Shilingi yapanda, wanaonufaika ni hawa

Dar es Salaam. Watanzania wanaopanga kuagiza magari, vipuri, ngano, mafuta ya kula na bidhaa nyingine kutoka nje ya nchi wanatarajiwa kunufaika na kupanda kwa thamani ya shilingi, hali itakayopunguza gharama za uagizaji wa bidhaa mbalimbali.

Sarafu ya ndani imepata nguvu kubwa dhidi ya Dola ya Marekani katika miezi ya hivi karibuni.

Aprili 2025, ilibadilishwa kwa wastani wa Sh2,668.90 kwa Dola 1 ya Marekani, lakini kufikia Jumatatu, Agosti 25, 2025, ilikuwa imeimarika hadi kiwango cha Sh2,454.74.

Kuimarika huko kumeleta faida halisi kwa watumiaji na wafanyabiashara. Miongoni mwa manufaa ya haraka zaidi ni kushuka kwa bei ya mafuta. Mapema mwezi huu, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ilitangaza punguzo la Sh34 kwa petroli na Sh10 kwa dizeli, hasa kutokana na kuimarika kwa shilingi.

“Kwa mwezi huu pekee shilingi imepanda thamani kwa wastani wa Sh52 ikilinganishwa na Julai. Hii imechangia kushuka kwa bei ya mafuta, ambayo petroli imeshuka kwa Dola 18 kwa tani ya ujazo na dizeli kwa Dola 3 (za Marekani) kwa tani ya ujazo,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wauzaji wa Mafuta (Taomac), Raphael Mgaya mapema mwezi huu.

Mgaya amesema hakuna mabadiliko makubwa yanayotarajiwa katika siku za usoni na gharama za mafuta huenda zikabaki imara au zikashuka kidogo.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imehusisha uimara wa sarafu hiyo na ufanisi wa mauzo ya nje, hususan mazao ya kiasili kama korosho, mauzo mazuri ya dhahabu na kuendelea kuimarika kwa sekta ya utalii.

Mapema mwezi huu Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa BoT, Dk Suleiman Misango, alisema bei za mafuta duniani pia zimeendelea kuwa nafuu, huku benki hiyo ikiendelea kuimarisha akiba ya fedha za kigeni.

Akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola 5.972 bilioni za Marekani mwishoni mwa Juni 2025, ikilinganishwa na Dola 5.346 bilioni za Marekani katika kipindi kama hicho mwaka 2024.

Akiba hiyo, ambayo ipo juu ya viwango vya kitaifa na vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), inatosha kufidia miezi 4.8 ya uagizaji wa bidhaa na huduma.

Aidha, faida za kuimarika kwa shilingi tayari zinaonekana katika soko la uagizaji.

Katika uagizaji wa magari kwa matumizi ya nyumbani, ulifikia Dola 436.4 milioni za Marekani mwaka ulioishia Juni 2025, ikilinganishwa na Dola 322.6 za Marekani milioni mwaka uliopita.

Uagizaji wa ngano ulipungua hadi Dola 345 milioni za Marekani kutoka Dola 393 milioni za Marekani, wakati mafuta ya kula yalifikia Dola 160 milioni za Marekani. Uagizaji wa mbolea pia uliongezeka hadi Dola 374.4 milioni za Marekani kutoka Dola 328.6 milioni za Marekani.

Wachumi wanasema kuimarika kwa thamani ya shilingi kunatoa nafuu kwa kaya na wafanyabiashara wa Kitanzania katika kipindi ambacho hali ya uchumi wa dunia imetikisa nchi nyingi zinazoendelea.

Wanaeleza kuwa, kupungua kwa gharama za uagizaji kunatoa nafasi kwa biashara kupanuka, watu binafsi kuwekeza kwenye magari au mitambo na wajasiriamali wadogo kuingia kwenye fursa mpya kama vile uokaji mikate au biashara ya jumla ya bidhaa muhimu.

Hata hivyo, baadhi ya sekta zinasema bado hazijaanza kuhisi manufaa ya moja kwa moja. Mwenyekiti wa Chama cha Waokaji Tanzania (TBA), Fransica Lyimo, ameiambia The Citizen kuwa mwenendo huo bado haujaleta nafuu kwa waokaji, kwani malighafi nyingi ziliagizwa wakati dola ikiwa juu.

“Idadi kubwa ya watu walinunua unga wa ngano kwa bei ghali, hivyo faida bado haijaonekana mara moja. Lakini endapo shilingi itaendelea kuwa imara kwa angalau miezi miwili, tunatarajia mabadiliko yatatiririka kwenye sekta yetu,” amesema.

Amesema gharama bidhaa nyingine pia bado ni changamoto. “Sekta ya uokaji pia inaathiriwa na bei za mafuta ya kula, sukari na umeme. Iwapo vyote vitadhibitiwa, basi bidhaa kama mkate zitashuka bei. Kwa sasa, ni wafanyabiashara wa jumla pekee wanaonufaika kwa kupata faida ya angalau Sh50 kwa kila mkate, huku waokaji wadogo wakihangaika,”amesema  Lyimo.

 “Kwa mfano, wakati wa msimu wa mihogo, matumizi ya mikate hupungua sana, na kuwaacha waokaji na mikate isiyouzwa.”

Kwa upande wake, mhadhiri mwandamizi wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Lutengano Mwinuka amesema shilingi imara huboresha moja kwa moja uwezo wa ununuzi wa Watanzania, hasa kwa bidhaa zinazotegemea uagizaji kwa kiwango kikubwa.

“Kuna fursa kubwa katika bidhaa kama mbolea na mafuta ya kula, pamoja na bidhaa zinazowekwa kwa wingi kama dizeli na petroli. Sarafu imara hubadilika kuwa akiba ya kifedha na kupunguza gharama kwa walaji. Huu ni wakati muafaka wa kuchunguza mifumo ya ununuzi wa pamoja wa bidhaa hizo,” amefafanua.

Hata hivyo, wachambuzi wanatahadharisha kuwa, ingawa kupanda kwa thamani ya shilingi kumekuwa na manufaa, kunahitaji usimamizi makini ili kuhakikisha ushindani wa mauzo ya nje hauathiriki.

Hivi sasa, kuimarika kwa shilingi kunatajwa kama faida kubwa kwa walaji, wafanyabiashara na uchumi mpana kwa jumla.