Bitegeko Asema Makundi Yamekwisha Muleba Kaskazini, Aahidi Kampeni za Kisayansi Muleba Kaskazini

Na Diana Deus-Muleba.

Mteule wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Muleba Kaskazini, Adonis Alfred Bitegeko, ameanza rasmi safari yake ya kisiasa kwa kutoa shukrani za dhati kwa wananchi wote wa Muleba, wajumbe wa CCM kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi Taifa, pamoja na watia nia aliokuwa akichuana nao katika mchakato wa kura za maoni.

Mamia ya wananchi wa Jimbo la Muleba Kaskazini walijitokeza katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba na kuongozana naye hadi Ofisi za CCM Muleba, ambapo mbele ya wananchi, Bitegeko alisisitiza kuwa ushindi wa kweli unaweza kupatikana endapo kila mmoja ataweka maslahi ya Muleba mbele ya maslahi binafsi.

Ameahidi kushirikiana na kila mdau na wananchi wote, pamoja na wagombea wote aliochuana nao katika mchakato wa kura za maoni, kwa lengo la kujenga mshikamano utakaochangia maendeleo ya Wilaya ya Muleba na Mkoa wa Kagera kwa ujumla.

“Leo tunavunja makundi. Tunaanza ukurasa mpya wa mshikamano. CCM ni chama kimoja, na Muleba Kaskazini ni familia moja. Ni lazima tushirikiane kwa dhati ili tufanikishe maendeleo ya wananchi wetu. Na hapa ni kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja,” amesema Bitegeko

Aidha, amesisitiza kuwa kampeni za mwaka 2025 zitakuwa za kisasa, zenye kujikita katika kuhamasisha maendeleo, mshikamano, na ushiriki wa wananchi wote bila kubagua. Amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kuwachagua Rais, Mbunge na Diwani wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi.