KIUNGO wa timu ya taifa la Sudan, Abdel Raouf amefunguka kuhusu uhusiano wake na Kocha Kwesi Appiah, akiueleza kuwa ni zaidi ya kocha na mchezaji kwenye kikosi hicho ambacho jana, Jumanne kilicheza mechi ya nusu fainali ya CHAN dhidi ya Madagascar.
Nyota huyo ambaye ni mchezaji wa Al-Hilal, alisema kocha huyo raia wa Ghana ni kama mlezi kwa namna ambavyo amekuwa akiwajenga wakati ambao wamekuwa wakiipambania Sudan mbali na nyumbani kutokana na machafuko yanayoendelea nchini humo.
“Anatusimamia, anatupa moyo na anatufanya tuhisi kuwa thamani yetu ipo. Ameleta heshima, imani na mshikamano kwenye timu hii,” alisema Raouf mwenye mabao mawili katika mashindano ya CHAN.
Aliongea kwa kusema; “Tumekuwa na fahari na ujasiri wa kukabiliana na hiki ambacho kinaendelea, tunaimani kwamba siku moja kila kitu kitakuwa sawa na tutakuwa na amani na familia zetu ndugu, jamaa na marafiki wataishi kwa amani.”
Raouf alieleza pia Appiah amekuwa akiwaeleza kuwa wanayo nafasi ya kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa Sudan, nafasi hiyo ni kila mmoja kufanya kile kinawezekana uwanjani ili kuwapa faraja nyumbani na pengine siku moja wanaweza kuwaunganisha kupitia wao.
Akiongelea maisha yake ya soka, alisema; “Nilipenda mpira tangu nikiwa mdogo, na nilibarikiwa kukutana na makocha wazuri walionihimiza kupigania ndoto zangu.”
Hii ilimfungulia milango ya kuwa mchezaji wa kulipwa ambapo alianza kwa kuichezea Al-Afarga Port Sud, Al-Shurta SC (Al-Qadarif), El Hilal El Obeid kabla ya 2020 kutua Al-Hilal.
Katika mashindano ya CHAN 2024, kiungo huyu amekuwa mhimili mkubwa wa timu hiyo ya taifa. Uwezo wake wa kudhibiti mchezo na kusambaza mipira katika maeneo yote ya uwanja umemfanya kuwa injini ya kikosi hicho cha Appiah.