Gavana wa Benki Kuu agoma kufukuzwa kazi na Trump

Washington. Gavana wa Benki Kuu ya Marekani, Lisa Cook, ameanzisha mvutano na Rais Donald Trump kwa kukataa kuondoka kwenye wadhifa wake baada ya rais huyo kutangaza kumfukuza kazi.

Mvutano huo umetokea baada ya jana Jumatatu Agosti 25, 2025 Rais Trump kutangaza amemfukuza kazi Cook kwa sababu maalumu ikiwamo kutaka benki hiyo ipunguze viwango vya riba.

Kufukuzwa kwa Cook ni mara ya kwanza katika historia ya miaka 111 ya Benki Kuu nchini humo, huku Trump akieleza kwamba siku si nyingi atamteua gavana mpya atakayemuunga mkono katika matakwa yake ya kupunguza viwango vya riba.

Hata hivyo, Cook alitoa taarifa Jumatatu usiku akisisitiza kuwa hataondoka kwenye wadhifa huo.

“Rais Trump amedai kunifukuza kwa sababu maalumu wakati hakuna sababu yoyote kisheria, na hana mamlaka ya kufanya hivyo sitajiuzulu. Nitaendelea kutekeleza majukumu yangu kusaidia uchumi wa Marekani kama nilivyokuwa nikifanya tangu mwaka 2022,” amesema.

Wakili wake, Abbe Lowell, pia alitoa taarifa kali dhidi ya Trump na kuahidi kuchukua hatua dhidi ya kile alichokiita hatua isiyo halali.

“Rais Trump kwa mara nyingine ameenda kwenye mitandao ya kijamii kunifukuza kupitia tweet, na mara nyingine tena tabia yake ya kutisha imekosa msingi wowote wa mchakato, hoja au mamlaka ya kisheria,” amesema Lowell na kuongeza: “Tutachukua hatua yoyote itakayohitajika kuzuia jaribio lake la kuvunja sheria,”  amesema.

Hatua hiyo ya Trump ni mapambano yake ya kutaka kuwa na udhibiti mkubwa juu ya taasisi ambayo kwa muda mrefu imechukuliwa kuwa huru kutoka kwenye siasa za kila siku.

Rais Trump amekuwa akimsukuma Mwenyekiti wa Benki Kuu, Jerome Powell, akitaka kupunguza kiwango cha riba za muda mfupi. Kumfukuza Cook kunaweza kufungua njia kwa Trump kumteua mfuasi wa MAGA (Make America Great Again) au ‘Ifaye Marekani kuwa taifa kubwa tena’

Katika barua aliyoposti kwenye jukwaa lake la Truth Social, Trump alisema anamfukuza Cook kutokana na madai kuwa alifanya udanganyifu wa mikopo ya nyumba.

“Kutokana na tabia yako ya udanganyifu na huenda ya kihalifu katika suala la kifedha… sina imani na uadilifu wako,” Trump aliandika.

Hadi sasa, Powell amesisitiza kuwa viwango vya riba vinapaswa kubaki juu kwa sababu mfumuko wa bei bado haujashuka kufikia lengo la asilimia mbili. Bei za bidhaa kwa watumiaji bado ni juu, na hivyo Benki Kuu imeacha riba ya asilimia 4.5 tangu Desemba 2024.

Rais Trump ameonesha wazi kutokubaliana na uamuzi huo, akitaka ipunguzwe hadi asilimia tatu.

Viwango vya chini vya riba hufanya iwe rahisi kwa wafanyabiashara kukopa pesa, na muhimu zaidi, hupunguza gharama ya mikopo kwa Wamarekani wa kawaida, hali inayowafanya kuwa na uwezo zaidi wa kutumia fedha kwenye bidhaa na huduma. Viwango vya juu vya riba hupunguza kasi ya ongezeko la bei.

