Othman: Lengo letu ni amani ya kudumu Zanzibar

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema malengo ya chama hicho ni kuifanya Zanzibar kuwa na amani na utulivu wa kudumu na siyo kuishia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Masoud ameyasema hayo jana, Jumatatu Agosti 25, 2025 alipozungumza na ujumbe wa kamati ya mambo ya nje ya Bunge la Marekani, uliofika  kujadili, kujifunza na kusikiliza moja kwa moja, hisia na maelezo ya viongozi wakuu wa nchi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.


Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema chama hicho kinashiriki uchaguzi siyo kwa sababu ya utashi wa kisiasa, bali ni kwa masilahi ya amani ya kudumu.

Amesema amani, utengamano na utulivu wa kudumu ni muhimu kwa uchumi wa Zanzibar, zaidi ya utashi wa kisiasa.

Hata hivyo, amesema kuelekea uchaguzi wa mwaka huu kuna viashiria vya ubadhirifu na uporaji wa demokrasia na matumizi mabaya ya dola.

Amesema azma hiyo mbaya inabainika pia kupitia kura ya siku mbili, iliyokosa mantiki na misingi ya kisheria, huku Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ikionekana kuziba masikio, licha ya kuwapo lawama.


“Kila tulipopaza sauti pamoja na watetezi wengine wa demokrasia, vikiwemo baadhi ya vyama vya siasa, ZEC imekuwa bubu na haionyeshi hisia yoyote. Si ya ushauri au angalau hata majadiliano.

“Katika mahitaji ya sasa ni mabadiliko na mageuzi makubwa ya mfumo wa uchaguzi nchini, kwani dhamira yao si njema na haiashirii kuwa na uchaguzi huru na wa haki, hali ambayo inaiweka Zanzibar na wananchi wake roho juu,” amesisitiza.

Hata hivyo, amesema wameamua kushiriki uchaguzi, wakiamini kwamba nchi inahitaji mabadiliko na mageuzi ya kimfumo, taasisi na uendeshaji kwa ujumla.

“Tunaamini tukishinda uchaguzi ndani ya miaka mitano, Zanzibar inaweza kurudi katika hadhi yake. Tukitarajia kuwepo mfumo wa uchaguzi wa haki ambao ni mfano bora kwa Afrika na ulimwenguni,” amesema.


Amesema Zanzibar yenye bahati na uzuri wake wa asili, haikupaswa kuwa ilipo sasa kiuchumi, kwa kuilinganisha na nchi za aina yake, mathalan visiwa vya Mauritius na Ushelisheli.

Amesema Zanzibar ilikuwa nchi ya mwanzo kwa mataifa ya kusini mwa Jangwa la Sahara, kuwa na mahusiano ya kidiplomasia, baina yake na Marekani mwaka 1833.

“Naamini bado tunayo fursa ya kuendeleza na kukuza mahusiano haya, kwa ajili ya maendeleo ya nchi zetu,” amesema.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la ‘Congress’ la Marekani, Philip Thomas amesema taasisi yake pamoja na serikali ya Marekani, zitapendezwa kuona Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, zinaendesha uchaguzi kwa misingi ya uhuru na haki.

“Wageni, na hasa kutoka nchini Marekani wanapendelea kuja kutalii na kujionea uzuri wa Zanzibar, katika fukwe zake za kupendeza, historia na utamaduni wake, bali hawapendi kabisa kuja wakaona machafuko na vurugu,” amesema.

Katika ujumbe huo, walikuwemo pia maofisa waandamizi kutoka ubalozi wa Marekani nchini, wakiongozwa na Richard Allen, mkuu wa kitengo cha siasa anayehusika na mambo ya Zanzibar.