Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akimkabidhi Cheti Mwenyekiti wa Bodi ya Hifadhi ya Ngorongoro, Jenerali Venance Mabeyo wakati wa ufungaji wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (CEOs Forum 2025) kilichofanyika Agosti 26, 2025 katika Ukumbi wa AICC Jijini Arusha. Cheti hicho kimekabidhiwa kwa kuwa NCAA imekuwa sehemu ya wadhamini wa kikao hicho.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akifunga Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (CEOs Forum 2025) kilichofanyika jijini Arusha katika Ukumbi wa AICC
……………………….
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewahimiza Wenyeviti na Wakuu wa Taasisi za
Umma nchini kusimamia utekelezaji wa
maazimio ya kimkakati yanayofikiwa katika vikao kazi wanavyofanya kwa kutambua kuwa wamebeba dhamana ya
kuboresha maisha ya Watanzania kupitia
mtaji wa shilingi Trilioni 86 ambao Serikali imewekeza kwenye Taasisi na mashirika yake..
Dkt. Biteko ameyasema hayo tarehe 26 Agosti 2025
jijini Arusha wakati
akifunga kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na
Watendaji Wakuu wa
Taasisi za Umma (CEOs FORUM 2025).
“Watanzania wanawategemea ninyi kuwabadilishia maisha, kama tunazungumza kuhusu
umaskini wa watu, Serikali inapaswa kuwa
kiongozi wa kuwaondolea watu umaskini wao, hivyo
hamna budi kutambua kuwa mnalo deni la kuboresha hali zetu na maisha yetu.” Amesema Dkt. Biteko
Dkt. Biteko amewahakikishia Watendaji hao kuwa
Serikali katika ngazi
zote inatambua mchango wa taasisi na mashirika katika ukuaji wa uchumi na pia inatambua
mchango wa vikao kazi vya watendaji hao
ambavyo vimepelekea mashirika kuongeza mchango wake katika mfuko mkuu wa Taifa.
” Vikao kazi hivi mnavyofanya vimeonesha
mchango wake katika uchumi,
mfano katika kikao kazi cha mwaka 2024 mliazimia
mashirika ya umma
yaboreshe utendaji na kuongeza uchangiaji
katika mfuko mkuu wa Serikali na
matokeo yameonekana mfano Shirika la Maendeleo ya Petroli ( TPDC) liliongeza uchangiaji wake kwa asilimia 100,
shirika hili liliongeza uchangiaji wake
kutoka shilingi bilioni 5.5 kwa mwaka 2023/2024
hadi shilingi bilioni 11.1 mwaka 2024/2025.” Amesema Dkt.Biteko
Ameongeza kuwa, uchagiaji wa Shirika la Nyumba
la Taifa (NHC) umeongezeka kwa
asilimia 363 katika mfuko mkuu wa Serikali ambapo NHC ilichangia shilingi bilioni 1.2 mwaka 2023/ 24 na
mwaka 2024/2025 ilichangia shilingi
bilioni 5.5.
Dkt. Biteko amewaeleza Wenyeviti wa Bodi na
Wakuu wa Taasisi kuwa “Rais Samia pamoja
na kuthamini mchango wenu kwa Serikali anatarajia mengi kutoka kwenu na Watanzania wana matarajio
makubwa hasa wakati tukielekea
kwenye utekelezaji wa Dira 2050, endeleeni kuongeza mchango wenu kwenye ukuaji wa uchumi, mjitegemee
na muwe mfano wa taasisi binafsi.”
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ametaka
viongozi hao kufanyia kazi
agizo lililotolewa na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango la
kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato.
Pia amempongeza Msajili wa Hazina kwa kuwa na
maono ya kuratibu kikao
kazi hicho ili kujadili masuala yatakayosukuma
mbele utendaji wa taasisi.
Katika hafla hiyo, Dkt. Biteko hakuacha
kukumbusha kuhusu ushiriki wa
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ambapo amesema uchaguzi huo uwe ni ajenda ya watu wote
wakiwemo Wenyeviti wa Bodi na Wakuu
wa Taasisi hivyo waone kuwa wana wajibu wa kuwasisitiza watu kwenye taasisi zao kujitokeza kusikiliza wagombea
na baadaye kupiga kura kwa amani
kwani kukiwa na amani mashirika hayo pia yatafanya
vizuri zaidi.
Naibu Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Mhe.
Stanslaus Nyongo kwa upande wake,
amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dira na muongozo katika kuendeleza mashirika ya umma ili
yaweze kuwa na tija nchini.
Amesema katika siku tatu za kikao kazi washiriki
wamejifunza na kubadilishana uzoefu
kupitia watoa mada wa ndani na nje ya nchi waliobobea.
Amesema Wizara ya Mipango na Uwekezaji
itahakikisha maazimio ya kikao kazi
hicho yanatekelezwa ipasavyo, pia Wizara itasimamia mageuzi ya kuhakikisha mashirika ya umma yanachangia ukuaji
wa pato la taifa hadi kufikia Dola
za Marekani trilioni 1 ifikapo 2050 ambapo kwa sasa pato la taifa ni dola za Marekani bilioni 85.
Kwa upande wake Salim Kali, Kaimu Mkuu wa Mkoa
wa Arusha amesema wilaya 6 za Mkoa wa
Arusha zimefikiwa na umeme hadi ngazi ya vijiji, pia miradi ya maji imefanyika pamoja na miundombinu ya
Barabara ambayo imewezesha maisha bora
kwa watu wa aina zote wakiwemo watalii.
Awali, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu
alisema kuwa katika kikao kazi hicho
kampuni zaidi 300 zimeshiriki huku washiriki wakiwa ni zaidi ya 650.
Alisema kikao kilikuwa na majadiliano
mbalimbali ya kina yanayolenga kusukuma
mbele uchumi wa nchi na kusimamia uwekezaji wa Serikali kwa
taasisi za umma wa zaidi ya shilingi trilioni
86.
Mkutano huo wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji
Wakuu wa Taasisi za Umma
uliongozwa na kaulimbiu ya
“Ushirikiano Endelevu wa Kibiashara
katika Mazingira Shindani Kimataifa- Nafasi ya
Mashirika ya Umma.”
Teresia Xavier Mhagama