Dar es Salaam. Mshtakiwa, Fred Chaula (56) na wenzake wawili, wanaokabiliwa na kesi ya mauaji watalazimika kuendelea kusalia rumande hadi Septemba 8, 2025. Hiyo, inatokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mbali na Fredy, washtakiwa wengine ni Bashir Chaula (49) dereva bodaboda na mkazi wa Tegeta pamoja na Denis Mhwaga, mkazi wa Iringa.
Washtakiwa hao kwa pamoja, wanadaiwa kumuua mwanafamilia aitwaye, Regina Chaula (62) na kisha mwili wake kuutupa kwenye shimo la maji machafu lililopo katika nyumba ya Regina, wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Leo, Jumatatu Agosti 25, 2025, wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru ameieleza Mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea.
Wakili Mafuru ametoa taarifa hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa kutajwa.
Hata hivyo, Julai 29, 2025 kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa, upande wa mashtaka uliieleza Mahakama hiyo kuwa upelelezi upo katika hatua za mwisho kukamilika.
Lakini leo, upande wa mashtaka umedai kuwa bado wanaendelea na upelelezi, hivyo wanaomba Mahakama iwapangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
“Mheshimiwa hakimu, upelelezi wa kesi hii ya mauaji bado unaendelea, hivyo upande wa mashtaka tunaomba Mahakama yako itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo upelelezi wa kesi hii umekamilika au laa,” alidai wakili Mafuru.
Mafuru baada ya kueleza hayo, wakili wa utetezi, Kung’e Wabeya aliomba upande wa mashtaka wakamilishe upelelezi kwa wakati ili kesi hiyo iweze kuendelea na hatua nyingine.
Hakimu Mushi baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 8, 2025 kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, washtakiwa hawakuletwa mahakamani hapo na badala yake imesikilizwa kwa njia ya mtandao.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Machi 12, 2025 na kusomewa kesi ya mauaji.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo, Januari 18, 2025 eneo la Bahari Beach, Wilaya ya Kinondoni.
Inadaiwa siku ya tukio, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kumuua Regina Chaula, ambaye ni mwanafamilia mwenzao, na kisha mwili wake kuutupa kwenye shimo la maji machafu lililopo katika nyumba ya marehemu (Regina), wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.