MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa la Algeria, Sofiane Bayazid ambaye amefunga mabao matatu kwenye mashindano ya CHAN 2024 ametajwa huko Uholanzi kwa kuhusishwa na Heracles inayoburuza mkia kwenye msimamo wa Eredivisie.
Licha ya Algeria kuishia robo fainali kwenye michuano hiyo, Bayazid alionyesha kiwango kizuri kiasi cha kumezewa mate na Heracles ambayo imeanza msimu huu wa Ligi Kuu Uholanzi kwa kuchapwa mechi tatu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Algeria inaelezwa kuwa MC Alger wapo tayari kumwachia mchezaji huyo ambaye bado wanamkataba naye hadi Juni 30 mwakani.
Msimu uliopita, Bayazid alibeba ubingwa wa Ligi Kuu Algeria akiwa na MC Alger kwa mujibu wa mtandao wa transfermark, mchezaji huyo anatajwa kuwa na thamani ya Euro 450,000 ambazo ni zaidi ya sh1.3 bilioni.
Heracles kwa sasa inahitaji kuboresha kikosi chake kabla ya dirisha la usajili kufungwa ili kubadili mwenendo wa timu hiyo na miongoni mwa maeneo ambayo wanataka kuboresha ni pamoja na safu yao ya ushambuliaji hivyo Bayazid anatazamwa kama suluhisho.