“Na huyo mtoto, mimi pia niliambiwa ni mwanangu. Jana ndio alinikataa akasema mimi si baba yake.”

Wote isipokuwa Sele walinionesha hati za ndoa tuliofunga kwa nyakati tofauti ambazo zilikuwa na saini yangu. Nilikuwa nimenyamaza kimya kwa aibu.

“Ina maana kwamba wakati ule nakuoa ulikuwa umeshaolewa na mwenzangu na ulikuwa ukitufanya wapumbavu, sio? Mimi nikisafiri unaenda kwa mume mwingine, na mume mwingine akisafiri unaenda kwa mwingine,” Mustafa akaniambia.

“Ujue za mwizi ni arubaini, arubaini zako zimetimia leo,” Musa akaongeza kupigilia msumari.

“Halafu we bwana, kama ninakukumbuka, tuliwahi kukutana mahali lakini sikumbuki ni wapi,” Mustafa akamwambia Musa.

“Umenikumbusha. Hata mimi nilikuwa najiuliza swali kama hilo tangu juzi. Hukuwahi kuja hospitali ya Muhimbili kunijulia hali nilipokuwa nimevunjika miguu kwa ajali ya gari?”

“Oh! Nimekumbuka sasa. Tulikutana hospitali ya Muhimbili. Mishi akaniambia wewe ni kaka yake!”

Hapo niliinamisha uso wangu chini kwa aibu.

“Unaona jinsi msichana huyu alivyokuwa akitufanya wapumbavu!” Musa akafoka.

Sele naye akaingiza msumari wa moto kwenye kidonda.

“Na mimi nina kumbukumbu kama hizo. We bwana, nilikuwa nakutazama sana tangu muda tulipokutana. Napata kumbukumbu kwamba tulikutana Tanga wakati wa msiba wa shangazi yake Mishi. Mishi akaniambia wewe ni kaka yake,” Sele alimwambia Mustafa.

“Ni kweli. Na mimi nimekukumbuka. Hivi huyu msichana alikuwa akizungusha akili zetu kiasi hiki!”

“Mimi nilikuwa na uchumba naye kabla yenu nyinyi, isipokuwa niliondoka nikaenda nje ya nchi nikakaa sana. Niliporudi, nikakutana naye, akaniambia aliolewa na kuachika. Kwa vile bado nilikuwa nampenda, tukakubaliana tuoane. Sasa jana, nampigia simu nikiwa Marerani, simu ikapokelewa na mtu mwingine, nikashangaa sana.”

“Niliipokea mimi, ndio nikakuuliza huyo Mishi ni nani wako, ukaniambia ni mke wako,” Musa akamwabia Sele na kuongeza:

“Hii simu kuwa nayo mimi imesaidia kufichua siri nyingi za huyu msichana.”

“Kwa kweli nilimuamini sana na sikutarajia kwamba alikuwa ni chui aliyevaa ngozi ya kondoo. Alikuwa akituzunguka wanaume watatu wenye akili zetu!” Mustafa akasema.

Wakati wote huo nilikuwa nimeinamisha kichwa changu kwa aibu. Sikuwa na jambo lolote la kupinga. Kwa kweli nilitahayari vibaya sana.

Watu hao waliendelea kunijadili kwa hasira na kuniuliza maswali ambayo sikuweza kuyajibu. Nilishukuru sana kwamba hakukuwa na yeyote aliyenipiga hata kibao.

Hatimaye, kile ambacho nilikuwa nakitarajia kilitokea. Alianza Mustafa kunihukumu:

“Mimi nimeshakuacha, si mke wangu tena. Na tangu hapo hukuwa mke wangu. Ulikuwa ukinitapeli tu.”

Nikamkubalia kimoyo moyo. “Hewala.”

“Mimi ndiye niliyenza kukuoa kabla ya wanaume wako wote, na mimi nasema kuwa nimekuacha talaka tatu. Bora kuishi bila mke kuliko mwanamke wewe.”

Nilimtarajia Sele naye kutoa kauli kama ile, lakini yeye alinyamaza.

