Yanga kutesti  mitambo na Wakenya | Mwanaspoti

BAADA ya Rayon Sports, mastaa wa Yanga wanatarajia kushuka tena dimbani Septemba 12 wakiivaa Bandari ya Kenya kwenye tamasha la Wiki ya Mwananchi.

Mara ya mwisho Yanga ilicheza mechi ya kirafiki ya kimataifa kwenye tamasha hilo dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu Zambia msimu wa 2024/24 ikicheza na Red Arrow ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Yanga ambayo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda inatarajiwa kuwapa furaha Wananchi kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam kwenye tamasha la Wiki ya Mwananchi ambalo limekuwa likifanyika kila mwaka.

Tamasha ya Wiki ya Mwananchi hufanyika kila mwaka ikiwa maalumu kwa ajili ya kufungua msimu kwa klabu ya Yanga na kutambulisha nyota wake wapya.

Ni tukio linaloambatana na shughuli mbalimbali, lakini kubwa zaidi siku ya kilele huwa na mchezo baina ya Yanga na timu inayoalikwa kutoka nje ya nchi.

Mwaka huu, kilele cha tamasha hilo kitakuwa ni Ijumaa ya Septemba 12 kwa mechi ya kimataifa ya kirafiki baina ya Yanga na Bandari itakayochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bandari, Tonny Kibwana amethibitisha juu ya ushiriki wa michuano hiyo alipokuwa akizungumza na Mwanaspoti na kubainisha kuwa wanatarajia kuwasiri nchini mwishoni mwa mwezi huu.

“Ni kweli tutashiriki michuano hiyo tukiwa kama timu mwalikwa na tunaamini mechi yetu na Yanga itakuwa sehemu ya kujipima ubovu kwa kubaini bora na upungufu wetu kipindi hiki cha maandalizi ya msimu mpya,” alisema na kuongeza:

“Kikosi kitaanzia Arusha ambapo tutaweka kambi ya muda kabla ya kuja Dar es Salaam kuvaana na Yanga hiyo siku ambayo ndio wanaadhimisha tamasha lao.”

Alisema wanatambua wanakuja kucheza na timu bora Afrika na kubwa kwenye ligi ya Tanzania mipango yao ni kutoa ushindani na kupata mchezo mzuri ambao utakuwa kipimo sahihi kwao kabla ya kurudi kwenye michuano ya ligi yao ya ndani.

Shauku ya mashabiki wa Yanga kwenye mchezo huo ni kushuhudia ubora wa nyota wao wapya waliosajiliwa dirisha hili kama Lassine Kouma, Moussa Bala Conte,  Andy Boyeli, , Abdulnasser Mohamed ‘Casemiro’ na wengine.