Muhudumu asimulia tukio la mtu kuuawa kwa kukatwa wembe, gesti

Shinyanga. Muhudumu wa gesti, Consolatha Jacob amesimulia tukio la mteja wake kuuawa kwa kukatwa wembe siku ya Agosti 23, 2025 ambapo alishuhudia mtu huyo akitokwa damu nyingi akiwa amelala kifudifudi.

Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 26, 2025 katika eneo la tukio ambapo ni gesti ya Bwashee iliyopo Mtaa wa Mwabundu, Kata ya Ndala Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga ameeleza kuwa aliitwa kwenda kuangalia chumbani akakuta marehemu amelala chini akitokwa damu nyingi,

“Alikuja ‘mdada’ (dada) akaomba chumba alinitajia jina la Mariam Said nikaendelea na mambo yangu, lakini mwanaume alipoingia sikumuona, kumbe walikuwa wamemuagiza boda (bodaboda) awaijie (aende kuwachukua).

“Nilikuwa naendelea na mambo yangu baada ya hapo boda akaja kuniita akasema dada samahani njoo uone nikaingia chumbani, nikaona uvunguni pametapakaa damu na mtu kalala chini kalalia tumbo,” amesema Consolatha.

Pia, ameongeza kuwa; “nikaondoka kwenda kumuita muhudumu mwenzangu na boda naye akaenda kumuita mwenyekiti, akawapigia Polisi ndio wakaja wakati huo huyo mdada niliyempa chumba hakuwepo, na bodaboda alikuwa anajua chumba maana walimpigia simu awaijie, lakini wakati anaingia hakunisemesha kama anaingia, lakini damu ilikuwa ni nyingi sana chini sikuendelea kumwangalia” ameongeza Consolatha.

Naye kaimu mwenyekiti wa Mtaa wa Mwabundu, Elizabeth Magesa ameeleza kuwa ilikuwa Jumamosi alifuatwa na makamanda kwamba kuna tukio limetokea mtaani kwake.

“Ilikuwa saa 12 jioni nilifuatwa na makamanda nikaambiwa kuna tukio katika mtaa wangu, nilipofika nikakuta maaskari na dokta ambaye ni askari pia, wakanipeleka eneo la tukio nikakuta damu imetapakaa sana, lakini aliyejeruhiwa alikuwa amepelekwa hospitali na mtuhumiwa alikuwa amekimbia” amesema Elizabeth.

Pia, ameongeza kuwa; “Agosti 24,  askari wakamtuma bodaboda aniijie (akamchukue) tena nilikuwa na wajumbe wangu, nikaenda eneo la tukio na mtuhumiwa alikuwa ameshapatika na alisema amemjeruhi Timothy (Timithoy Magesa (35) kwa wembe, katika kukagua tukazunguka nyuma ya gesti tukakuta wembe ukiwa na damu. Karibu na dirisha la nyuma la gesti hiyo damu nyingi zilitapakaa kuanzia dirishani na chini,” ameongeza Elizabeth.

Awali Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi alieleza kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 23,2025   katika nyumba ya wageni ya Bwashee iliyopo kata ya Ndala Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga

“Kabla ya mauaji hayo, Pendo (Pendo Samson Methusela (37) alipigiwa simu na mwanamke mwingine kwa kutumia simu ya marehemu, akimuonya aachane naye kwa madai kwamba ndiye anayempenda baada ya muda Timothy (marehemu) alimtafuta Pendo na kumtaka wakutane katika nyumba hiyo ya kulala wageni ili wazungumze” alisema Magomi.

Aliongeza kuwa; “Walipokutana walianza kugombana kuhusu mwanamke aliyempigia simu, hali iliyosababisha Pendo kutumia wembe aliokuwa nao kumkata Timothy katika mkono wake wa kushoto pamoja na tumboni hali iliyosababisha kuvuja damu nyingi” alisema Magomi.

Magomi alieleza kuwa, Timothy alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, huku akianisha kuwa tukio hilo limetokea kutokana na wivu wa mapenzi na kwamba taratibu za kisheria zitakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa katika vyombo vya sheria.