“Sasa huyu mtoto atakuwa ni wa nani?” Musa akauliza akiwa na maana ya Rama.

Mustafa akabetua mabega yake.

“Mimi nilipima naye damu, nikaambiwa si mwanangu, kwa hiyo simtaki.”

“Na mimi simtaki. Nikimchukua huyo mtoto hata kama atakuwa ni wangu, itakuwa si halali kwa sababu nimezaa na mke wa mtu. Namuachia mwenyewe. Kwaherini.”

Mustafa alipotuambia hivyo, aligeuka na kuelekea kwenye mlango, akaufungua na kutoka. Nikajua zama zangu na Mustafa ziliishia hapo.

“Na mimi nakwenda zangu. Hakuna cha kuniweka tena hapa,” Musa naye akasema, kisha akanitazama.

“Nakwambia tena, nimeshakuacha. Wewe si mke wangu. Kwaheri.”

Musa naye akatoka kwa hasira.

Sikujua Sele naye angeniambia nini. Nilikuwa nikiomba Mungu kimoyo moyo na kutubu makosa yangu ili Sele asiniache kwani alikuwa ndiye tegemeo langu.

Nilipoona Sele yuko kimya, niliinua uso wangu na kumtazama. Nikaona ameinamisha kichwa chake akiwaza.

Baada ya ukimya wa takriban dakika moja, Sele akainua kichwa chake.

“Mishi, naomba nikuulize,” sauti ya Sele ikasikika kama iliyokuwa ikitokea kwa mbali.

“Niulize,” nikamwambia kwa sauti iliyopoteza matumaini.

“Kwanini ulinifanyia hivi?”

Kwanza nilinyamaza kimya kwani sikuwa na jibu. Aliponuiliza kwa mara ya pili, nikamjibu:

“Naomba unisamehe kwa makosa yangu.”

“Swali langu lilikuwa, kwanini ulinifanyia hivi?”

“Sina jibu isipokuwa kukuomba msamaha.”

“Unaniomba msamaha ili iweje?”

“Si nimekukosea, naomba unisamehe.”

“Sikiliza Mishi. Nilikuamini sana na nilikupenda sana. Sikujua kama ulikuwa msichana uliyekosa uaminifu kiasi hicho. Una ujasiri unaotisha na ungeweza kutugombanisha waume watatu kama tusingetumia busara zetu,” Musa aliniambia.

Alinyamaza kidogo kisha akaendelea:

“Kwa mfano, kama Musa au Mustafa angekuja kunifumania na wewe hapa nyumbani, yeye akiamini wewe ni mke wake na mimi nikiamini wewe ni mke wangu, nini kingetokea?”

Sikujibu kitu. Sele akaendelea:

“Si ingekuwa balaa, kwa sababu mimi niliyekuoa mwisho ndiye ningeshikwa ugoni. Je, kama ningeuawa, wewe ndio ungefurahi?”

“Yaliyopita yamepita, mume wangu, hakuna haja ya kuyarudisha tena. Nilikubali unioe kwa sababu nilikuwa nakupenda na sikuwa na njia nyingine.”

“Unaolewa na waume watatu, halafu unaniambia ulikubali nikuoe kwa sababu ulikuwa unaniipenda, na ilikuwaje uolewe na mume wa pili wakati tayari ulikuwa na wa kwanza?”

Mh! Ilibidi ninyamaze. Sikuwa na jibu.

“Mbona hujibu?” akaniuliza.

“Hao waume wawili wameshaniacha, nitabaki na wewe, mpenzi wangu wa zamani,” nikamwambia.

“Huwezi kubaki na mimi. Hivi hujui kuwa ndoa yetu haikuwa ya halali? Wewe si mke wangu. Sihitaji hata kukupa talaka. Wewe ondoka tu uende zako.”

Nikanyanyuka na kumfuata. Nilitaka kumkumbatia niendelee kumuomba msamaha.

“Sele mume wangu, hata wewe unaniambia hivyo wakati ndiye niliyekutegemea.”

