WAKATI Mbeya City ikiendelea na mazungumzo na uongozi wa klabu ya KVZ ili kuondoka na beki wa kikosi hicho, Juma Hassan Shaaban ‘James’, timu ya Pamba Jiji nayo imetupa kete yake kuitaka saini hiyo.
Taarifa ilizozipata Mwanaspoti zinaeleza, Mbeya City ilikuwa ya kwanza kuzungumza na KVZ na kukwamia katika majadiliano ya dau, hivyo kuna uwezekano wa Pamba Jiji kumsajili beki huyo endapo muafaka utapatikana kwa haraka.
Wakati hayo yakijiri, beki huyo amekosekana katika mazoezi ya KVZ inayojiandaa kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Zanzibar huku timu hiyo ikiwa na wiki sasa ikijifua, jambo lililolifanya Mwanaspoti limtafuta James kutaka kujua sababu ya kutoonekana.
James alisema, kilichomfanya asiwepo kikosini hapo ni baada ya kupewa taarifa ya kuwa uongozi wake upo katika mazungumzo na Pamba Jiji.
“Ni kweli sijafika mazoezini, kwani uongozi wangu umenitaka nisubiri kwanza upo katika mazungumzo na timu ya Pamba inayohitaji huduma yangu, kwa hiyo nitapewa muongozo baadaye,” alisema James.
James alisema timu ambayo itafika makubaliano na uongozi wake kati ya hizo mbili yupo tayari kuitumikia kwa nguvu zake zote kwa sababu uwezo wa kufanya hivyo anao.
Beki huyo alisema sio tu timu za Tanzania Bara, hata za visiwani hapa ikiwa ipo ambayo inamtaka isisite kuzungumza na uongozi wake.
Endapo Pamba Jiji itafanikiwa kuinasa saini ya beki huyo, itakuwa imesajili nyota wa pili kutoka Zanzibar baada ya kumchomoa mshambuliaji wa timu ya Mlandege, Abdallah Iddi ‘Pina’ ambaye alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2024-2025.