KADHALIKA katika chupa hizo pia kutakuwa na alama zao za vidole kwa vile kila mmoja alikuwa akishika chupa na kujimiminia.
Baada ya kuwaza hivyo niliinuka nikaenda pale kando ya meza na kuzitazama zile bilauri bila kuzigusa. Nikahisi kwamba alama zao zilikuwepo.
Nikatoa kitambaa kutoka mfukoni mwangu na kumwambia mwenyeji wangu anipatie mfuko ili nitie zile bilauri pamoja na chupa kadhaa.
Mwenyeji wangu alitoka mle chumbani. Baada ya muda kidogo alirudi akiwa ameshika mfuko wa nailoni.
“Huu utafaa?” akaniuliza.
“Utafaa sana, ulete.”
“Ukunjue nitie hizi bilauri.”
Mtu huyo akaukunjua mfuko huo nikaziokota zile bilauri kwa hadhari kwa kutumia kitambaa kisha nikazitia ndani ya ule mfuko. Pia niliokota chupa nne, nazo nilizitia kwenye mfuko huo.
Baada ya hapo niliushika ule mfuko nikamwambia yule mtu.
“Nitahitaji kuonana na wapangaji wote wa nyumba hii. Labda kwa kesho au keshokutwa. Kwa leo acha niende nikashughulikie hizi chupa.”
“Sawa. Nimekuelewa lakini jambo moja linanitatiza kidogo”
“Hizo chupa na bilauri unakwenda kuzishughulikia kivipi?”
“Ni mambo ya kipolisi. Nitakuja kuwaambia.”
Nikatoka mle chumbanni nikiwa na mfuko wangu wa nailoni.
“Hiki chumba bado kina karantini. Mtu yeyote haruhusiwi kuingia. Sawa?”
Nikatoka nje na kujipakia kwenye gari. Nililiwasha na kurudi kituo kikuu cha polisi.
Nilishuka kwenye gari hilo nikaingia kituoni na kwenda moja kwa moja katika ofisi iliyokuwa ikishughulika na uchukuaji wa alama za vidole ambayo ilikuwa chini ya Sajin Meja Ibrahim.
Nilifurahi nilipomkuta ofisa huyo akisoma gazeti.
Kwa vile kicheo nilikuwa mkubwa kwake, aliponiona alisimama na kunipigia saluti.
Hakukaa tena kwenye kiti.
“Karibu afande,” akaniambia.
“Asante. Kaa kwenye kiti,” nikamwambia huku na mimi nikiketi kwenye kiti cha wageni.
Niliuweka ule mfuko juu ya meza. Nikatoa kitambaa na kuzitoa zile bilauri pamoja na chupa.
“Kama umesikia kuna mtu amenyongwa jana usiku huko Kisosora?”
“Uchunguzi wake uko mikononi mwangu. Nimeelezwa kuwa aliyenyongwa na aliyemnyonga mwenzake wote wawili walikunywa pombe chumbanni kwa marehemu hadi usiku mwingi. Baaada ya hapo inasemekana mmoja alimnyonga mwenzake na kutoweka. Umenielewa?’
“Nimekuelewa afande.”
“Sasa huyo mtu hafahamiki ni nani. Wenyewe walikuwa wanakunywa chumbani. Sauti zao ndizo zilizokuwa zinasikika. Kwa hiyo nimechukua….”
“Ngoja nikukatishe kidogo. Kama walikuwa wanakunywa pamoja, hao watu watakuwa wanafahamiana!”
“Ndiyo, wanafahamiana”
“Sasa walikuwa katika chumba cha nani?”
“Swali zuri. Walikuwa katika chumba cha yule aliyenyongwa. Ina maana kwamba aliyemnyonga mwenzake alidhamiria kumuua. Alimsubiri alewe sana kisha akamnyonga kirahisi.”
“Sasa hizi bilauri na hizi chupa ndizo walizokuwa wakitumia. Kuna alama zao za vidole. Alama ninazohitaji mimi ni za muuaji. Nataka tuzijue na tuwe nazo ili yeyote tutakayemshuku na kumkamata tunalinganisha alama zake za vidole. Tukiona ndio hizo tunamshitaki kwa mauaji.”