Sele hakuniruhusu nimfikie, akaninyooshea mkono kunizuia.

“Huko huko! Nimeshakwambia mimi si mume wako. Kitendo ulichofanya hakistahili msamaha hata chembe. Tafadhali chukua kila kilicho chako uondoke hapa nyumbani. Sitaki kukuona tena,” Sele alisema kwa dhati. Uso wake ulikuwa mtulivu, lakini macho yake yalikuwa yanawaka.

Nikapiga magoti na kusota kumfuta.

“Sele, nisamehe. Rudisha moyo wako kwangu. Naapa kuwa sitakukosea tena.” Sasa nilikuwa nimeilegeza sauti yangu na kuwa kama tulivyokuwa kitandani.

Sele akanyamaza kimya. Nikazidi kumsogelea. Sasa hakunizuia.

“Mimi sijui ni ibilisi gani aliyekuwa amenipata, yaani ninajuta. Lakini ningekupata wapi, Sele, kama ningekwambia nimeolewa… Sele wangu… hebu kumbuka tulikotoka…”

Sele aligeuza kichwa chake upande mwingine, hakutaka kutazamana na mimi. Alionesha kuchukia, lakini sura yake ya ujana haikuwa ya kutisha kama ilivyokuwa ya Musa na Mustafa.

Muda ule nilijua nilikuwa nimemwambia maneno yaliyomchanganya. Kwa vyovyote vile, niliamini alikuwa akifikiria kurudisha moyo wake.

SEHEMU YA 40
“SELE, niambie basi, kama umenisamehe,” nikamwambia nilipoona kimya kimezidi.

Sele hakunijibu chochote. Bila shaka alikuwa akishindana na moyo wake. Upande mmoja wa akili yake ulikuwa ukikubali ombi langu, upande mwingine ulikataa. Nilikuwa kama niliyekuwa nikiyasikia mawazo yake.

“Huyu ni wa kumuacha tu aende zake!” Upande mmoja wa akili yake ulimwambia.
“Hapana, muhurumie mwenzako. Kumbuka mmetoka mbali,” upande mwingine ulijibu.
“Upumbavu huu alioufanya hauvumiliki!” Upande wa kwanza uliendelea kuniwekea ngumu.
“Hapana, usiwaze hivyo; msamehe tu, hatarudia tena. Muangalie jinsi anavyotia huruma,” upande wa pili uliendelea kunitetea.

Na hapo hapo Sele akageuza uso wake na kunitazama mara moja, kisha akaurudisha uso wake kulekule. Niliona macho yake yalikuwa yamepungua ukali, ingawa bado yalikuwa mekundu.

“Muhurumie tu,” nilimsoma alipokuwa akiendelea kusemeshana na akili yake.

Sasa ule upande wa pili wa akili yake, usionitakia mema, haukupinga.

“Nakupenda, Sele,” nikamwambia kwa sauti ya unyenyekevu.

Nilipoona yuko kimya, nilisota hadi kule alikoelekea, nikawa mbele ya macho yake. Masikini Sele, machozi yalikuwa yakimtoka! Nilihisi alikuwa akifikiria kuniacha huku bado ananipenda.

Na mimi, machozi yakanitoka hapo hapo. Nikataka nisogee ili nimkumbatie, kumbembeleze. Lakini akanizuia nisimguse na hapo hapo akainuka.

“Tafadhali niachie,” aliniambia.

Alisimama kando yangu, akanitazama kwa hasira.
“Tafadhali chukua kila kilicho chako uondoke hapa nyumbani,” akaniambia.

“Sele, nikubembelezeje unielewe? Si nimeshakuomba msamaha? Kwanini hutaki kunisamehe? Nimefanya kosa gani kwako lisilosameheka?”

“Sitaki tena kuendelea kusemeshana na wewe. Naomba uchukue kila kitu chako uondoke!” Akaniambia.

Alipoona nimesita nikimtazama kwa uso wa huzuni, Sele aliondoka kwa hatua za haraka akaingia chumbani. Nikatikisa kichwa changu kusikitika kwa sababu nilijua kuwa ule ulikuwa ndio mwisho wangu na Sele.

