ADEM YASHIRIKI KIKAO KAZI CHA WENYEVITI WA BODI NA WATENDAJI WAKUU WA TAASISI ZA UMMA ARUSHA

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Mtendaji Mkuu wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dkt. Maulid J. Maulid, ameungana na viongozi wengine wa taasisi mbalimbali za umma kushiriki kikao kazi cha Wenyeviti na Wakuu wa Taasisi kinachoendelea jijini Arusha kuanzia Agosti 23 hadi 26, 2025.

Kikao hicho kimeandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kufunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Phillip Isidor Mpango, ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa waandaaji, lengo la kikao hicho ni kujengea uwezo Wenyeviti na Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma kwa kubadilishana uzoefu juu ya uimarishaji wa utendaji, kutambua changamoto na kuibua mbinu sahihi za kuongeza ufanisi katika usimamizi wa taasisi hizo.

Aidha, kikao hicho kinatarajiwa kuwezesha taasisi za umma kufikia malengo ya kuanzishwa kwake pamoja na malengo makuu ya Serikali, ikiwemo kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.

Katika hotuba zake, viongozi waliwataka washiriki kuhakikisha uwajibikaji, ushirikiano na sekta binafsi na kuongeza tija katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Kikao hicho kitafungwa rasmi tarehe 26 Agosti 2025 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Mashaka Biteko.