Bado Watatu – 6 | Mwanaspoti

“NIKAITAZAMA namba yake na kuiandika kwenye notibuku yangu kisha nikaingia upande wa meseji zilizotoka ambazo aliziandika marehemu mwenyewe.
Huko nilikuta meseji kadhaa lakini nilizozitilia maanani zilikuwa meseji mbili ambazo aliziandika katika tarehe ya jana yake.
Moja iliuliza.
“Nyumbani wapi?”
Ya pili ikauliza.
Utakuja saa ngapi?”
Nikahisi kwamba meseji hizo zilikuwa majibu ya zile meseji zilizotumwa ambazo moja zilisema; “Itabidi nije nyumbani kwako tuzungumze tupate na bia mbili tatu.”
Na ya pili iliyosema. “Nyumbani kwako.”
Na ya tatu iliyosema. “Kwenye saa tatu hivi.”
Bila shaka mtuma meseji alipomwambia marehemu kuwa itabidi aje nyumbani kwake wazungumze na kupata bia mbili tatu, marehemu alimuuliza. “Nyumbani wapi?”
Mtuma meseji akamjibu. “Nyumbanni kwako”
Marehemu akamuuliza. “Utakuja saa ngapi?”
Mtuma meseji akamjibu. “Nitafika kwenye saa tatu hivi”
Hapo nikawa nimeupata vizuri mfuatano wa meseji hizo. Sasa nikaitafuta ile namba kwenye orodha ya majina yaliyosajiliwa. Nikaikuta ikiwa na jina la Thomas Christopher.
Nikajiambia. “Sasa nimeshampata muuaji, ni Thomas Christopher!”
Ilikuwa ni kiasi cha kwenda kwenye kampuni ya simu inayomiliki mtandao anaoutumia mtuhumiwa na kuomba nipatiwe picha yake na anuani yake.
Nikishapata picha yake na anuani yake itakuwa ni rahisi kumkamata. Ni kiasi tu cha kufika nyumbani kwake na kumuulizia. Atakapojitokeza tu ninamtia mikononi!
Hivi ndivyo tulivyowakamata watuhumiwa wengi kwa kutumia njia za mitandao.
Nikajiambia hii kazi ambayo niliiona ngumu, sasa ningeweza kuimaliza kwa saa kadhaa.
Kwanza nikafanya kama nataka kutuma pesa kwenye ile namba kwa kutumia simu yangu. Likajitokeza jina lile lile la Thomas Christopher.
Nikaona lile jina lilikuwa sahihi na mtuhumiwa tungeweza kumkamata mara moja.
Nikajaribu kuipiga ile namba, ikawa haipatikani.
“Si kitu” nikajiambia kimoyo moyo na kuendelea kujiambia.
Hata kama atakuwa ametoa laini, bado tunao uwezo wa kumpata.
Nikahisi kwamba niilikuwa nimefanya ugunduzi mkubwa kwa kutumia muda mchache tu. Sikukaa tena ofisini. Niliihifadhi ile simu kisha nikatoka na kurudi ofisini kwa Sajini Meja Ibrahim.
Sajini Meja Ibrahim alipoona nimerudi tena alishituka kidogo.
“Afande kuna tatizo?’ akaniuliza.
“Si tatizo…,” nikamwambia kisha nikaketi na kuongeza:
“Nimekuja kukufahamisha kwamba nimegundua jina la mtuhumiwa wetu.”
“Anaitwa nani?”
“Anaitwa Thomas Christopher.”
“Umelipataje hilo jina?”
“Nimelipata kutoka katika simu ya marehemu. Nimeona jinsi walivyowasiliana kwa meseji jana usiku.”
“Sasa kama umegundua jina itanirahisishia uchunguzi wangu. Kama ana rekodi hapa polisi tutampata mara moja.”
Sajin Meja Ibrahim alichukua kalamu akaandika lile jina kwenye karatasi.
“Hili jina nitabaki nalo.”
“Sasa nataka niende kwenye kampuni ya simu nikaone usajili wake”
“Utakwenda leo?”
“Jua limekuchwa sana. Nitakwenda kesho asubuhi.”