Sikujua Sele alifuata nini kule chumbani nikamfuata. Nilikuta amefungua kabati, akitoa nguo zangu na kuzitupa juu ya kitanda.

“Ngoja nitoe mwenyewe,” nikamwambia.
“Haya njoo utoe,” akaniambia.

Nikamfuata Sele kimapenzi ili nijaribu kuushawishi moyo wake kwa mara nyingine.
“Tafadhali usinisogelee!” Akaniambia akiwa ameukunja uso wake.
“Sele, usinikatili kiasi hicho, hebu jaribu kurudisha moyo wako, mpenzi wangu.”

Alipoona ninaendeleza maombi yangu aligeukia kabati na kuendelea kutoa nguo zangu.
“Acha. Nitatoa mwenyewe,” nikamwambia.

Akaacha kutoa nguo hizo. Nikatoa mwenyewe nguo pamoja na vitu vyangu vingine vilivyokuwa ndani ya kabati. Baadaye nilizipanga kwenye sanduku. Nilipomaliza, niliinua uso wangu nikamtazama Sele. Na yeye alinitazama. Nikaurudisha uso wangu kwenye sanduku nikalifunga.

“Haya, kwaheri ya kuonana,” akaniambia.

Moyo wangu ulikuwa mzito sana kuondoka pale nyumbani, lakini sikuwa na jinsi. Nikajiuliza, nikiondoka pale nyumbani, nitakwenda wapi wakati shangazi yangu alikuwa ameshakufa? Sikupata jibu.

“Subiri, nioge kabisa tafadhali,” nikamwambia Sele.

Nilipoona amenyamaza, nilijaribu kutumia kete yangu ya mwisho kwa Sele.
Nilivua nguo zangu mbele yake ili niende nikaoge. Nilikuwa na hakika kwa jinsi nilivyoumbika, Sele asingejizuia kunitamani na hivyo kunisamehe.

Sikushughulika kumtazama ili asigundue kuwa nilikuwa namtega; nikachukua taulo na kuingia bafuni. Nilipotoka kuoga, sikumuona Sele chumbani. Nilivaa nguo zile zile, nikachukua masanduku yangu mawili nikatoka nayo.

Nilimkuta Sele sebuleni, akinisubiri. Bila shaka alindoka mle chumbani ili asinione nikiwa mtupu wakati ninatoka bafuni, akihofia kwamba angepata ushawishi.

Alipoona ninatoka na masanduku yangu, alitia mkono mfukoni, akatoa kitita cha noti akanipa shilingi laki moja.
“Zitakusaidia kwa usafiri,” akaniambia.

Nikahisi machozi yakianza tena kunitoka. Hata hivyo niliyafuta kwa mkono wangu, nikamuita mwanangu na kuelekea naye kwenye mlango.

Nilipofika kwenye mlango niligeuka na kumtazama Sele.
“Njoo unifungulie mlango,” nikamwambia.

Japo nilikuwa na masanduku mawili, ningeweza kuweka chini sanduku moja na kufungua mlango, lakini sikutaka kufanya hivyo.

Sele akaja kwenye mlango na kuufungua.

Nikatoka na mwanangu nikiwa na masanduku yangu. Nilipouvuka mlango nilisimama. Nilijiambia pale ndio nilikuwa na nafasi ya mwisho ya kumshawishi Sele.

Nikageuka na kutazamana na Sele aliyekuwa amesimama kwenye mlango.
“Yaani hujanisamehe, Sele?” Nikamuuliza kwa sauti ya kusikitisha ya mtu aliyekata tamaa na anayejaribu bahati yake kwa mara ya mwisho.

Sele alijikaza, akaniambia,
“Sijakusamehe.”

“Haya, kwaheri,” nikamuaga huku nikijaribu kutoa tabasamu.
“Wewe nenda, acha nifikirie. Nikiamua kuwa nimekusamehe nitakutafuata,” Sele akaniambia.

