Bado Watatu – 3 | Mwanaspoti

“HUMU ndani asiingie mtu yeyote. Tutarudi tena. Sawa?”

“Humu ndani mnaishi watu wangapi?”

“Ukiacha marehemu ambaye hakuwa na mke wala watoto, tuko familia tatu.”

“Mwenye nyumba anaishi hapa hapa?”

“Mwenye nyumba hakai hapa.”

Nikatoka katika kile chumba pamoja na yule mtu. Polisi walikuwa wametangulia kutoka. Nikamuamrisha yule mtu afunge ule mlango.

“Hakikisha hakuna mtu anayeingia humu chumbani,” nikamsisitizia mtu yule baada ya kuufunga mlango.

“Sawa. Hakuna mtu atakayeingia.”

Tukatoka nje. Polisi wenzangu walikuwa wakinisubiri. Nikawaagiza waupeleke ule mwili hospitalini. Mimi nikajipakia kwenye gari nililokwenda nalo na kuondoka nikiwa na vile vitu nilivyovichukua kutoka katika mifuko ya marehemu.

Dakika chache baadaye nikawa kwenye ofisi ya ofisa upelelezi wa mkoa.

“Ndiyo ninarudi kutoka mahali ulikoniagiza,” nikamwambia ofisa huyo wakati ninakaa kwenye kiti.

“Ndiyo. Mmeshaushughulikia mwilli wa marehemu?”

“Tumeushughulikia na nimewaacha polisi wanaupelekeka katika hospitali ya Bombo. Ni kweli hilo tukio limetokea. Uchunguzi wetu wa awali umeonyesha kuwa marehemu amenyongwa.”

“Amenyongwa katika mazingira gani na amenyongwa na nani?”

“Tumeukuta mwili wake ukining’inia kwenye kitanzi chumbani mwake huku mlango ukiwa umefungwa kwa ndani. Tulilazimika tuvunje mlango ili tuweze kuingia ndani.”

“Kama mlango ilifungwa kwa ndani, kwanini unaamini kuwa amenyongwa na hakujinyonga mwenyewe?’

“Nilitarajia afande ungeniuliza swali hilo. Hata mimi nilijiuliza swali hilo nilipofika katika eneo la tukio. Jibu lake ni kwamba tumegundua kwamba amenyongwa kutokana na mambo kadhaa,”

“Nitajie moja baada ya jingine.”

“La kwanza ni kwamba nimepata maelezo kwamba marehemu alikuwa na mwenzake aliyekuwa naye chumbani mwake usiku uliopita. Nimeelezwa kwamba sauti zao zilisikika wakizungumza hadi saa sita usiku na hata tulipovunja mlango tulikuta chupa tupu za bia, hali iliyoonyesha kuwa walikuwa wanakunywa pombe.”

Wakati wote nikimueleza ofisa huyo alikuwa akitingisha kichwa kuonyesha kunikubalia.

“Sasa nilichohisi mimi ni kwamba huyo mtu alimngojea mwenzake alipolewa akamnyonga kisha akatoka kwa kuparamia ukuta na kushukia ukumbini. Chumba cha marehemu hakikuwa kimewekewa dari.”

“Je, waliokupa maelezo walikwambia huyo mtu aliyekuwa na  marehemu chumbani ni nani?”

“Hajafahamika isipokuwa walisikia tu sauti yake.”

“Sasa huyo ndiye mtuhumiwa wetu namba moja.”

“Kwa hiyo hadi hapo tumeshagundua kuwa marehemu alinyongwa na mtu aliyekuwa naye chumbani. Kitendo cha kufunga mlango kwa ndani na yeye kutoka kwa kuparamia ukuta kinaonyesha kuwa alitaka isitambulike mapema kuwa marehemu amenyongwa mle chumbani. Lakini pia tulikuta kitu kilichotushitua.”

“Tulikuta kipande cha karatasi katika shingo ya marehemu kilichoandikwa, Bado Watatu.”