“Huo usajili ndio utakaokuongoza kumpata.”
“Kwa sababu kuna picha yake na anuani yake.”
“Na kwa upande wangu kama nitamgundua, tutamkamata kirahisi sana.”
“Sawa. Acha niende nikampumzike.”
Nikainuka kwenye kiti.
“Sawa afande, tutaonana kesho.”
Nikatoka ofisini humo.
Karibu maafisa wote wa polisi tunafanya kazi hadi saa nane. Unaweza kuendelea na kazi kama utakuwa umepangiwa zamu au kumetokea dharura ya kikazi.
Kwa vile nilikuwa nimeshakamilisha kazi yangu nikaona niondoke nirudi nyumbani.
Nyumba yangu ilikuwa katika eneo la Nguvumali. Nilipofika nyumbani nilioga nikabadili nguo na kutoka tena. Nilikwenda katika eneo la jirani ambako kulikuwa na hoteli ambayo mara nyingi hula chakula ninapokuwa maeneo ya nyumbani.
Baada ya kula na kushiba vizuri nikarudi nyumbani. Niliketi sebuleni nikafungua sabufa na kuweka miziki ya kizazi kipya.
Nilihitaji muda wa kutosha wa kutafakari kuhusu hatima yangu na Hamisa. Nilijiambia kama sitatumia busara kumtuliza Hamisa huenda nikashindwa kufanya kazi zangu.
Kabla ya Hamisa, nilishawahi kupenda wasichana wengi lakini kwa Hamisa ilikuwa ni zaidi ya kupenda. Pale nilikuwa nimefika. Ndiyo sababu wazo la kumuacha au kuniacha yeye, lilikuwa likikereketa moyo wangu.
Nilikuwa tayari nimeshatoa simu yangu ili nimpigie bila kujali kwamba alikuwa kazini lakini nikajiambia ni vyema nimpe muda zaidi wa kutafakari, pengine hasira zake zitaisha na tunaweza kurudisha uhusiano wetu.
Nilipoafikiana na wazo hilo nikairudisha simu kwenye stuli iliyokuwa kando yangu.
Niliamini kuwa mapenzi yalikuwa na nguvu kubwa ya kuweza kumiliki moyo wa mtu na kumfanya ashindwe hata kuwaza mengine.
Nikatikisa kichwa changu kisha nikajiambia hakuna lenye mwanzo likakosa kuwa na mwisho. Mwisho wa dhiki hii ninayoipata utafika tu.
Asubuhi ya siku iliyofuata nilikwenda kazini kwangu. Kisha nikachukua gari na kuelekea kwenye ofisi za kampuni ya simu ambayo mtandao wake ndio aliokuwa akiutumia Thomas Christopher.
Nilipofika nilipata ushirikiano wa kutosha nikaweza kutolewa picha ya mtu huyo pamoja na maelezo machahe yaliyokuwa katika usajili wa laini yale.
Laini hiyo ilisajiliwa mwaka mmoja na nusu uliopita. Ilisajiliwa mjini hapo hapo kwa kutumia barua ya mwenyekiti wa mtaa. Mwenye laini hiyo alikuwa mkazi wa eneo la Chuda nyumba namba 313.
Nilipoitazama picha niliyotolewa na afisa wa kampuni ya simu niligundua ilikuwa picha ya kijana ambaye nilishindwa kumfikiria kwamba angeweza kuwa na moyo wa kuua mtu.
Lakini kutokana na uzoevu nilioupata katika  kazi yangu niligundua kuwa mara nyingi wauaji waliokubuhu wana sura tofauti na vitendo vyao. Wengi wao ambao nilikutana nao wana sura nzuri na ni vijana.
Si wauaji wanaohitaji kukunja uso pale wanapompiga mtu risasi au kumnyonga. Wanaweza kuua mtu huku wanatabasamu. Kwao tendo hilo la mauaji ni la furaha.
Nilimshukuru afisa wa kampuni ya simu aliyenipa ushirikiano kisha nikatoka. Kwa vile nilishautambua mtaa aliokuwa anaishi mtu niliyekuwa nikimtuhumu kuua pamoja na namba ya nyumba anayoishi, nilijiambia sasa kazi iliyobaki ni ya kwenda kumkamata.
