KIUNGO mshambuliaji wa Namungo, Pius Buswita amesema ujio wa Heritier Makambo katika timu hiyo unaongeza nguvu ya ushindani na namba, idadi ya mabao katika michuano yote ya msimu ujao.
Buswita katika misimu miwili Namungo, alifunga jumla ya mabao 10, 2023-2024 mabao saba na msimu uliopita alifunga matatu na asisti mbili, alisema kwa kiwango na kipaji alichonacho Makambo safu ya ushambuliaji ya timu hiyo anaamini msimu ujao itakuwa na mabao mengi.
“Nilicheza na Makambo msimu wa 2018-2019 na alifunga mabao 17 kisha akaondoka kwenda kujiunga na Horoya AC, msimu uliyopita akiwa na Tabora United alimaliza na mabao sita na asisti nne na aliumia hakucheza mechi nyingi, hilo linanipa imani ataongeza idadi ya mabao mengi katika timu,” alisema Buswita na kuongeza;
“Makambo ni mchezaji mwenye bidii ya mazoezi na mhamasishaji wa wengine kujituma, kwani nililiona hilo tukiwa Yanga hata kama anakuona pengine haupo mchezoni atakufuata na kukujenga kuhakikisha unarejea katika morali yako.”
Pia alisema anafurahia kuona uwepo wa wachezaji wengine wapya katika kikosi chao kama beki Hussein Kazi aliyetokea Simba akiamini kiwa kipaji chake ataongeza nguvu katika eneo la ulinzi.