“Utanitafuta, utajua niko wapi?” Nikamuuliza.
“Namba yako ninayo.”
“Sawa,” nilimwambia ‘sawa’ kwa shingo upande.

Nikageuka na kuchanganya mwendo kuelekea barabarani huku mwanangu akinifuata nyuma.
“Yote umeyataka wewe, mwanangu, yasingenikuta,” nikamwambia Rama, lakini nilikuwa kama nikisema peke yangu.

Wakati ninatembea nilikuwa nikijiuliza niende wapi, kwani sikuwa na pa kwenda. Nikafikiria niende kwa rafiki yangu Amina nimdanganye kuwa nimekwenda kumtembelea.

Wazo la kwenda kwa Amina nikaliondoa haraka. Niliona kwa muda mrefu nilikuwa sijafika kwake na, isitoshe, yale masanduku niliyokuwa nayo yangezusha umbea. Amina angegundua mara moja kuwa nilikuwa nimeachika na mimi sikutaka ajue.

Nikaamua kukodi teksi niende nikapangishe chumba cha hoteli ili niweze kutafakari zaidi. Nikakodi teksi na kumwambia dereva anipeleke hoteli yoyote iliyo nzuri. Dereva akanipeleka katika ile hoteli ambayo kabla sijaoana na Sele tulikuwa tunakwenda.

Nilipangisha chumba, nikapanda kitandani na mwanangu. Wakati nikiendelea kuwaza, Rama alishuka kitandani na kuanza kucheza.

Licha ya kuweza kumwambia Musa si baba yake, hakuwa akijua nini kilikuwa kinaendelea. Na hata kama aliona jinsi nilivyokuwa nasutwa na kupewa talaka, yalikuwa yameshamtoka kichwani mwake. Ndio mambo ya kitoto.

Sikutaka hata kumgombesha kwa sababu nilijua hakuwa na akili, na pia mimi ndiye niliyekuwa na makosa, si yeye; kwani alichokisema Rama ndicho alichokuwa anakijua.

Nilimtupia jicho nikamtazama alivyokuwa anacheza, kisha nikatikisa kichwa kusikitika.

Mawazo yangu zaidi yalikuwa kwa Sele. Japokuwa nilikuwa na waume watatu, Sele ndiye niliyekuwa nikimpenda zaidi. Na hata baada ya kuachwa na Musa na Mustafa, tegemeo langu lilikuwa kubaki na Sele.

Kitendo cha Sele kunifukuza nyumbani kwake na kuniambia sikuwa mke wake na sikustahili kupewa talaka, kwa kweli kiliniuma.

Laiti Sele angeujua moyo wangu ulivyokuwa kwake, asingenifukuza nyumbani kwake. Yeye siye niliyemfanyia ubaya. Niliyemfanyia ubaya ni Musa, ambaye kisheria ndiye aliyekuwa mume wangu na ndiye niliyemsaliti.

Mustafa alikuwa amedandia tu gari la watu. Akiondoka ni sawa.

“Sasa wewe, Sele, kitu gani kinakuuma wakati umebaki peke yako?” Nikajisemea peke yangu kama kichaa.

Kumpenda Sele hakukutokana na hofu ya maisha yangu. Nilikuwa nampenda tu. Kimaisha nilikuwa vizuri. Akaunti yangu kwa wakati ule ilikuwa na zaidi ya shilingi milioni thelathini na tano, ambazo ningeweza kufanyia biashara yoyote.

Lakini tatizo langu halikuwa pesa wala biashara; lilikuwa mapenzi ya Sele. 

Nilifikiria kila njia ya kurudi kwake. Upande mmoja wa akili yangu ukanituma niende kwa mganga nikamroge Sele anifuate mwenyewe, tena aje kwa magoti anibembeleze.

Lakini sikuwahi kwenda kwa mganga hata siku moja katika maisha yangu. Hata ile imani ya kuamini vitu vya kishirikina nilikuwa sina. Lile wazo la kwenda kwa mganga lilinijia tu kwa sababu ya kutangatanga.

