ANNA KILANGO ACHUKUA FOMU YA UBUNGE AKITANGAZA KUVUNJWA MAKUNDI NDANI YA CCM.

NA WILLIUM PAUL, SAME. 

MBUNGE mteule wa Chama cha Mapinduzi katika Jimbo la Same mashariki wilayani Same mkoani Kilimanjaro, Anna Kilango Malecel amechukua fomu ya kugombea katika Jimbo hilo huku akitangaza kuvunja makundi ndani ya CCM. 
Anna Kilango alichukua fomu hiyo jana katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Same mashariki katika ofisi za halmashauri ya Same ambapo alisindikizwa na viongozi wa Chama wilaya pamoja na wanachama na wananchi wa same mashariki. 
Alisema kuwa, kwa sasa utaratibu ndani ya Chama umeshakamilika ambapo ameteuliwa kupeperusha bendera ya CCM na kuwataka wana CCM wote kuvunja makundi na kuwa na kundi moja la CCM kuhakikisha wagombea Udiwani, Mbunge na Rais wanashinda kwa kishindo. 
“Ninatambua wapo wanachama katika kipindi cha kura za maoni walikuwa hawaniungi mkono na ilikuwa ni haki yao kabisa maana wagombea wote tulikuwa wana CCM sasa jina limerudi moja la kwangu nawaombeni tuvunjeni makundi kuanzia sasa na tupambane kuhakikisha wagombea wa Chama chetu wanashinda kwa kishindo” Alisema Anna Kilango.