Unguja. Wakati Tanzania ikiendelea kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, kundi la vijana wa Pangawe, Unguja, limebuni teknolojia ya kutumia maganda ya miwa kuzalisha mkaa mbadala.
Ubunifu huo unatajwa kuwa suluhisho muhimu kwa kulinda mazingira, kuboresha afya za watumiaji na kutoa ajira kwa vijana.
Ripoti ya Hali ya Mazingira Zanzibar ya mwaka 2021 inaonesha kuwa, zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa vijijini hutegemea kuni na mkaa wa miti kwa ajili ya kupikia, hali inayosababisha ukataji mkubwa wa miti.
Sensa ya misitu ya mwaka 2023 imebaini kupungua kwa ujazo wa misitu ya mikoko kutoka mita za ujazo 41 mwaka 2013 hadi 18.9 kwa Unguja, na kutoka mita za ujazo 39.8 hadi 38.3 kwa Pemba, mtawalia.
Upotevu huo unakadiriwa kufikia wastani wa asilimia 1.2 kwa mwaka, sawa na hekta 1,277, kutokana na ujenzi, uchomaji mkaa, maendeleo ya miundombinu na mabadiliko ya tabianchi.
Serikali imesisitiza azma ya kupanda miti mipya kwa kushirikiana na jamii ili kurejesha misitu iliyoharibiwa, sambamba na kusukuma mbele matumizi ya nishati safi.
Hata hivyo, utekelezaji wake umekuwa ukikwamishwa na changamoto za gharama, upatikanaji wa vifaa na mitazamo ya wananchi.
Katika hali hiyo, ubunifu wa vijana wa Pangawe unaibuka kama suluhisho bunifu na endelevu, linalosaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa wa miti huku likiunga mkono jitihada za kitaifa za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Jinsi mkaa huo unavyotengenezwa
Mhandisi wa Mazingira, Michael Alfred, anasema walifanya tafiti kuhusu aina mbalimbali za taka zinazoweza kuzalisha nishati mbadala na kubaini kuwa, maganda ya miwa ndiyo rahisi zaidi kupatikana Zanzibar kutokana na biashara kubwa ya juisi ya miwa.
Maganda hayo yanachakatwa kuwa mkaa kupitia mchakato wa kukausha, kuchoma na kuchanganya na unga wa mihogo ili kupata bidhaa bora inayoshikamana.
“Maganda mabichi ya mua yakikaushwa kwa jua, huchukua kati ya siku moja hadi tatu kukauka kutegemea unyevu wake. Baada ya hapo huingizwa kwenye pipa maalumu kwa ajili ya kuchomwa kidogo (carbonization) na baadaye kusagwa kuwa unga. Hatua inayofuata ni kuchanganya unga huo na unga wa mihogo uliopikwa kwa ajili ya kuushikamanisha,” anasema Michael.
Kila kilo tatu za unga wa muhogo huchanganywa na kilo 50 za unga wa miwa, matokeo yake ni mkaa mbadala wenye mwako wa kudumu na usio na moshi mwingi. Kilo moja ya mkaa huu huuzwa Sh1,000 na wateja wake ni pamoja na wananchi wa kawaida na hoteli.
“Kiwango hicho kinaweza kupika kwa kutwa nzima chakula cha familia ya watu chini ya watano,” anafafanua.
Michael anabainisha kuwa, mradi huu ulianza mwaka 2023 na unatarajiwa kuendelea hadi mwishoni mwa 2025, ukiwa na lengo la kutoa nishati nafuu, kupunguza takataka mitaani na kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaochochewa na mkaa wa miti.
Mradi huu umeajiri vijana zaidi ya 30 na kuwapa kipato cha kuendesha maisha.
Abdulmalik Seif Issa, katibu wa kikundi hicho, anasema mbali na faida za kiuchumi, vijana wamepata ujuzi wa kipekee utakaowasaidia kuendeleza ubunifu huo hata nje ya kikundi.
