MIEMBENI imefuzu robo fainali ya michuano ya Yamle Yamle Cup inayoendelea kisiwani Unguja kufuatia ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Welezo City.
Mchezo huo uliopigwa jana Jumatatu saa 12:30 jioni kwenye Uwanja wa Mao A, dakika tisini matokeo yalikuwa sare ya mabao 2-2.
Wakasa Mbaraka aliitanguliza Miembeni kwa kufunga mabao mawili dakika ya 2 na 30, kabla ya Aboubakar Lipi na Najim Maalim dakika ya 66 na 84 kuisawazishia Welezo na kufanya mikwaju ya penalti kuamua mshindi.
Kabla ya mchezo huo, majira ya saa 10:00 jioni Mwembe Makumbi Combine iliichapa Kajengwa FC mabao 2-0 na kufuzu robo fainali ya michuano hiyo.
Mabao ya Yakoub Said dakika ya 45 na Michael Joseph aliyekamilisha hesabu hiyo dakika ya 87, yalitosha kuifanya Mwembe Makumbi kuondoka uwanjani wakiwa wababe.
Mashindano hayo yataendelea leo jioni ambapo Nyamanzi City itavaana na Magari ya Mchanga huku Mazombi FC wakitoana jasho na Kundemba.