Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni akiwamo Amos Makalla kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ili kuanza rasmi majukumu yao mapya katika utumishi wa umma nchini.
Katika hafla hiyo ya uapisho iliyofanyika Ikulu jijini Dodoma leo Agosti 26, 2025 Rais Samia ametaja sifa zilizombeba Makalla katika uteuzi huo akisema ni utumishi uliotukuka aliouonesha akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Amos Makalla umekuwa kiongozi mzuri, kwa muda mfupi umeongoza kwa mafanikio makubwa kwa kukiunganisha chama chetu, sasa tumekuongezea jukumu jipya nenda kafanye kazi kwa uaminifu mkubwa,” amesema Rais Samia.
Rais Samia ameongeza kuwa sifa nyingine iliyombeba Makalla ni uzoefu wake katika kazi alizopitia ndani ya Serikali ikiwamo ukuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine alikofanya kazi kwa weledi na mafanikio makubwa.
Mkuu huyo wa nchi ameweka wazi kuwa, Mkoa wa Arusha umepewa kipaumbele katika ujenzi wa miradi ya kimkakati katika kuvutia uwekezaji au utalii hivyo inahitaji uongozi imara akimwagia sifa Makalla kuwa ana sifa za kutimiza lengo hilo.
“Nina imani kubwa kwa uzoefu wako katika uongozi wa mikoa ulikopita, utaenda kusimamia vizuri Mkoa wa Arusha, Serikali ina mipango mkubwa kuhusu Mkoa wa Arusha ikiwamo ujenzi wa mradi wa uwanja mkubwa wa michezo kwa ajili ya maandalizi ya AFCON, sina wasiwasi na wewe nenda kayasimamie hayo,” amesisitiza Rais Samia.
Mbali na Makalla, viongozi wengine walioapishwa katika hafla hiyo ni Khatib Kazungu ambaye ameteuliwa na kuapishwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, aliyeagizwa kumsaidia mkuu wa mkoa huo kutimiza malengo ya Serikali katika kujenga mji huo.
“Dodoma tunajenga miradi mingi ikiwamo Uwanja wa Ndege wa Msalato, ujenzi wa Mji wa Serikali, reli ya SGR na mingine mingi, nenda kasimamie vizuri na mkuu wa mkoa ili iende vyema,” amesisitiza Rais.
“Mkoa wa Dodoma umekuwa kivutio kikubwa cha utalii pia, kwa uzoefu wako una upeo mkubwa kulishika jiji hili na kuhakikisha mipango hii inakwenda vizuri, nenda kamsaidie mkuu wa mkoa kufikia malengo hayaya Serikali.”
Viongozi wengine waliokula kiapo hicho cha uaminifu katika utumishi wa umma ni Lurent Ndumbaro aliyeteuliwa kuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Dk Deo Mwasonga aliyeteuliwa kuwa balozi, Salama Akubu pamoja na Hassan Kitenge wote wameteuliwa kuwa maofisa katika utumishi wa umma.
Akitoa maelekezo ya jumla kwa watendaji hao wa umma wapya, Rais Samia amewataka kudumisha uongozi bora kwa kudhibiti rushwa na kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali za nchi kwa masilahi ya wananchi ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2050.
“Kwa watumishi wa umma, tumezindua dira yetu 2050 inayoonesha dira ya Tanzania tunayoitaka. Watanzania wanataka uadilifu, utumishi unaoendana na teknolojia ya sasa na kuhakikishha rasilimali zinatumika kwa maslahi ya watazania,” amesema.
“Nendeni mkapambane na tatizo sugu la rushwa ambalo bado linatunyemelea nchini mwetu, Watanzania pia wanataka utumishi wa umma unaotambua umuhimu wa kuunga mkono maendeleo ya sekta binafsi ili kufanya kazi mkono kwa mkono na sekta hiyo kwa maendeleo.”
Rais Samia amewatakia majukumu mema katika nafasi hizo mpya akidokeza kuwa Serikali imeongeza bajeti katika sekta ya utumishi wa umma ili kufikia matamanio ya wananchi kama yalivyoainishwa katika Dira 2050.