Dar es Salaam. Wadau wa elimu nchini wameendelea kuitazama Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 kwa jicho la matumaini makubwa, hasa katika nguzo ya pili inayohusu “Uwezo wa Watu na Maendeleo ya Jamii”.
Kwa mujibu wa dira hiyo, elimu ni injini kuu ya maendeleo ya watu na jamii, na hivyo uwekezaji wake unaelekezwa katika misingi ya haki, usawa, na ubora.
Andiko la Dira 2050 nguzo ya pili, linataja matarajio kadhaa yanayolenga mwishowe kuwezesha uwezo wa watu na maendeleo ya jamii. Dira inataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na:
Mosi; taifa ambalo kila mtoto anapata malezi na makuzi bora, analindwa na anapata msingi imara wa kujifunza na wa maisha, kupitia vituo vya malezi na makuzi, pamoja na elimu bora na ya lazima ya awali, inayotolewa kupitia mfumo madhubuti na endelevu unaojitegemea.
Pili, mfumo wa elimu na mafunzo bora, jumuishi, unaostahimili changamoto, wenye viwango vya ubora vinavyotambulika kimataifa, unaozalisha wahitimu wenye maarifa, ujuzi, na stadi za maisha pamoja na mtazamo chanya utakaowawezesha kuchangia katika maendeleo endelevu ya Taifa. Walimu na wakufunzi mahiri na wenye ari watakuwa nguzo muhimu katika mchakato wa ujifunzaji na ufundishaji.
Tatu, shule na taasisi za elimu salama na jumuishi zinazoweka kipaumbele kwenye ustawi na fursa sawa kwa watoto na vijana wote.
Nne, wahitimu wenye ujuzi stahiki na uwezo wa kushindana na kufanikiwa katika soko la ajira kimataifa.
Tano, jamii bunifu na stahimilivu inayoongozwa na maarifa katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Sita, jamii yenye elimu na maarifa ya fedha ambapo watu wana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi juu ya matumizi ya fedha, kusimamia rasilimali kwa ufanisi na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.
Saba, jamii inayojifunza bila kikomo kwa lengo la kujenga uwezo wa kila Mtanzania kukabiliana na mabadiliko ya kiulimwengu.
‘’Tanzania inalenga kuwa na mfumo wa elimu jumuishi unaoandaa wananchi kwa ujuzi na maarifa yanayohitajika katika uchumi wa kisasa na kimataifa. Ili kuwajengea watoto na vijana uwezo wa kuchangia maendeleo ya uchumi unaoendeshwa na mabadiliko ya kiteknolojia, ni muhimu kuweka mkazo katika stadi za sayansi, teknolojia, uhandisi, na hisabati, pamoja na ujuzi wa kina wa kidijitali, ‘’inasema sehemu ya andiko la Dira 2050 na kuongeza:
‘’Vilevile, stadi za maisha, elimu ya ujasiriamali, na usimamizi wa fedha zinahitajika ili kuwaandaa watoto na vijana kwa dunia inayobadilika, ikiwemo kupunguza pengo la ujuzi na kuimarisha usawa wa kijinsia. Kupitia mfumo jumuishi wa elimu na mafunzo, Tanzania inakusudia kujenga nguvukazi yenye ujuzi, uthabiti, na uwezo wa kuchochea maendeleo ya taifa.’’
Katika mahojiano na Mwananchi, wadau mbalimbali wameeleza mitazamo yao kuhusu matarajio hayo, wakisisitiza kuwa mwelekeo uliowekwa kwenye dira hiyo unaleta sura mpya ya elimu inayozingatia maendeleo jumuishi na yanayomlenga kila Mtanzania kuanzia utotoni hadi utu uzima.
Kwa mujibu wa Dira ya 2050, uwezo wa watu na jamii hujengwa kupitia elimu bora, malezi yenye tija, huduma bora za afya, na hifadhi madhubuti ya jamii. Elimu imewekwa kama msingi wa kutatua changamoto mbalimbali, kuimarisha mshikamano wa kijamii, na kuandaa raia wenye ujuzi na maarifa yanayohitajika katika uchumi wa kisasa.
Mdau wa elimu, James Ndalahwa wa jijini Dar es Salaam anaeleza: “Matarajio ya Dira 2050 ni mapinduzi ya kweli katika elimu. Inaweka msisitizo katika kuanza kujenga uwezo wa mtoto tangu umri mdogo, jambo ambalo linatupa nafasi ya kuandaa kizazi cha kesho chenye uwezo wa kuvumbua, kushindana na kushiriki kikamilifu katika dunia ya leo.”
Katika kuimarisha msingi huo, nyaraka ya dira inaeleza bayana umuhimu wa elimu ya awali kwa watoto, ikisema kuwa asilimia 90 ya ukuaji wa ubongo hutokea kabla ya miaka minane. Hili ni eneo ambalo wadau wengi wamekuwa wakisisitiza lifanyiwe kazi kwa dharura.
“Tukiwekeza katika miaka mitano ya kwanza ya mtoto, tutaondoa mizizi ya umasikini wa elimu kwa vizazi vijavyo. Ni hatua muhimu ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikipuuzwa,’’ anasema mwalimu Clara Msuya kutoka mkoani Morogoro.
