MSHAMBULIAJI mpya wa Namungo, Herbert Lukindo amesema amejipanga vyema kuhakikisha anafanya vizuri na kikosi hicho na kuziba pengo la baadhi ya nyota walioondoka klabuni hapo akiwemo Meddie Kagere.
Lukindo amejiunga na Namungo kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea KenGold ya Mbeya iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu msimu uliopita.
Namungo imesafisha kikosi chake dirisha kubwa ikiachana na nyota 12 akiwemo mshambuliaji mkongwe, Meddie Kagere na beki Erasto Nyoni, Saleh Karabaka na Emmanuel Asante.
Wengine ni Erick Malongi, Derick Mukombozi, Issa Abushehe, Najim Mussa, Joshua Ibrahim, Erick Kapaito, Emmanuel Charles na Anderson Solomon.
Baada ya fagio hilo, Namungo imesajili wachezaji wapya 11 hadi sasa akiwemo mshambuliaji hatari, Heritier Makambo, Andrew Chamungu, Saleh Machupa, Cyprian Kipenye, Rashid Mchelenga, Mussa Malika, Lucas Kikoti, Abdallah Denis, Abdallah Mfuko na Hussein Kazi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lukindo aliyewahi kukipiga Pamba Jiji, Biashara United na Mbao alisema anahitaji kufanya vizuri msimu huu ili aendelee kubaki Ligi Kuu na kufikia malengo ya kucheza soka la ushindani.
“Nimefurahi kubaki ligi kuu naamini msimu huu utakua bora zaidi ya uliopita. Sasa hivi ni kipindi cha maandalizi najiandaa vizuri nadhan msimu ukianza mambo yatakua mazuri,” alisema Lukindo.