Dar kinara wanafunzi wanaohama shule za msingi nchini

Dar es Salaam. Mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Tabora na Geita imetajwa kuwa kinara nchini kwa wazazi kuhamisha watoto wao wanaosoma shule za msingi kwenda maeneo mengine nchini.

Jambo hilo linatajwa kuchangiwa na kuhama kwa wazazi wao kikazi, kutafuta sehemu ambazo watoto wanaweza kupata elimu bora na usalama wa wanafunzi.

Ripoti ya Best Education ya mwaka 2025 inautaja mkoa wa Dar es Salaam kuwa kinara kwa kushuhudia uhamisho mkubwa wa wanafunzi wa shule ya msingi kutoka mkoa huo kwenda maeneo mengine.

Ripoti hiyo iliyochapishwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inaonesha kati ya Aprili hadi Desemba mwaka jana, wanafunzi 22,531 wa shule za msingi walihamishwa kutoka Dar es Salaam na kupelekwa shule nyingine.

Dar es Salaam ilifuatiwa na Mwanza iliyoshuhudia uhamisho wa wanafunzi 19,452, Tabora ikiwa namba tatu, wanafunzi 11,317 walihamishwa, Geita wanaunzi 11,158 na Morogoro wanafunzi 9,695.

Kwa jumla wanafunzi 183,901 wa shule za msingi walihamishwa kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine katika mwaka 2024 huku wanafunzi 193,831 wakihamia.

“Kwa jinsi Dar es Salaam ilivyo kwa mtoto ambaye hawezi kuhimili mikiki mikiki,  siyo sehemu inayoweza kumpa utulivu wa akili hasa kama hauna uwezo wa kumpeleka mtoto shule nzuri ambayo atakuwa na uhakika wa usafiri kwenda na kurudi shuleni,” amesema Mercia Samson, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam.

Amesema mara nyingi mzazi anapoamua kumhamisha mtoto shule hutafuta kitu bora kwa ajili yake na wakati mwingine huweza kufikia uamuzi huo hata kama yeye atabaki katika mkoa husika.

“Wakati mwingine unaangalia mtoto anaondoka saa 11 alfajiri na kurudi saa 2 usiku kwa sababu ya foleni kama shule iko mbali au usafiri unasumbua, ukigeuka nyuma unaona kwa bibi yake kuna shule ambayo iko mita 100 kutoka nyumbani na wanafundisha vizuri, unaamua kumpeleka kwa sababu unamuepusha na mambo mengi,” amesema.

Alichokisema Mercia ni tofauti na Lazaro Msangi ambaye anabainisha kuwa shughuli za wazazi ni jambo linalochangia kwa kiwango kikubwa Watoto kuhamishwa shule.

“Kwa umri ambao mtoto wa shule ya msingi anakuwa nao mara nyingi wazazi wanapohama huhama nao tofauti na wale wa sekondari. Kwa jiji kama la Dar es Salaam sasa hivi bado watu wanahamia Dodoma na maeneo mengine wakipata fursa hivyo ni rahisi, pia jiji hili lina watu wengi ndiyo maana idadi inaonekana kuwa kubwa,” amesema.

Hata hivyo, Dar es Salaam mbali na kuongoza kutoa wanafunzi wengi wanaohama, jiji hilo pia ndiyo linalopokea wanafunzi wengi wanaohamia.

Katika kipindi husika, wanafunzi 20,622 waliliripotiwa kuhamia kutoka mikoa mbalimbali huku Mwanza nayo ikisalia nafasi ya pili kwa kupokea wanafunzi 17,317, Geita 13,199, Mara (12,284), Pwani (11,471).

Akizungumza na Mwananchi, Mdau wa Elimu, Dk Luka Mkonongwa amesema upo uwezekano wa hali hii kuchangiwa kwa asilimia kubwa na wazazi wengi kuhama eneo moja kwenda lingine huku akitolea mfano wa namna serikali inavyohamia Dodoma.

“Mzazi akihama eneo moja kwenda lingine ni rahisi kuondoka na mtoto wake wa shule ya msingi, wanaofuata ubora wa elimu ni wachache kwani shule ya msingi watoto wengi bado wako chini ya uangalizi wa wazazi na wengi hawako tayari kukaa nao mbali,” amesema.

Amesema ikiwa wachache wanaohama kwa kufuata ubora wa elimu asilimia kubwa ni wale wanaopelekwa shule za bweni tofauti na zile walizokuwa wakisoma awali ili kuondokana na tabu ambayo mzazi aliibaini.

“Na ninasema wanaofuata ubora wa elimu si wengi kwa sababu kila mkoa sasa una shule nyingi tena zinazofanya vizuri kuliko zile zilizopo mkoani Dar es Salaam, labda tungeangalia wanaohama kutoka shule za Serikali kwenda za binafsi huko tungewapata wengi kwa sababu wanataka kujenga msingi imara wa Watoto kabla hawajafika ngazi za juu,” amesema.

Shule za binafsi nyingi zinakuwa na walimu wa kutosha, vitabu na hata idadi yao kwa darasa inawekwa kulingana na kiwango cha Serikali huku lugha ya Kiingereza inayotumika ikitajwa kuwa moja ya kinachowavuta wazazi ili kuhakikisha Watoto wanakuwa na msingi mzuri.

Takwimu Msingi za Tanzania 2024 zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeonesha pia kuwapo kwa ongezeko la wanafunzi wanaondikishwa katika shule za msingi za binafsi kila mwaka kati ya 2020 hadi 2024.

Idadi ya wanafunzi wanaosoma katika shule hizo iliongezeka kutoka 465,111 mwaka 2020, ikafikia 509,195 mwaka 2021, wanafunzi 548,465 walikuwapo katika shule hizo mwaka 2022, kabla ya kufikia 601,108 mwaka 2023 na hatimaye 651,210 mwaka 2024.