Kiwanda kingine cha madini kujengwa Bahi

Bahi. Serikali imezindua mpango wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kusindika na kuyeyusha madini ya nikel na shaba kitakachogharimu Sh30 bilioni na kutoa ajira za moja kwa moja kwa watu 300.

Leo Agosti 26, 2025, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda hicho katika kijiji cha Zanka, Wilaya ya Bahi.

Mpango wa ujenzi wa kiwanda hicho umekuja ndani ya saa 24 tangu  Mavunde alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa maabara kubwa ya utafiti wa madini kwa Afrika Mashariki na Kati itakayojengwa eneo la Kizota jijini Dodoma na ujenzi ukikamilika utafanya mkoa huo kuwa na viwanda vitano vinavyohusika na madini moja kwa moja.


Mavunde ametaja faida tano za uwepo wa kiwanda cha kusindika na kuyeyusha madini ya nikel na shaba cha Zhong Zhau ikiwemo kuongeza pato la Taifa, lakini akisisitiza ajira kwa Watanzania na kuboresha maisha.

Ametaja faida nyingine kuwa ni kupata kodi na teknolojia mpya za kisasa katika sekta ya uchenjuaji wa madini, ajira kwa wananchi na uchumi wa wananchi kuongezeka kupitia viwanda hivyo, na jamii itaboresha huduma kwenye maeneo husika.

“Serikali itapata kodi ambayo itawezesha kujenga uchumi wa nchi, lakini tutapata nafasi ya kujifunza teknolojia mpya ya kuchenjua madini mbalimbali na kuikuza sekta hii,” amesema Waziri Mavunde.

Amewaagiza wachimbaji wadogo kuchangamkia fursa hiyo ili kupata masoko ya uhakika zaidi ambapo watajua ni wapi wanapaswa kupeleka bidhaa zao.

Amesema mahitaji ya kiwanda hicho kitakapokamilika ni tani 280 kwa mwaka, hivyo ni lazima wachimbaji wadogo wazalishe kwa tija ili  kufikia mahitaji ya kiwanda hicho.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wachimbaji wa Madini ya Nikel na Shaba Tanzania (Basemato), Tobias Kente ameiomba Serikali kuongeza nguvu ya utafiti katika maeneo yanayopatikana madini hayo ili wachimbaji wasichimbe kwa kubahatisha.

Kente ametaja eneo la Haneti ambalo linazalisha nikel lakini kunahitajika kufanyika utafiti zaidi, kwani eneo hilo ni dogo hivyo wangetamani leseni yake itanuliwe ili viwanda vipate nafasi.

“Lakini kule Mpwapwa pakafanyiwe utafiti ili waweze kuchimba na kuna maeneo kule ya kusini yanahitaji utafiti wa kutosha kuliko ilivyo sasa watu wanachimba bila kuwa na uhakika,” amesema Kente.


Mwenyekiti huyo amesema kwa muda mrefu wachimbaji wa madini ya nikel na shaba wamekuwa na kilio lakini sasa changamoto ya uwepo wa kiwanda imetatuliwa, kwani kiwanda hicho kitaanza kufanya kazi kati ya Oktoba au Novemba 2025.

Naye, Kamishna wa Madini, Abrahman Mwanga amesema ujenzi wa kiwanda hicho utakapokamilika utakuwa umemaliza changamoto mbalimbali za wachimbaji madini.