Unguja. Baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kutoa ratiba ya kuchukua na kurejesha fomu, mtiania urais kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi anatarajia kuchukua fomu Agosti 30, 2025.
Siku hiyo baada ya kuchukua fomu, Dk Mwinyi ambaye ndiye Rais wa Zanzibar anayemaliza awamu ya kwanza ya utawala wake, atazungumza na wananchi katika uwanja wa Mao kutoa mwelekeo wake kisha litafanyika tamasha kubwa ambalo litajumuisha wasanii wa muziki tofauti kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi, ratiba ya kuchukua fomu za udiwani, uwakilishi na urais inaanza Agosti 28 hadi Septemba 10, 2025 na uteuzi utafanyika Septemba 11, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 26, 2025, Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho Zanzibar, Khamis Mbeto amesema Dk Mwinyi atawasili ofisi za Tume saa 4:00 asubuhi.
“Mgombea wetu ataondokea Mazizini atafika Tume akiongozwa na Naibu Katibu Mkuu, sekretarieti na viongozi wastaafu wa chama maana tumeambiwa awe na watu wasiozidi 20,” amesema.
Amesema baada ya kumaliza kuchukua fomu, atapanda gari maalumu la wazi kupitia Kwalaju, Magereza, Miembeni Mapinduzi Square hadi ofisi za chama, Kisiwandui.
Mbeto amesema baada ya mtiania wao kufika makao makuu ya chama, atazulu kaburi la hayati Abeid Amani Karume, kisha kuzungumza na wazee wa chama na ataelekea katika viwanja vya Mou ambapo atazungumza na wananchi.
Kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho, baada ya kumaliza kuzungumza na wananchi katika uwanja huo, kutakuwa na tamasha ambalo litajumuisha wasanii mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Visiwani
“Lengo ni kusikiliza na kuzindua nyimbo zilizotungwa na wasanii hao ambazo zitatumika wakati wa kampeni.”
Miongoni mwa wasaani watakaoshiriki kutumbuiza katika tamasha hilo ni pamoja na Dulla Makabila, Zuchu, Mboso Marioo na Jux.