Nilikitoa kile kipande cha karatasi kutoka kwenye mfuko wangu wa koti na kumpa.

Alipokisoma na yeye alishituka kidogo.

“Umetafsiri kitu gani kutokana na maneno haya?” akaniuliza.

“Nimetafsiri kwamba kuna watu watatu ambao nao watauawa.”

“Halafu hapa chini kuna saini na alama ya dole gumba!”

“Naamini ni saini ya huyo muuaji pamoja na alama yake ya dole gumba.”

“Kwanini aweka sahihi yake na alama ya dole gumba?”

 “Nafikiri ni jeuri yake tu. Lakini nitaifanyia uchunguzi hii alama ya dole gumba pamoja na sahihi. Inawezekana ameweka alama ya dole la marehemu ili kutubabaisha.”

Ofisa upelelezi akanikubalia kwa kichwa.

“Umegundua sababu ya huyo mtu kumnyonga mwenzake na kuandika kwamba bado watatu?”

“Sasa ninakupa kazi. Hii itakuwa kazi yako ya kwanza ukiwa inspekta. Mtafute huyo mtu umkamate kabla hajanyonga watu wengine. Tunataka atueleze wamemkosea nini hao watu na ni kina nani.”

“Nimekuelewa afande.”

“Ni muhimu pia kujua huyu mtu aliyenyongwa ni nani anafanya kazi gani na ndugu zake ni kina nani.”

“Unapochunguza kumjua mtu aliyeuawa unaweza kupata sababu za yeye kuuawa na kukurahisishia kumpata muuaji.”

“Ninafahamu afande. Hiyo kazi iko ndani ya uwezo wangu.”

“Ni lini unatarajia kuimaliza kazi hii?”

“Nipe wiki moja afande.”

“Baada ya wiki moja utakuja kunieleza ulichogundua. Sasa nakutakia kazi njema.”

Nikainuka kutoka kwenye kiti na kumuaga ofisa huyo kisha nikatoka ofisini mwake.

Nikiwa ndani ya ofisi yangu nilianza kutafakari kuhusu hatua za kuchukua. Hatua ya kwanza niliyopanga ni kuwahoji wakazi wa nyumba ile lilipotokea tukio ili maelezo yao yaweze kunisaidia katika upelelezi wangu.

Nikatoka tena ofisini na kurudi tena Kisosora katika ile nyumba. Bado nilikuta watu waliokuwa wamezagaa barazani.

Nikasimamisha gari na kushuka. Yule mtu aliyetupa maelezo mara ya kwanza alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa hapo. Aliponiona ninashuka kwenye gari akanifuata.

“Umerudi?” akaniuliza.

“Ninataka kuonana na baadhi ya wakazi wa humu ndani ukiwamo wewe.”

“Mimi nipo. Mwenzangu mmoja amefika sasa hivi, alikuwa ametoka kidogo. Na wengine wapo makazini mwao mpaka jioni ndio wanarudi.”

“Sawa. Hebu twende ndani.”

Tukaingia ndani ya ile nyumba.

“Nadhani unakumbuka kwamba nilikuagiza asiingie mtu katika chumba hiki.”

Nikamwambia mtu huyo wakati tukiwa ukumbini.

“Hakuna mtu yeyote aliyeingia tangu mlipoondoka.”

Kwa vile mlango huo niliuvunja haukuweza kufungika kwa kitasa, nikausukuma na kuingia ndani ya chumba hicho.

Awamu ya kwanza nilipoingia katika chumba hicho ilikuwa ni ya kushughulikia mwili wa marehemu, awamu hii sasa ilikuwa ni ya upelelezi.

Nilivyoingia nilianza kukikagua kile chumba. Ile meza iliyokuwa na chupa za bia ilikuwa chini ya mahali ambapo yule mtu alinyongwa. Nikapata picha kwamba aliyemnyonga mwenzake alipanda katika meza hiyo ambayo ilimuwezesha kumtia mwenzake kwenye kitanzi.