Dira ya 2050 pia imeweka bayana kuwa elimu inapaswa kuwa endelevu yaani kujifunza bila kikomo, jambo ambalo limepokewa vyema na wanaharakati wa elimu.
“Elimu ni mchakato wa maisha yote. Tunahitaji mfumo utakaomwezesha kila mtu, hata mzee wa miaka 60, kupata fursa ya kujifunza jambo jipya,” anasema Dk Godfrey Magesa.
Mbali na kujifunza bila kikomo, mfumo wa elimu unatarajiwa kuwa jumuishi kwa maana ya kutotoa mwanya kwa ubaguzi wowote. Hii inajumuisha wanawake, watu wenye ulemavu na wale wanaoishi katika mazingira magumu, ambao mara nyingi wamekuwa wakiachwa nyuma.
Zainabu Ramadhani kutoka asasi moja ya kiraia anaeleza: “Hatua ya kuifanya elimu kuwa jumuishi ni mafanikio makubwa. Tunahitaji kuona shule na taasisi za elimu zikiwa salama na rafiki kwa kila mtoto bila kujali uwezo wake wa kimwili au kijamii.”
Elimu kwa ajira na ushindani kimataifa
Matarajio mengine ya elimu katika dira yanaelekeza kwenye kuhakikisha kuwa wahitimu wa elimu wanakuwa na uwezo wa kushindana katika soko la ajira, siyo tu ndani ya nchi bali pia kimataifa. Hili linahitaji mfumo wa elimu unaozingatia ujuzi wa sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), pamoja na ujuzi wa kidijitali na stadi za maisha.
Kwa mujibu wa dira, Tanzania inalenga kuandaa wahitimu wenye mtazamo chanya, maarifa, stadi za maisha, na ujuzi unaowawezesha kuchangia katika maendeleo ya taifa kwa njia bunifu.
“Tunahitaji kuachana na elimu ya nadharia pekee. Elimu yetu lazima ilenge kumpa kijana uwezo wa kuanzisha biashara, kusimamia fedha zake, na kushindana katika soko la ajira la dunia,” anasema Joseph Mwakalinga, mtaalamu wa maendeleo ya vijana.
Hali hiyo inaleta hitaji la kuboresha mitaala, mazingira ya kujifunzia, na mafunzo ya walimu ili yaendane na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira duniani.
Katika muktadha huo, walimu na wakufunzi wamewekwa kama mhimili wa mabadiliko ya elimu. Dira ya 2050 inasisitiza kuwa mafanikio ya mfumo wowote wa elimu hayawezi kupatikana bila walimu mahiri na wenye ari, kama anavyosisitiza Sarah Ngoi, mkurugenzi wa shule binafsi jijini Arusha:
“Uwekezaji katika mafunzo ya walimu ni jambo lisiloepukika. Tunahitaji walimu waliobobea si tu katika somo lao, bali pia katika teknolojia, ubunifu na malezi ya watoto.”
Kwa sasa, juhudi zimeanza kuonekana katika kuboresha miundombinu ya kujifunzia, kupanua fursa za mafunzo kazini kwa walimu, pamoja na kupitia upya sera na mitaala ya elimu.
Katika dunia ya sasa yenye changamoto nyingi, dira imetoa mwongozo wa kuhakikisha kuwa shule na taasisi za elimu ni maeneo salama na yenye fursa sawa kwa watoto na vijana wote. Hii ni pamoja na kutokomeza ukatili shuleni, kuweka mazingira rafiki kwa mtoto wa kike, na kuimarisha huduma za kijamii kwa wanafunzi.
“Tanzania mpya inahitaji shule zisizotisha bali zinazojenga,” anasema mchambuzi wa elimu, Dk Elibariki Ndegela, akiongeza: “Shule jumuishi si neno tu la kisiasa, bali linahitaji utekelezaji wa dhati katika ngazi zote.”
Katika sura ya mwisho ya matarajio, Dira ya 2050 inaeleza dhamira ya kujenga jamii inayotumia maarifa katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Elimu ya fedha, ujasiriamali, na usimamizi wa rasilimali imewekwa kama nyenzo muhimu kwa jamii hiyo.
Aidha, Tanzania inatarajia kuwa jamii inayojifunza bila kikomo, inayoongozwa na maarifa, maadili, na mshikamano. Lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, kushiriki kikamilifu katika maisha ya taifa, na kukabiliana na changamoto za kidunia.
Kwa kuangazia dira hii, ni wazi kuwa mwelekeo wa elimu wa Tanzania unalenga si tu kutoa maarifa, bali pia kujenga utu, uwezo wa kuhimili mabadiliko, na misingi ya maendeleo jumuishi. Hata hivyo, changamoto bado zipo ikiwemo uhaba wa walimu, miundombinu duni, na utekelezaji wa sera.
“Dira ni ramani nzuri, lakini bila hatua za makusudi na rasilimali za kutosha, tutabaki na ndoto. Serikali, sekta binafsi, na jamii kwa ujumla lazima tushirikiane,’’ anaeleza Michael Munishi.