Nani amefeli hapa; mfumo wa elimu au mwanafunzi?

Arusha. Gazeti hili tarehe 20 Agosti mwaka huu lilikuwa na ripoti ya Tamisemi kuhusu elimumsingi (BEST 2025), iliyoonyesha kwamba kuna uhaba mkubwa wa walimu katika shule zetu. 

Ilikuwa ripoti ya kusikitisha, hasa ukizingatia kwamba mtoto wetu wa Kitanzania ana haki ya kupata elimu bora kama vile alivyo na haki ya kupata malezi bora.

Pia haki ya kutunzwa na wazazi au walezi, kutibiwa akiugua, kuwa na usalama wa maisha yake, kupewa mahitaji yake ya kila siku na kadhalika. Kwa sababu hiyo, elimu bora ni haki, wala si fadhila, kwa kila mtoto wa Taifa letu.

Ninawapa pongezi Tamisemi kwa kuthubutu kutoa ripoti hiyo ijapokuwa si nzuri kufuatana na nia ya Taifa letu kutoa elimu bora.

Naomba uthubutu huo uwe kichocheo cha kuendelea kuboresha elimu katika Taifa hili.

Hivi majuzi jirani yangu alikuwa anatafuta kijana wa kumsaidia shambani kwake na katika kuzungumza na watu wachache, baba mmoja alituambia kwamba mtoto wake wa kiume, umri miaka 15, alifeli darasa la saba hivi karibuni, na hivyo kijana huyo alikuwa tayari kupewa ajira ya kufanya kazi shambani. 

Kijana huyo akapata hiyo ajira, na katika kuangalia utendaji wake shambani, alionekana ni mchapa kazi, mbunifu na mwenye kujituma katika kazi zote alizopewa. 

Hili lilinifanya niongee tena na mzazi wake kujua ni kweli mtoto huyu alifeli darasa la saba au vipi. 

Baba alinihakikishia kwamba mtoto wake huyo alifeli darasa la saba, na mtoto mwenyewe akanisisitizia kwamba alifeli darasa na saba.

Jambo hili lilinipa tafakari nikajiuliza: hapa aliyefeli ni nani? Ni huyu mtoto au ni mfumo wetu wa elimu? 

Inakuwaje mtoto huyu mwenye vipaji vingi, mchapa kazi, mwenye mawazo ya maendeleo, mchangamfu na mdadisi, akafeli darasa la saba? Ni nani aliyefeli hapa, ni mtoto huyu au ni mfumo wetu wa elimu? 

Nakubaliana na mhariri wa gazeti la Mwananchi kwa maoni yake ya tarehe 21 Agosti mwaka huu, kwamba Serikali yetu ina wajibu wa kumaliza uhaba wa walimu shuleni. 

Naamini kwamba wizara zinazohusika zinatambua tatizo hili na wanajua vizuri kwamba dawa yake ni kuajiri walimu wa kutosha shuleni. Nina imani kwamba Serikali inajua vizuri jambo hili.

Unajiuliza: shida ni nini? Mbona walimu hawatoshi? Fikiria shule moja huko mkoani Mtwara ina mwalimu mmoja na wanafunzi 495! 

Takwimu zinaonyesha kwamba takriban asilimia 63 ya shule za msingi za Serikali nchini zina upungufu wa walimu, huku mwalimu mmoja akibeba mzigo wa kufundisha wastani wa wanafunzi 56 badala ya 45 waliopendekezwa. 

Ripoti ya Tamisemi inaonyesha kuwa kuna shule 17 nchini zina mwalimu mmoja anayefundisha wastani wa wanafunzi 200 au zaidi, huku shule 975 mwalimu mmoja akifundisha wanafunzi kuanzia 100.

Katika shule aliyosoma kijana aliyetajwa hapo juu, kulikuwa na wanafuzi 90 darasa la saba, wasichana 50 na wavulana 40. Katika mazingira haya, kijana wetu angetoboa?

