Tanga. Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mafia mkoani Pwani, Salehe Kikweo amefariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu Hospitali ya Mji Handeni, Mkoa wa Tanga.
Taarifa ya kifo hicho imetolewa na Katibu wa CCM, Wilaya ya Handeni, Mayassa Kimbau leo Jumanne Agosti 26, 2025 kupitia mitandao ya kijamii na kueleza Kikweo amefariki dunia asubuhi ya leo hospitalini hapo na mwili wake umehifadhia hapohapo.
Amesema taarifa zaidi kuhusu wapi yatafanyika mazishi yake itatolewa baadaye baada ya familia na viongozi wengine kukutana ili kupanga taratibu vizuri. Kikweo ni mwenyeji wa Handeni.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa ya msiba wa ndugu yetu, kaka yetu mpendwa Kikweo aliyefariki asubuhi hii ya leo na mwili umehifadhiwa Hospitali ya Bomani, mipango ya mazishi inaendelea kufanyika,” imeeleza taarifa hiyo.
Akizungumzia msiba huo, Mwenyekiti wa CCM, wilayani Handeni ambaye ni mmoja wa viongozi aliyefanya kazi na katibu huyo kwa muda, amesema kifo cha Kikweo kimetokea ghafla na wala hajaugua.
Amesema jana Jumatatu Agosti 25, 2025 alikuwa naye kwenye shughuli zao za kawaida ambapo hadi jioni waliagana na kila mmoja kuelekekea kwake, na hakuwa na dalili zozote za kuumwa.
“Lakini usiku alipigiwa simu na marehemu akiomba msaada wapi atapata huduma ya umeme akaendelee na shughuli zake, kwani kwake umeme ulikuwa unasumbua na alikuwa na kazi nyingi za kufanya,” amesema.
“Tuliongea kwenye simu akiomba nimtafutie sehemu ambayo ataweza kupata huduma ya umeme wa jenereta kutokana na shida ya umeme kwake, lengo akaendelee na shughuli zake ambapo pia alisema hakuwa anajikisia vizuri anahitaji utulivu,” amesema Changago.
Amesema alitafuta dereva wa pikipiki na kufanikisha kupelekwa sehemu yenye umeme kwa ajili ya kufanya shughuli zake.
Marehemu Salehe Kikweo atakumbukwa zaidi katika harakati zake za kukipambania chama chake katika chaguzi hasa Handeni, ambapo aliwahi kufanya tukio la kuvaa Baibui ili kuweza kufuatilia vijana waliotaka kuhujumu shughuli za uchaguzi 2015.
Alifanya kazi zaidi na aliyekuwa mbunge wa Handeni wakati huo likiwa ni jimbo moja marehemu, Abdallah Kigoda ambae aliongoza kwa muda mrefu.