Shinyanga. Wananchi wa Kata ya Itwangi, Halimashauri ya Wilaya ya Shinyanga, mkoani Shinyanga, wameiomba Serikali kuweka matuta katika barabara kuu ya eneo hilo kufuatia wimbi la ajali zinazodaiwa kusababisha vifo vya watu, wakiwemo wanafunzi.
Wananchi hao wamesema ajali zimekuwa zikijirudia mara kwa mara kutokana na madereva kuendesha kwa mwendo kasi na kutokuheshimu alama pamoja na vivuko vya barabarani vilivyopo.
Wakizungumza Agosti 24, 2025, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, katika ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi, wakazi hao walisema ajali ya hivi karibuni ilitokea Agosti 7, 2025 na kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja.
“Butu Nkinga, mkazi wa eneo hilo, alisema: ‘Hii barabara inamaliza watu wetu, watu wazima na watoto, hasa wanafunzi. Ajali ni nyingi kwa sababu madereva wanaendesha kwa kasi na hawafuati sheria. Tunaomba Serikali iingilie kati kutuokoa.”
Naye Kapela Msafiri aliunga mkono hilo akisema: ‘Naomba Serikali iweke matuta kwa sababu kila dereva ana akili zake. Wengine hufuata sheria, lakini wengine siyo. Hii barabara inatuangamiza.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Itwangi, Kisendi Lubinza, alisema ajali zimekuwa kero kubwa kwa wananchi na kusisitiza kuwa serikali haina budi kuchukua hatua za haraka.
“Wananchi wamezungumza mambo mengi lakini mimi nasisitiza hili la ajali. Jamani tutaisha kwenye hii barabara kama hakuna hatua itakayochukuliwa. Tunaomba sana matuta,” alisema Lubinza.

Akijibu malalamiko hayo, Mtatiro, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa Serikali itashirikiana na kamati husika kuangalia namna bora ya kuipatia suluhu.
“Mlitaka lami lakini pia lami hii imekuwa ni chanzo cha kero nyingine, ni wajibu wa Serikali kusikiliza na kutatua kero za wananchi hili la ajali na mwendokasi wa madereva tumelibeba na tunaenda kulifanyia kazi na kamati husika” alisema Mtatiro.