Nafikiria mzigo mkubwa walionao walimu katika mazingira haya. Mishahara yao bado si ya kuridhisha, vifaa vya kufundishia ni vichache, maktaba hazipo, kisha kuna wanafunzi 90 darasani.

Mwalimu huyu anateseka.Itawezekanaje huyu mwalimu aamke asubuhi akiwa na ari kubwa ya kuwahi shuleni? 

Ni kitu gani kinamvutia aende shuleni? Ni jambo lipi litamfanya apende kazi ya ualimu?

Watoto ni wengi darasani hivyo mwalimu hana fursa ya kumshughulikia mwanafunzi mmoja mmoja. Vitabu ni vichache, na maktaba haipo.

Mchana huyu mwanafunzi hatakula, na bado ana safari ya kilomita mbili au tatu za kutembea kurudi nyumbani, iwe jua au mvua, joto au baridi, vumbi au matope. Ni jambo gani linampa huyu mwanafunzi motisha na ari ya kwenda shule? 

Ni miujiza ilioje kwamba wapo wanafunzi wanaofaulu darasa la saba na kuendelea kidato cha kwanza!

Yapo mambo mawili ambayo nchi za wenzetu kama Finland wanazingatia katika ufundishaji na ujifunzaji. 

La kwanza ni lile la mwalimu kuwa na fursa ya kushughulikia mwanafunzi mmoja mmoja (individual attention to each student).

Mfano mzuri ni malezi waliotoa mababu zetu kwa watoto wao. Mzazi alimlea mtoto wake mmoja mmoja. 

Kila mtoto alipata fursa nzuri ya kulelewa na baba na mama. Sikumbuki hata siku moja utotoni wazazi waliitisha kikao cha watoto na kutufundisha maadili.

Ilitokea tu pale watu wazima walipotupa hadithi zenye lengo la malezi, lakini wazazi walitambua kwamba kila mtoto anapaswa kupewa malezi kwa nafasi yake.

Katika mfumo wetu ambapo kuna watoto zaidi ya 45 darasani haiwezekani mwalimu amshughulikie mwanafunzi mmoja mmoja.

Kule Finland na nchi nyingi za Ulaya, Japan, Canada na kadhalika hilo linawezekana kwa sababu mwalimu mmoja ana wanafunzi wasiozidi 25 darasani. Hili ni jambo la msingi sana katika ufundishaji na ujufunzaji.

Jambo la pili ni mwalimu apate fursa ya kumshughulikia mwanafunzi kuendana ha vipaji vyake. 

Mfumo wetu wa elimu unaonekana kuamini kwamba wanafunzi wote darasani ni sawa, wote wanapenda hisabati, wote wanapenda fizikia, wote wanatamani kushinda somo la kemia. Hili si kweli. Kila mwanafunzi ana vipaji totaufi, ana malengo totauti. 

Ni makosa kumwadhibu mwanafunzi huyu kwa sababu hapendi hisabati na yule mwingine kwa sababu hapendi historia. 

Makosa haya yote yanafanyika siku zote katika mfumo wetu wa elimu bila hata sisi kutambua kuna shida kama hii. Mfumo wetu wa elimu unakosa maarifa katika mambo haya mawili.

Tufanye nini? Kwanza tuongeze bajeti ya elimu kwa kiwango kikubwa. Tukumbuke shule ni mwalimu na mwalimu bora ndiye nguzo ya elimu bora.

Mwalimu Julius Nyerere alisema: kupanga ni kuchagua. Ni lazima tuchague kuongeza bajeti ya elimu. Fedha zipo, utajiri tunao, shida ni nini? 

Hebu tufikirie mshahara wa mbunge na mshahara wa mwalimu wa shule ya msingi. Je, si wote wanahudumia Taifa hili? 

Wote wawili ni wahudumu muhimu katika taifa. Kwa nini mishahara yao inapishana sana? 

Mifano ni mingi ya watumishi wa Serikali wanaopata mishahara mikubwa ilihali walimu wetu wanateseka shuleni. Shida yetu si fedha, shida ni ubinafsi wa wachache ambao hawajali hatma ya Taifa letu. Tutoke huko.