“Sasa ili kujua alama za nani ni za nani ni lazima tupate pia alama za vidole vya marehemu,”
“Tutakwenda hospitalini ukachukue alama zake.”
Nikatia mkono mfukoni na kutoa kile kikaratasi tulichokikuta kwenye kitanzi chenye sahihi na alama ya dole.
“Hiki kipande cha karatasi tulikikuta kwenye kitanzi alichofungwa marehemu. Kimeandikwa ‘Bado Watatu’ yaani baada ya marehemu kunyongwa bado watu wengine watatu ambao watanyongwa pia au watauawa kwa njia nyingine. Hiki kikaratasi kina sahihi na alama ya dole gumba. Jaribu kulinganisha alama hiyo na hizo utakazozipata kwenye hizi bilauri na chupa. Tunashuku huenda ni alama ya mtu aliyemnyonga mwenzake.”
“Sawa. Sasa ni muda gani tutakwenda huko hospitalini kuchukua alama za vidole za marehemu?”
“Mimi nadhani twende sasa hivi ili utakapoanza kutafuta hizo alama, vielelezo vyote uwe unavyo hapa.”
“Sawa, tunaweza kwenda.”
Dakika chache baadaye, mimi na Sajin Meja Ibrahim tukawa kwenye gari tukienda Hospitali ya Bombo. Tulipofika tulitoa ombi la kutaka kuchukua alama za vidole za mwili wa mtu aliyefikishwa na polisi asubuhi akiwa amenyongwa.
Tulipokubaliwa tuliongozwa na daktari hadi mochwari ambako mwili huo ulikuwa umehifadhiwa. Sajin Meja Ibrahim akafanya kazi yake iliyomchukua dakika tatu tu kisha tukaaga na kuondoka.
Mimi na Sajin Meja huyo tuliachana tuliporudi kituo kikuu cha polisi. Kwa vile nilikuwa na gari la idara ya upelelezi nilikwenda katika hoteli moja iliyokuwa maeneo ya forodhani nikaliegesha gari na kwenda kupata kinywaji.
Niliagiza soda ya CokaCola nikawa nakunywa taratibu. Kutokana na kutingwa na mawazo ya mchumba wangu niliyekuwa nimefarakana naye, niliona niyawache kwanza mawazo ya kazi nimuwaze Hamisa.
Nilikuwa nikijiuliza kama nilikuwa nipo tayari kukubali kuachana na Hamisa kwa sababu ya kunituhumu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Helena?
Jibu lililotoka akilini mwangu ni kuwa sikuwa tayari kuacha uchumba wangu na Hamisa uvunjike.
Nilikuwa bado nampenda Hamisa na mipango ya ndoa yetu ilikuwa imekaribia.
Nikatoa simu yangu kwenye mfuko wa koti langu na kumpigia.
Simu iliita mpaka ikakata yenyewe. Hamisa hakupokea simu. Nikampigia kwa mara ya pili. Nilijiambia labda hakuusikia mlio wa simu ya mara ya kwanza, pengine alikuwa mbali na simu.
Hii mara ya pili pia simu yangu haikupokewa. Iliita mpaka ikakata yenyewe.
Kama hapo mwanzo nilijipa tamaa kwamba Hamisa hakuusikia wito wa simu, mara hii ya pili sikutaka kujidanganya tena. Nikajiambia Hamisa hakupokea simu yangu kwa makusudi. Alikuwa ameshadhamiria kukata mawasiliano na mimi.
“Huyu msichana ana chuki ya namna gani. Hataki hata kuombwa radhi!” nikajiambia kimoyo moyo kwa hasira.
Sikumaliza soda niliyokuwa nakunywa nikampungia mkono mhudumu kumuita. Alipofika nilimlipa pesa ya soda hiyo kisha nikainuka.
“Huendelei kunywa tena?” Akaniuliza.
“Hapana,” nikamjibu nikiwa nimeshampa kichogo.