Nikajiambia siwezi kwenda kwa mganga kumroga mwanaume. Kama mapenzi yetu yameshafikia tamati sikuwa na sababu ya kuhangaika.

Nilikaa pale hotelini kwa siku moja. Mpaka kunakucha siku ya pili nilikuwa nimeshafanya uamuzi wa kurudi Tanga nimuache Rama kisha nirudi tena Dar.

Nilijiambia nitakaporudi Dar ningeweza kuanzisha biashara yoyote itakayoniwezesha kuishi katika jiji hilo.

Nikakodi teksi iliyotupeleka kwenye kituo cha mabasi cha Mbezi, mimi na mwanangu. Nikakata tiketi ya basi la kwenda Tanga.

Sehemu ya 41
WAKATI tumekaa kwenye siti tukisubiri safari, Rama alinishitua aliponiambia.
“Mama! Baba yulee!”
Alikuwa akinionyesha nje ya dirisha. Nikaangalia alikokuwa akinielekeza.
Nikashituka nilipomuona Sele amesimama pembeni mwa basi akitutazama.
Alipoona tunamuangalia aligeuza uso akaondoka mahali pale na kupotea. Nikajiuliza Sele alikuwa akitufuatilia? Au alituona tunaingia ndani ya basi akiwa katika harakati zake mwenyewe?
Sikupata jibu. Lakini nilijiambia huenda alikuwa katika shughuli zake mwenyewe kwani kama alikuwa bado ananipenda asingenifukuza nyumbani kwake.
Nikayaacha mawazo ya Sele ambayo niliona yalikuwa yakiniumiza kichwa bure. Nikaendelea kufikiria maisha yangu.
Muda wa safari ulipowadia, basi likaondoka. Tuliondoka saa nne asubuhi tukafika Tanga saa tisa alasiri.
Kwa vile nyumbani kwetu kulikuwa jirani na stendi ya mabasi, tulikwenda kwa miguu, hatukuwa na haja ya kukodi teksi.
Tulipofika nyumbani nilimkuta shangazi yangu akitokea uani. Shangazi huyo alikuwa mdogo wa shangazi aliyekuwa akinilea huko Dar ambaye alifariki.
“Shikamoo shangazi,” nikamuamkia.
“Marahaba.” Shangazi akaniitikia kwa wasiwasi kama vile hakuwa amenitambua.
“Habari za hapa shangazi?”
“Nzuri, nani mwenzangu? Mishi?”
“Ndiye Mishi.”
“Macho hayaoni vizuri mwanangu, nimekutambua kwa sauti tu. Ndio unatoka Dar?”
“Ndiyo nimeingia sasa hivi.”
“Hajambo mwenzako?”
Shangazi alikuwa amemkusudia mume wangu.
“Nimeachwa shangazi,” nikamwambia.
Shangazi akashituka. Alikuwa anataka kuingia chumbani kwake akasita kwenye mlango.
“Umeachwa?” Akaniuliza kama vile hakuwa amenisikia vizuri.
“Nimeachwa, nimeamuakurudi kwetu.”
“Kisa?”
“Yule mwanamme ni mnayanyasaji sana. Jana usiku alilala nje, leo asubuhi tukagombana akanipa talaka yangu.”
Shangazi akaguna na kunyamaza kwa muda.
“Hamkupata suluhu?”
“Sitaki suluhu na yeye, nimechoka na tabia zake. Atakuja kuniletea ukimwi bure. Bora nirudi kwetu.”
“Makubwa! Haya karibu huku chumbani.” Shangazi akaniambia huku akiingia chumbani kwake.
Nikamfuata humo chumbani pamoja na masanduku yangu. Niliyaweka chini nikamwambia Rama.
“Mwamkie bibi.”
“Shikamoo bibi.” Rama akamwamkia shangazi.
“Marahaba mjukuu wangu, hujambo?”
“Sijambo.”
“Mwanao amekuwa mvulana sasa.”
“Ndio nimekuletea mjukuu wako.”
