……………….
Wakazi wa Jiji la Mwanza wamepongeza kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme, wakisema imeleta matumaini mapya ya kupunguza gharama za maisha na kuboresha afya kwa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambao husababisha madhara kiafya na uharibifu wa mazingira.
Kampeni hiyo, inayoendeshwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na UKAid na taasisi ya Modern Energy Cooking Services (MECS), inalenga kupunguza utegemezi wa nishati chafu kama kuni, mkaa na gesi, na kuhamasisha matumizi ya nishati salama, rafiki kwa mazingira na afya ya mtumiaji.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Medical Research, Yudas Hume, amesema kuwa zaidi ya kaya 800 zenye wakazi wapatao 22,000 watanufaika na kampeni hiyo kupitia elimu waliyoipata kuhusu matumizi ya nishati safi ya umeme kwa kupikia.
Kwa mujibu wa Dora Urio, mhamasishaji wa nishati safi kutoka shirika la TaTEDO-SESCom, Serikali inalenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kitaifa za kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuboresha afya ya jamii.
Katika soko la Kishimba, wauzaji wa samaki wamelalamikia madhara ya moshi unaotokana na matumizi ya kuni, wakisema huwasababishia matatizo ya macho na kifua. Mwenyekiti wa soko hilo, Khalid Masesa, amesema moshi huo pia huathiri biashara kwa kuwafukuza wateja.
Muuzaji wa samaki, Rozy Zakaria, amesema matumizi ya majiko ya umeme yataboresha mazingira ya biashara, kupunguza moshi na kuongeza idadi ya wateja. Wakazi wa Mwanza wameitaka Serikali kuongeza kasi ya usambazaji wa elimu na vifaa vya nishati safi kwa bei nafuu ili kusaidia kaya nyingi zaidi kufikia mabadiliko hayo.
Kwa ujumla, kampeni hiyo imepokelewa vyema na wakazi wa Mwanza ambao wanatumaini kuwa itakuwa chachu ya kubadilisha maisha yao kwa njia chanya na endelevu.