“Tunajivunia kuona vijana wakijiajiri kupitia teknolojia hii. Ingawa soko bado ni dogo, tunaona mwamko unaongezeka polepole. Baadhi ya mamalishe na hoteli tayari wananunua mkaa wetu,” anasema Abdulmalik.
Mbali na kupunguza utegemezi wa misitu, mkaa wa miwa unatajwa pia kuwa bora kiafya kwa kuwa, hauna moshi mwingi unaosababisha magonjwa ya mfumo wa hewa.
Mwingine ni Aisha Badulla, mkazi wa Mwembetanga na mmoja wa wateja wa mkaa huo anasema, “ni mkaa mzuri, hauishi haraka kama ule wa kuni, hauna moshi na hautoi uchafu. Ningependa wananchi wengi zaidi wapewe elimu ya kutumia nishati hii.”
Changamoto zinazokabili mradi
Pamoja na mafanikio haya, kikundi kinachozalisha mkaa wa miwa kinakumbana na changamoto kadhaa.
Abdulmalik Seif Issa anasema kwanza ni uhaba wa mashine; kwa sasa wanayo mashine moja tu, hali inayosababisha foleni kubwa na kuchelewesha uzalishaji. Pili ni ukosefu wa soko maalumu, jambo linalowafanya kuendelea kutumia mbinu za kuelimisha jamii kupitia vipeperushi na maonesho.
Aidha, wananchi wengi bado hawana imani na mkaa huu, wakihofia hautaweza kuchukua nafasi ya mkaa wa miti waliouzoea. Kikundi pia hakina ofisi maalumu ya kufanyia kazi, jambo linalopunguza ufanisi na usalama wa shughuli zao.
Yussuf Seif Issa, mkufunzi wa mradi huo, anaamini Serikali ikiweka mazingira wezeshi, mradi huu unaweza kukua na kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya nishati safi Zanzibar. “Tunaiomba Serikali itupe eneo maalumu kwa ajili ya kujenga kiwanda, sambamba na kutusaidia kupata masoko ndani na nje ya nchi,” anasema.
Msaada wa serikali na taasisi
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imesisitiza kuwa itaendelea kuwapa kipaumbele vijana wabunifu.
Waziri Tabia Mwita Maulid anasema: “Tutahakikisha vijana wanaojituma na kubuni miradi ya ajira wanapata msaada wa fedha na pia kuwatafutia masoko ili kukuza huduma zao.”
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Salum Amer, anasema baraza linahamasisha vijana kuchangamkia fursa kama hizi na linawasilisha changamoto zao serikalini ili zipatiwe ufumbuzi.
Hitaji la mabadiliko ya haraka
Kwa mujibu wa wataalamu, iwapo mkaa mbadala wa maganda ya miwa utapewa msukumo wa kutosha, unaweza kuchukua nafasi kubwa katika kupunguza utegemezi wa nishati chafu.
Michael anasema hiyo ni muhimu kwa kuwa, upotevu wa misitu si tu unachochea mabadiliko ya tabianchi bali pia unaathiri usalama wa chakula na vyanzo vya maji.
Wakati Serikali ikiendeleza mikakati ya kitaifa ya nishati safi, miradi ya ubunifu wa vijana kama huu inatajwa kuwa chachu ya mabadiliko.
“Kitu cha msingi kinachohitajika sasa ni elimu ya kutosha kwa wananchi, uwekezaji wa kifedha, vifaa vya kisasa na sera zinazowezesha soko la bidhaa hizi mbadala,” anasema.
Katika sura ya kwanza ya Utangulizi ya Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya nishati Safi ya Kupikia 2024 – 2034, kwenye matokeo yanayotarajiwa ua mkakati huu namba nne ni, “kuongezeka kwa wigo wafiti na ubunifu wa teknolojia zinazohusu nishati yakupikia.”
Pia, hili linatajwa kama miongoni mwa dhima ya mkakati huu katika sura ya tatu, ikiashiria Serikali imepanga kuunga mkono tafiti kama hii.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.