“Nimesikitika sana ulivyoniambia umeachwa. Sisi zamani mume akiacha mke, mke huondoki kwa mume mpaka ipite miezi mitatu na mume anakuwa na jukumu la kukupatia mahitaji yako kama mke wake. Ikipita miezi mitatu kama hajakwambia amekurudia, ndio unaondoka.” Shangazi akaniambia.
“Sheria hiyo haipo siku hizi. Mume akikuacha anakufukuza hapo hapo.”
“Ni kosa lakini huenda akarudisha moyo akakufuata.”
Shangazi aliponiambia hivyo nilinyamaza kimya. Sikutaka kumueleza ukweli juu ya kuachwa kwangu kwani angeshangaa. Niliona nidanganye ili nijipe sheria huku nikijua kuwa si Musa wala Mustafa ambaye angeamua kunifuata.
Baada ya mazungumzo marefu na shangazi, nilifagia chumbani kwake nikatoa nguo zake pamoja na zangu ambazo zilihitaji kufuliwa nikazifua.
Mbali na shangazi yangu kulikuwa na ndugu zangu wengine ambao tulikutana baada ya kurudi kutoka kwenye shughuli zao.
Siku ile mlo wa usiku pale nyumbani niliugharamikia mimi. Niliagiza kilo moja ya nyama na mchele kilo mbili.
Kwa vile nyumba yetu ilikuwa na nafasi, nilipata chumba cha kulala na mwanangu.
Nilikuwa nimepanga nikae siku mbili kisha nimuache mtoto nirudi Dar lakini nilishindwa kuondoka haraka kwa sababu sikuwa na mtu wa uhakika wa kumuachia mwanangu. Shangazi yangu mwenyewe alikuwa mtu mzima na alikuwa haoni vizuri, nisingeweza kumuachia mwanangu.
Ndugu zangu wengine walikuwa na shughuli zao. Ilikuwa vigumu kuwaambia kuwa nawaaachia mwanangu wamlee. Nikajikuta nikiendelea kukaa pale.
Pale barazani mwa nyumba yetu palikuwa na dada yangu mmoja akiendesha biashara yake ya kahawa na kashata kila ifikapo jioni.
Alikuwa ameweka meza yake na mabenchi ya kukalia ambapo wanywaji kahawa hufika kujipatia kahawa na kashata. Mara nyingi ninakaa naye na kumsaidia kuuza kahawa.
Siku moja aliniambia alikuwa akijisikia kuumwa akaniacha nimuuzie kahawa yake, yeye mwenyewe akarudi ndani kujipumzisha. Nilikuwa nampimia mtu mmoja kahawa nikaona gari likisimama mbele yetu. Nikalitambua lilikuwa gari la Sele.
Ghafla nikamuona Sele akishuka kutoka kwenye gari hilo. Nilishituka sana kumuona. Nikawa nimeduwaa kumtazama kijana huyo ambaye sikutegemea tena kumuona maishani mwangu.
Alifunga mlango akanifuata kwenye meza.
“Hujambo Mishi?” Alinisalimia huku akiketi kwenye benchi. Uso wake ulikuwa ukitabasamu.
“Sijambo Sele. Unatoka wapi?”
“Natoka Arusha, nimekufuata wewe.”
“Umenifuta mimi?”
“Ndio nimetamani kahawa yako na kashata za Tanga.” Nikajua Sele ananitania.
Nikatabasamu.
“Karibu,” nikamwambia. Nilimtilia kahawa nikampa na kashata.
Aliionja kahawa kisha akangata na kashata.
“Umeanzisha mradi wa kahawa na kashata?” Akaniuliza.
“Namuuzia dada yangu.”
“Nimekuja kukuchukua,” akaniambia.
“Twende wapi?”
“Turudi nyumbani.”
“Umeshanisamehe?”
“Yaliyopita yameshapita. Nimekosa amani kwa kipindi chote.”
Aliponiambia hivyo nilikuwa nimeshika birika ya kahawa ili nimtilie yule mtu mwingine. Mwili ulinisisimka, birika ikaniponyoka mikononi. Nikajikuta nikikurupuka kumfuata huku nikiipeleka mbele mikono yangu kama ninayepokea mgeni.