Nilikuwa ninatoka na kuelekea nilipoliacha gari. Nilijipakia kwennye gari hilo nikaliwasha na kuondoka.
Hamisa alikuwa akiishi Sahare. Nilikuwa nimeamua kumfuata nyumbani kwake ili nikazungumze naye. Ingawa hakuwa muuguzi aliyeajiriwa katika hospitali ya serikali nilijua muda ule ningemkuta nyumbani kwani kwa wiki ile alikuwa akiingia kazini saa nane mchana.
Niliitazama saa yangu ambayo iliniambia ilikuwa saa sita na nusu. Mpaka nafika Sahare ilikuwa saa saba kamili.
Wakati naliegesha gari mbele ya nyumba aliyokuwa anaishi Hamisa, niliona mlango wa mbele wa nyumba hiyo ukifunguliwa kisha Hamisa akatoa kichwa na kunichungulia. Alipoona ni mimi niliyesimamisha gari alirudisha kichwa haraka na kufunga mlango.
Nilishuka kwenye gari nikapiga hatua kuelekea kwenye mlango. Nilibisha sambamba na kuufungua mlango huo. Nilijua Hamisa anaweza hata kuninyamazia kimya, bora tu niingie ndani.
Niliingia nikatokea kwenye sebule ndogo lakini iliyopambwa vizuri. Nikajikaribisha mwenyewe kwenye sofa. Hamisa hakuwepo. Nilihisi kwamba alikuwa chumbani.
Wakati nimekaa nikitazama picha zilizokuwa zimepachikwa kwenye kuta kama vile nilikuwa naziona kwa mara ya kwanza siku ile wakati siku zote zilikuwepo, Hamisa akatoka chumbanni akiwa amevaa sare yake ya kazi ya rangi nyeupe pamoja na kitu kama kikofia alichokipachika kichwani.
Pia alikuwa amebeba sweta lake la baridi pamoja na mkoba wake aliokuwa ameupachika begani.
“Habari ya saa hizi?” akanisalimia wakati ananipita akielekea kwenye mlango wa mbele. Alinisalimia bila hata kugeuza uso kunitazama.
“Nzuri,” nikamjibu na kuongeza.
“Nimekupigia simu mara mbili. Hukuona ‘missed calls’ zangu?”
Hamisa alikuwa ameshafika kwenye mlango. Akageuka na kunitazama. Nilikuwa kama niliyempandisha hasira.
“Ulikuwa unataka niini?” akaniuliza kwa sauti ambayo haikuwa tulivu.
“Kwanini unaniuliza hivyo wakati unajua tuko kwenye uhusiano”
“Sikiliza Fadhil mimi nataka kutoka kwenda kazini. Kama huna chochote cha kuniambia nenda zako!”
“Siamini kama ni wewe Hamisa uliyebadilika hivyo!”
“Huamini nini? Kama mimi nimebadilika Helena si yupo?”
Helena ndiye huyo msichana aliyekuwa akinishuku naye.
“Sikiliza Hamisa. Acha kuunda mambo kwa kutumia hisia. Helena si mpanzi wangu. Helena ni mtumishi mwenzangu.”
“Kwenda zako. Tafadhali Fadhil ondoka uende zako. Mimi nataka kufunga mlango wangu.”
Hamisa akatazama saa yake ya mkononi kisha akaongeza.
Nikapiga hatua kuelekea kwenye mlango, mahali ambapo alikuwa amesimama. Kama vile hakutaka nimsogelee karibu, alitoka nje na kusimama kando ya mlango.
“Mbona unatoka?” nikamuuliza.
“Nataka kwenda zangu kazini” akaniambia.
“Hamisa nina mazungumzo na wewe. Niambie nikufute saa ngapi kazini kwako.”
Toka… toka… tokaaa!” akaniambia huku akinisisitizia kwa mkono wake kuwa nitoke. Nikatoka.
“Usithubutu kunifuata kazini kwangu. Unanifuata kazini kwa mpango gani?” akaniuliza huku akifunga mlango wake. Inaendelea...