Uamuzi wa Trump wa kumfukuza kazi Cook imeelezwa ni hatua kali na hasa ikizingatiwa kuwa kwa miezi kadhaa, amekuwa akijaribu kupunguza uhuru wa Benki Kuu.

Kwa kawaida, Benki Kuu hujilinda dhidi ya mashinikizo ya kisiasa wakati inajaribu kudumisha mfumuko wa bei wa chini na ukuaji wa ajira kote Marekani.

Ripoti ya ajira ya Julai ilikuwa mbaya, jambo lililompa Trump hoja kwamba viwango vya riba vinapaswa kupunguzwa. Wakati huohuo, kiwango cha msingi cha mfumuko wa bei kiliongezeka tena huku wachumi huru wamegawanyika kuhusu njia sahihi ya kuchukua.

Taarifa zinasema kitendo cha kumuondoa Cook kwenye bodi ya uongozi wa Benki Kuu kunampa Trump nafasi ya kumteua mtu mtiifu kwake, kwa kuwa ameshaweka wazi atateua  maofisa wanaounga mkono kupunguza viwango vya riba.

Hivi karibuni Trump ameongeza juhudi zake za kushinikiza viwango vya chini kwa kumshambulia mara kwa mara kiongozi wa Benki Kuu, Jerome Powell.

Kupunguza viwango vya riba kunaweza kuwaongezea Wamarekani na wafanyabiashara fedha za kutumia, jambo ambalo linaongeza matumizi, bei za hisa na akiba za kustaafu.

Rais pia amekuwa akionyesha nia ya kumwondoa Powell ili kushinikiza upunguzaji wa viwango kwa njia ya kisiasa.

Wiki iliyopita, Scott Bessent, Katibu wa Hazina wa Ikulu ya White House, alisema ataanza kufanya mahojiano ya kutafuta mrithi wa Powell, Septemba ikiwa ni miezi tisa kabla ya muhula wake kwisha.

Mapema mwezi huu, Trump alimteua Mwenyekiti wa Baraza la Washauri wa Uchumi, Stephen Miran, kumalizia muhula uliobaki baada ya Gavana Adriana Kugler kujiuzulu ghafla.

Bill Pulte, mteule wa Trump katika shirika linalosimamia mashirika ya mikopo ya nyumba Fannie Mae na Freddie Mac, alitoa shutuma dhidi ya Cook wiki iliyopita.

Pulte anadai kuwa Cook alidai kuwa na makazi makuu mawili  huko Ann Arbor, Michigan na Atlanta mwaka 2021 ili kupata masharti bora ya mikopo ya nyumba.

Msimamizi huyo pia aliposti sehemu ya barua yake kwa Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Pam Bondi, akisema kuwa shirika lake limepata nyaraka za mikopo ya Cook, na kueleza kuhusu mikopo hiyo miwili ya Juni na Julai 2021.

“Anapaswa kujiuzulu kwa sababu alichofanya kinatosha kufukuzwa kazi,” aliandika katika chapisho tofauti.

Tangazo hilo lilitolewa siku chache baada ya Cook kusema hataki kuondoka kazini licha ya Trump hapo awali kumtaka ajiuzulu. Bodi ya Benki Kuu ina wajumbe saba, na hatua ya Trump inaweza kuwa na athari kubwa kiuchumi na kisiasa.

Viwango vya riba ya mikopo mara nyingi huwa juu kwa nyumba za pili au zile zilizonunuliwa kwa ajili ya kupangishwa.

Trump alisema wakati wa kutangaza hatua hiyo kuwa ana mamlaka ya kikatiba ya kumuondoa Cook, lakini kufanya hivyo kutazua maswali kuhusu udhibiti wa Benki Kuu kama chombo huru.

Kufukuzwa huko kunaweza kuchochea mapambano ya kisheria, na huenda Cook akaruhusiwa kubaki kwenye nafasi yake wakati kesi ikiendelea. Cook atalazimika kupambana kisheria binafsi kama mlalamikaji, badala ya Benki Kuu yenyewe.