Kiti cha uenezi CCM moto, miaka minne ya Rais Samia

Dar es Salaam. Kiti cha Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kuwa kaa la moto kwa kila anayeteuliwa kukikalia kwani wamekuwa wakitumikia kwa muda mfupi kabla ya kuondolewa.

Tangu Rais Samia Suluhu Hassan ameingia madarakani Machi 19, 2025 na kuwa mwenyekiti wa chama hicho, tayari CCM kimekuwa na makatibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo watano katika kipindi cha miaka minne pekee.

Mabadiliko ya hivi karibuni ni yale ambayo Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Nec) imeyafanya Agosti 23, 2025 kwa kumteua Kenan Kihongosi kuwa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, akichukua nafasi ya Amos Makalla ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Baadhi ya wachambuzi wamebainisha kwamba nafasi hiyo ina presha kubwa na kwamba baadhi ya makada wanaoteuliwa wamekuwa wakikivusha chama kwenye nyakati fulani, hivyo baada ya kuvuka, anatafutwa mwingine.


Alipoingia madarakani na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM, Rais Samia alifanya kazi na Humphrey Polepole, kama katibu wa itikadi na uenezi aliyemkuta. Polepole aliteuliwa kushika nafasi hiyo Desemba 13, 2016 akijaza nafasi iliyoachwa na Nape Nnauye.

Aprili 30, 2021, halmashauri kuu ya CCM ilimteua Shaka Hamdu Shaka kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo akichukua nafasi ya Polepole ambaye alibaki kuwa mbunge na baadaye kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi na baadaye kuhamishiwa Cuba.

Januari 14, 2023, Halmashauri Kuu ya CCM ilifanya uteuzi mwingine wa Sophia Mjema kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo akichukua nafasi ya Shaka aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.

Mjema alifanya kazi hiyo kwa miezi 10 pekee ambapo Oktoba 22, 2023, Paul Makonda aliteuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM kujaza nafasi yake baada ya yeye kuteuliwa kuwa Mshauri wa Rais, Masuala ya Wanawake, Watoto na Makundi Maalumu.

Safari ya Makonda kwenye nafasi hiyo imekuwa ya muda mfupi kwa kuwa amedumu kwa miezi mitano hadi Machi 31, 2024 Rais Samia alipofanya mabadiliko kwa kumtoa na kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Aprili 4, 2024, NEC ilimteua Makalla kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, akichukua nafasi ya Makonda. Wakati akiteuliwa kwenye nafasi hiyo, Makalla alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Makalla ametumikia nafasi ya Mwenezi kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi mine, kabla ya kuteuliwa na Rais Samia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, akijaza nafasi iliyoachwa wazi na Kihongosi.

Wakati huohuo, halmashauri kuu ya CCM ilimteua Kihongosi kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo ambapo amekuwa mtu wa tano kushika nafasi hiyo tangu Serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani.

Viongozi wa ngzi ya kata na mkoa wa Dar es Salaam wakiwa katika ukumbi kwaajili ya kikao kazi na katibu wa NEC Itikadi,Uenezi na Mafunzo,Kenani Kihongosi.Picha



Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie amesema kuna mambo mengi yanajitokeza, hivyo mabadiliko yanayotokea yanalenga kuendana na mambo hayo na hali halisi katika maisha ya jamii.

“Wakati Rais Samia anaingia madarakani, mikutano ya vyama vya siasa ilikuwa imesitishwa, lakini alipoingia, mabadiliko fulani yakafanyika, shughuli za kisiasa zikaendelea kufanyika, ukosoaji unafanyika, kwa hiyo lazima waendelee kujipanga kuelekea uchaguzi unaokuja,” amesema.

Mwanazuoni huyo amebainisha kwamba aina ya watu wanaokuwepo kwenye muundo wa chama lazima nao wabadilike ili kubeba majukumu ya chama ili kiweze kuvuka salama katika kipindi hicho.

“Aina ya watu wanaowekwa kwenye hiyo nafasi lazima nayo ibadilike. Kila mtu ana hulka yake, vionjo vyake na namna yake ya kufanya kazi, kwa hiyo ilikuwa ni lazima mabadiliko hayo yafanyike ukizingatia kwamba Rais Samia alikipokea chama katikati,” amesema.


Ameongeza kuwa mwenyekiti wa sasa, Rais Samia, ana haiba yake tofauti na mtangulizi wake, hivyo anaona ni muhimu kutafuta watu wanaoendana na haiba yake ili kukifanya chama kiendelee kubaki na ushawishi.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Gregory Songo amesema kubadilishwa kwa watendaji hao kunamaanisha kwamba hajapatikana mtu anayetosha katika nafasi hiyo katika hali zote.

“Tuliona Polepole alikaa kwenye nafasi hiyo katika kipindi chote cha uongozi wa hayati John Magufuli, lakini katika kipindi hiki cha Samia, watu watano wamebadilishwa kwenye ofisi hiyo, maana yake ni kwamba hawajatosha,” amesema.