Wafugaji 34,484 kunufaika na chanjo ya mifugo Handeni

Handeni. Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Salum Nyamwese amewataka wafugaji wilayani humo kujitokeza kuchanja mifugo ili kudhibiti magonjwa ya kideri, sotoka na homa ya mapafu ambayo ndio yanayosumbua zaidi mifugo.

‎Akizungumza wakati wa mwendelezo wa kuzindua kampeni ya chanzo ya mifugo kwenye kata mbalimbali za wilaya hiyo leo Jumatatu Agosti 25, 2025 amesema wafugaji wanatakiwa kujitokeza kushiriki shughuli hiyo ya kitaifa, ili kupunguza magonjwa  ya mifugo.

Amesema katika Wilaya ya Handeni yapo magonjwa matatu ikiwamo homa ya mapafu inayowasumbua zaidi ng’ombe.

Mkuu wa wilaya ya Handeni Salum Nyamwese(kushoto) akikagua baadhi ya mifugo ambayo inatarajiwa kutambuliwa kwa kuwekwa alama na kuchanjwa.Picha  na Rajabu Athumani



Lakini kwa upande wa mbuzi na kondoo amesema wao husumbuliwa na ugonjwa wa sotoka ambao unaathiri mwili wake, ikiwemo mfumo wa upumuaji na hupata vidonda na baadaye kukosa hamu ya kula na kusababisha wakose afya au kufa.

Kadhalika kwa upande wa kuku wao husumbuliwa na ugonjwa wa kideri ambacho ni hatari kinaweza kuwaua  wengi kwa mara moja, jambo linalosababisha hasara kwa wafugaji.

 “Niwaombe mhamasishane wafugaji wote mjitokeze kuchanja na tunatarajia kuchanja mifugo 148,172 kwa mjini pekee,” amesema Nyamwese.

‎Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri hiyo, Aldegunda Matunda, amesema kati ya idadi hiyo ya mifugo; ng’ombe ni 38,006, mbuzi 25,356, kondoo 9,567 na kuku 75,243 ambapo mfugaji atalipia nusu ya gharama.

‎Amesema Halmashauri hiyo inakadiriwa kuwa na wafugaji wapatao 34,484.

Sekta ya mifugo imekuwa ikichangia asilimia 21.78 ya mapato ya halmashauri kwa mwaka, sambamba na kuinua kipato cha wananchi na ndio maana wanatoa huduma hiyo.

‎Amesema wamepokea mgao wa chanjo za ruzuku kutoka Serikali Kuu pamoja na vitendea kazi kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mifugo na wamejipanga kutoa elimu kwa wataalamu walioko kwenye kata mbalimbali ili kusimamia hatua hiyo ipasavyo.

Daktari wa Mifugo halmashauri ya Mji Handeni, ‎Michael Lingofu amezitaja chanjo zitakazotolewa ni ya homa ya mapafu kwa ng’ombe (cbpp), homa ya sotoka kwa mbuzi na kondoo (ppr), na kideri kwa kuku, katika kata zote 12 za halmashauri hiyo.

Baadhi ya wafugaji wa kata ya Malezi halmashauri ya Mji Handeni mkoani Tanga wakishiriki zoezi la kuwekwa alama ya utambuzi mifugo yao,pamoja na kupata chanjo.Picha na Rajabu Athumani



Mmoja wa wafugaji Lazaro Wangese ameiomba Serikali kuweka msisitizo kwa wafugaji wote kuchanja, kwani bila kufanya hivyo zoezi hilo linaweza lisiwe na faida kwao kwa maambukizi kuendelea kubakia.

Ameshauri uwekwe utaratibu wa kuwabana wafugaji wote mifugo yao ichanjwe, lengo likiwa ni kudhibiti kabisa magonjwa hayo kwa ukanda wao.

Rais Samia Suluhu Hassan alizindua kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo Juni mwaka huu, wilayani Bariadi mkoani Simiyu, ambapo itatekelezwa kila mwaka hadi mwaka 2029, na itagharimu Sh216 bilioni hadi kukamilika.