Same. Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linawashikilia watu 12 kwa tuhuma za kumjeruhi na kumpora Sh20 milioni, mwenyekiti mstaafu wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Yusto Mapande.
Tukio la kujeruhiwa kwa mwenyekiti huyo lilitokea Agosti 21, 2025 wakati akingia nyumbani kwake baada ya kutoka kwenye shughuli zake za biashara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao akisema wanashikiliwa kwa mahojiano.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linaendelea na uchunguzi wa tukio la kujeruhi lillotokea Agosti 21, 2025 saa tatu na nusu usiku huko maeneo ya Mjohoroni, Wilaya ya Same ambapo Yusto Mapande, mfanyabiashara na mwenyekiti wa Halmashauri ya Same aliyemaliza muda wake na aliyekuwa mtiania wa nafasi ya Ubunge wa Same Magharibi ndani ya Chama cha Mapinduzi.
“Alijeruhiwa kwa kukatwa na kitu chenye makali mkono wa kulia na wahalifu ambao walifanikiwa kukimbia,” amesema.
Kamanda Maigwa amesema baada ya tukio hilo kuripotiwa Polisi walianza upelelezi mara moja ambapo hadi sasa wamewakamata watuhumiwa 12 kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo.
“Uchunguzi utakapokamilika taratibu za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani,” amesema Kamanda Maigwa
Aidha, amesema majeruhi huyo alipatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani siku hiyohiyo.
Akielezea tukio hilo, Mapande amesema tukio hilo lilitokea wakati akiingia getini kwake akitoka kwenye biashara zake na ndipo alipovamiwa na kuanza kushambuliwa na watu ambao alidai walikuwa kwenye pikipiki na kumpora Sh20 milioni.
Amesema walipomaliza kumjeruhi walizunguka upande wa pili wa gari wakakagua na walifanikiwa kuondoka na Sh20 milioni ambazo zilikuwa ni fedha kwa ajili ya kwenda mnadani kesho yake.
“Baadaye nikasikia wakisema tayari, wakazunguka upande wa pili wakaangalia angalia kwenye gari na bahati mbaya kwenye gari kulikuwa na Sh20 milioni ambapo kesho yake tulikuwa tunaenda kwenye mnada,” amedai Mapande.