Sele aliponiona najipeleka kwake alisimama. Nikamkumbatia na kuizungusha mikono yangu nyuma ya shingo yake. Sikuona aibu watu waliokuwa wakitutazama.
Sele naye aliizungusha mikono yake na kukishika kiuno changu kilichokuwa kimejaa hamu ya kushikwa na yeye. Tukaungana na kuwa kama kitu kimoja.
Yule mtu aliyekuwa akisubiri nimpimie kahawa alikuwa ameshangaa akitutazama.
Sele alikuwa anataka kuniachia baada ya kupigana mabusu kwa sekunde kadhaa.
“Nishike usiniachie, nitaanguka,” nilimwambia. Mwili wote ulikuwa umenilegea.
“Imetosha.” Sele aliniambia huku akiniachia kidogokidogo.
“Nakupenda Sele,” nikamwambia na kuongeza:
“Umenitesa sana.”
“Ndio sababu nimekufuata, sheikh aliniambia ni lazima tuoane upya. Ile ya kwanza hakikuwa ndoa halali.”
“Usijali mpenzi wangu tutaoana hapa hapa.”
“Natumaini umejifunza vya kutosha.”
“Sitarudia tena upumbavu ule.”
“Ninakuamini.”
Aliponiambia hivyo nikamg’ang’ania tena.
Barazani kwetu watu walikuwa wametoka wakiangalia sinema ya bure kati yangu na Sele. Nikamuachia Sele kisha nikamshika mkono na kuingia naye ndani.
Siku  ile Sele alikwenda kulala gesti. Siku ya pili yake tukaoana tena pale nyumbani. Siku ileile tukaondoka kurudi Dar pamoja na mwanangu.
Tulipofika nyumbani kwetu Dar, Sele hakuacha kunieleza hisia zake.
“Nilikuwa nashindwa kufanya kazi zangu kila nilipokukumbuka. Tangu siku ile nilikuwa nashindana na moyo wangu kuhusu suala lako, mpaka juzi nikaamua kukufuata.”
“Ulikuwa ukiumia eh?” Nikamuuliza kwa sauti ya taratibu.
“Sana!” Sele akaniambia kwa mkazo.
“Ni kwa sababu ulitambua kuwa hata mimi nilikuwa nakupenda na sikuwa na ubaya na wewe. Wa kunilaumu mimi alikuwa mume wangu wa kwanza.”
“Usiseme hivyo. Siku moja kabla ya kukufuata Tanga nilikwenda kwa mwanasheria mmoja kumuelezea matatizo uliyoyasababisha, akaniambia tunaweza kukushitaki. Aliniambia kosa ulilofanya ni kubwa. Ungetakiwa kutufidia sisi sote na bado ungekabiliwa na kifungo kisichopungua miaka saba.”
Sele aliponiambia hivyo nilishituka sana. Kumbe kama Musa na Mustafa wangeamua kwenda mahakamani ningekiona cha moto!
“Siku ile tulipokuwa tunarudi Tanga tulikuona katika kituo cha mabasi cha Mbezi. Ulikuwa unatufuatilia sisi?”
“Nilikuwa nikiwafuatilia, moyo wangu ulikuwa hautaki nikuache lakini niliushinda.”
“Pole,” nikamwambia Sele kwa sauti laini.
“Nimeshapoa lakini nilikiona cha moto.”
“Na mimi pia nilikiona,” nilizidi kumlegezea sauti.
Sele hakuvumilia. Kilichofuata baada ya hapo ninakijua mimi na Sele.
Hadi hii leo ninaposimulia kisa hiki bado ninaishi na Sele kama mke na mume. Nimeshamzalia Sele watoto wawili mapacha, wote wanaume. Sele alifurahi kupindukia kuwapata watoto hao.
Mwenzenu hivi sasa nimekuwa mke muaminifu. Sitamani mwanaume hata aweje. Namtamani Sele peke yake. Na nimeapa kuwa sitatoka nje ya ndoa yangu.