Nilikwenda kwenye kituo cha polisi nikachukua polisi wanne wenye bunduki nikawapakia kwenye gari na kwenda nao Chuda eneo ambalo lilikuwa katikati ya jiji.
Niliutafuta mtaa huo niliokuwa nikiutaka nikauona. Sasa nikapunguza mwendo ili niipate nyumba namba 313.
Kilichonipa moyo ni kwamba mara tu tulipoingia katika mtaa huo, nyumba ya kwanza kuiona ilikuwa namba 320. Nikaendelea kwenda mbele. Namba hizo zilikuwa zinarudi nyuma. Niligundua kuwa mtaa huo niliutokea kwa nyuma.
Nikaendelea kwenda hadi nikaiona nyumba namba 313. Nilikuwa karibu kupiga vigelegele kimoyomoyo baada ya kuiona namba hiyo iliyokuwa imeandikwa kwenye geti. Katika maisha chezea raia wenzako, lakini usichezee polisi. Wanao uwezo wa kukupata mahali popote ulipo!
Lakini pamoja na furaha yangu kuona upelelezi wangu umekuwa na mafanikio, nilishituka kuona nyumba yenyewe si tu ilikuwa ya ghorofa bali pia ilikuwa ya kifahari. Kwa vyovyote vile haikuwa nyumba ambayo anaweza kuishi mtu  mwenye kazi ya kuua watu!
Hilo lilinipa shaka sana.
Nilimwambia polisi niliyekuwa nimeketi naye katika siti ya mbele.
“Nyumba yenyewe ndio hii hapa.”
Polisi huyo naye alishangaa akadhani labda nilimuonyesha nyumba iliyofuatia, akaniuliza.
“Ipi, ile pale?” alionyesha nyumba ya pili baada ya ile ambayo ilikuwa nyumba ya kawaida.
“Hapana. Ni hii hapa.”
Nikamuonyesha ile nyumba ya ghorofa.
“Una maana…una maana….?”
“Najua umeshangaa kuiona nyumba yenyewe lakini ndiyo hiyo nyumba namba 313. Tazama kwenye geti.”
Polisi huyo akatazama kwenye geti na kuisoma namba 313.
“Kweli ndiyo hiyo. Nilikuwa nauliza una maana huyo mtu atakuwa anaishi katika nyumba hii?”
“Hebu twende.”
Nikafungua mlango na kushuka. Polisi niliyekuwa nimekaa naye akashuka.
Mimi na polisi huyo ndio tuliokwenda kubisha geti.
Baada ya kubisha kwa sekunde kadhaa mwanamke mmoja akaja kutufungulia. Alikuwa msichana mrembo ambaye sikuhisi kama alikuwa hausigeli.
Kutokana na wigi la thamani alilokuwa amevaa pamoja na ngozi yake ya mwili ambayo ilionekana kunawiri kutokana na kupakwa losheni za bei ya juu, nilihisi allikuwa ndiye mama mwenye nyumba.
Alipotuona na nilidhani alipomuona mwenzangu aliyekuwa amevaa mavazi ya kipolisi, aligutuka. Macho yake yaliingia hamaki ya hofu akawa anatutazama kwa zamu.
“Karibuni.” akatuambia.
“Habari yako?” nikamsalimia.
“Nzuri. Naweza kuwasaidia”
“Wewe ni mkazi wa nyumba hii?” nikamuuliza.
“Ndiyo mimi ni mkazi wa nyumba hii”
“Sawa.  Tulikuwa tunamuulizia Thomas Christopher”
Nilitamka Thomas Christopher kama vile nilikuwa namhamu.
“Thomas Christopher?” Msichana akauliza huku akiwa amekunja uso akionyesha kuvuta kumbukumbu.
“Ndiyo Thomas Christopher”
Msichana akatikisa kichwa.
“Simfahamu. Humu ndani ninaishi mimi na mume wangu ambaye haitwi jina hilo.” Inaendelea...