Kwa vile mwenzake huyo alikuwa amelewa na pengine alilewa sana, ilikuwa rahisi kwa muuaji kuweza kumtia kwenye kitanzi na kumnyonga.

Pia niligundua sehemu ya ukuta ambayo mtu huyo alitokea baada ya kufanya tukio hilo. Niliona stuli ilikuwa imesogezwa kwenye kabati lililokuwa limegamizwa kwenye ukuta.

Nikajiambia muuaji alikanyaga katika stuli hiyo kisha akapanda juu ya kabati kabla ya kufikia mwishoni mwa ukuta na kupituka upande wa ukumbini.

Nilifungua kabati hilo na kuchunguza ndani. Mlikuwa na nguo chache za kiume. Sikuona kitu kingine kilichonipa udadisi. Nikalifunga.

Baada ya hapo nilikaa kwenye sofa nikamwambia yule mtu kwamba nilitaka anipe maelezo yake kuhusu lile tukio. Na yeye akakaa kwenye sofa jingine.

Nilitoa notibuku yangu na kalamu kisha nikamuuliza.

“Uliniambia unaitwa nani?”

“Naitwa Alphonce Kabendera.”

Nikaandika jina hilo kwenye notibuku yangu na kuendelea kumuulliza.

“Miaka arobaini na mitano”

“Wewe na marehemu nani alianza kukaa katika nyumba hii?”

“Marehemu alifika katika nyumba hii mwaka gani?”

“Sidhani kama amekamilisha mwaka. Labda niseme ana kama miezi tisa hivi tangu apange chumba katika nyumba hii.”

“Alisema alitokea wapi?”

“Yeye ni mkazi wa hapa hapa Tanga.”

“Hakuwahi kutuambia alikotokea”

“Labda aliwahi kuwaambia kwao ni wapi?”

“Hilo pia hakuwahi kutueleza.”

“Alikuwa akifanya kazi gani?”

“Kwa mujibu wa maelezo yake alikuwa na ofisi iliyokuwa ikishughulika na udalali wa nyumba, viwanja na mashamba.”

“Ofisi yake iko wapi?’

“Sikuwahi kumuuliza ofisi yake iko wapi?”

“Alikuwa anapenda kunywa pombe?”

“Aliyemnyonga huyu mtu itakuwa ni rafiki yake ambaye alikunywa pombe naye jana usiku.”

“Ni kweli. Na niliwasikia wakizungumza hadi karibu saa sita usiku nilipopitiwa na usingizi. Sasa sijui kama waligombana baadaye…!”

“Kutoka na mazingira ya tukio lenyewe pamoja na kile kikaratasi tulichokikuta katika shingo ya marehemu, inaonekana haya mauaji ni ya kupanga. Yule mtu alikuwa amedhamiria kumnyonga mwenzake.”

“Sasa kosa lake lilikuwa nini?”

“Kama kuna kosa analijua aliyemuua mwenzake, sisi tunataka kuwapata marafiki zake. Ninyi wakazi wenzake ndio mtakaotuonyesha hao marafiki zake.”

“Kwa kweli hatuwafahamu. Kama nilivyokwambia huyu mtu ana muda mfupi tu katika nyumba hii, isitoshe anapotoka asubuhi anarudi usiku labda siku za Jumapili ndio anachelewa kutoka.”

Hapo hapo nikakumbuka kitu. Moyo wangu ukafarijika. Nikajiambia sasa nimeshamgundua muuaji!

Muuaji nitamkamata kwa kutumia alama zake za vidole, niliendelea kujiambia.

Pale kwenye meza palikuwa na bilauri mbili na chupa tupu kadhaa za bia. Bilauri moja alikuwa akiitumia muuaji na nyingine marehemu. Kwa hiyo ni lazima alama zao za vidole zitakuwa zimeshika katika bilauri  zile kwa vile glass zinanasa kirahisi alama za vidole na hukaa kwa muda mrefu.