Mbeya City yashusha mido Mnigeria

Mbeya City iko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa kiungo raia wa Nigeria, Paschal Onyedika Okoli, ikiwa ni harakati za kukisuka kikosi hicho kwa msimu wa 2025-2026, kwa lengo la kuongeza na kuleta ushindani zaidi.

Nyota huyo aliyezaliwa Oktoba 17, 1997, anakaribia kukamilisha dili hilo baada ya kuachana na Klabu ya NK Celik Zenica ya Bosnia and Herzegovina, akiwahi kuichezea pia Bursaspor ya Uturuki, kuanzia ngazi ya timu za vijana hadi ya wakubwa.

Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata, zinaeleza Okoli yupo hatua za mwisho za kukamilisha dili hilo na tayari ametua nchini ili kumalizia mazungumzo hayo, kisha kusaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine.

“Ni kweli amewasili Tanzania na ameomba muda apitie mkataba tuliompa kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho, tuna matumaini makubwa ya kumpata kwa sababu ameonyesha dhamira ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026,” kilisema chanzo hicho.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Mbeya City, Gwamaka Mwankota alisema wachezaji waliokamilisha usajili wao watawaweka wazi, ingawa kuna wengine wanaoendelea na mazungumzo nao na watakapokamilisha watawatangaza wote.

Mbeya City iliyorejea tena Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, tayari imeanza mawindo ya nyota wapya wa kuwaongezea nguvu na hadi sasa inaendelea na usajili ili kuhakikisha inaongeza ushindani msimu ujao.

Hadi sasa, Mbeya City imetambulisha nyota mbalimbali wakiwemo, Ibrahim Ame (Mashujaa FC), Omary Chibada (Kagera Sugar), Kelvin Kingu Pemba (Tabora United), Hamad Majimengi, Habib Kyombo (Pamba Jiji) na kipa, Beno Kakolanya (Namungo).

Wengine ni Yahya Mbegu (Mashujaa), Jeremie Ntambwe Nkolomoni (Coastal Union), Vitalis Mayanga (Geita Gold) na Famara Camara (Ranheim IL), ikiwa ni maingizo mapya yanayotazamiwa kuleta ushindani zaidi katika hekaheka za Ligi Kuu Bara.