Oussama katika vita ya ufungaji CHAN 2024

MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa ya Morocco, Oussama Lamlioui, amekuwa silaha ya maangamizi kwa Morocco kwenye michuano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN 2024), huku akiwa katika nafasi nzuri ya kutwaa tuzo ya mfungaji bora.

Kabla ya mechi za nusu fainali ambazo zilipigwa leo Jumanne, Lamlioui alikuwa akiongoza orodha ya wafungaji akiwa na mabao manne katika mashindano hayo ambayo kwa mara ya kwanza yanafanyika ukanda wa Afrika Mashariki ndani ya ardhi ya Tanzania, Kenya na Uganda.

Lamlioui amefunga mabao hayo muhimu, yakiwemo mabao yaliyoleta ushindi kwa Morocco dhidi ya DRC na Tanzania, yakihakikisha Morocco inaendelea kwenye hatua ya nusu fainali.

Mabao yake yamefanya Morocco kuwa hatari zaidi mbele ya lango na kuongeza matumaini ya kurejea nyumbani na medali kama sio za ubingwa, mshindi wa pili au wa tatu.

Mshambuliaji huyo wa RS Berkane anapigiwa chapuo la kuwa mfungaji bora kutokana na wapinzani wake wakuu, Sofiane Bayazid wa Algeria, Thabiso Kutumela wa Afrika Kusini na Allan Okello wa Uganda wenye mabao matatu kila mmoja timu zao zimeishia robo fainali.

Wachezaji ambao wanaweza kutoa changamoto kwa Lamlioui kwenye vita ya ufungaji ni Lalaina Rafanomezantsoa na Fenohasina Razafimaro wa Madagascar pamoja na Abdel Raouf kila mmoja akiwa na mabao mawili katika mashindano hayo.

Akiongelea kiwango cha mshambuliaji huyo, kocha wa Morocco, Tarik Sektioui alisema, “Oussama anajua kusoma mchezo, na huchukua nafasi muhimu wakati timu inahitaji bao. Uwepo wake ni mihimu kwa Morocco.”

Lamlioui ana uzoefu mkubwa wa soka la Afrika, huku akijivunia ushindi wa mataji matatu ikiwemo ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na RS Berkane msimu uliopita ambapo walitwaa baada ya kuifunga Simba jumla ya mabao 3-1 kwenye fainali.