Msajili amkalia kooni Mpina asema hastahili kuwa mgombea urais

Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imebatilisha uteuzi wa Luhaga Mpina kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo, ikisema haukufuata taratibu za chama hicho, hivyo hastahili kuwa mgombea wa nafasi hiyo.

Uamuzi huo, unakuja baada ya ofisi hiyo kuwakutanisha viongozi wa chama hicho na Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala aliyelalamikia kupitishwa kwa Mpina, akidai kulivunja kanuni.

Mpina amekutana na kigingi hicho siku moja kabla ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kufanya uteuzi wa wagombea udiwani, ubunge na urais watakaoshiri Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025.

Baada ya hatua hiyo, inafuata hatua ya kuweka mapingamizi dhidi ya mgombea urais, hatua inayoweza kuwekwa na mgombea mwingine yeyote, msajili wa vyama au Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mwisho wa kuweka pingamizi kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi, ni hadi keshokutwa Agosti 28, saa 10:00 jioni, isipokuwa kama aliyeliweka ni Msajili wa Vyama vya Siasa, ukomo wake ni ndani ya siku 14 baada ya siku ya uteuzi.

Mpina na mgombea mwenza wa urais wake, Fatma Fereji walikwishachukua fomu na INEC za kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo na wanatarajia kesho Agosti 27 kuzirejesha kwa ajili ya uteuzi.

Tayari wawili hao wamezunguka mikoani kusaka wadhamini 200 katika kila mkoa kwenye mikoa isiyopungua kumi, ikiwemo miwili ya Zanzibar.

Aidha, wamekula kiapo Mahakama Kuu ya Tanzania mbele ya Jaji Hussein Mtembwa, ikiwa ni sehemu ya masharti ya kisheria yanayowataka wagombea wote wa nafasi ya urais kutimiza, kabla ya kuanza rasmi kampeni za uchaguzi mkuu.

Chanzo cha hatua hiyo ya msajili ni kitendo cha Monalisa kukiandikia chama chake, kisha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, akipinga uteuzi wa Mpina, kwa kurejea kifungu cha 16(4)i, iii na iv, cha Kanuni za Kudumu za Uendeshaji chama toleo la mwaka 2015 alizodai zilikiukwa wakati wa uteuzi.

Kwa mujibu wa kifungu cha 16 (4) (i) “wagombea wa urais/viongozi wa chama katika ngazi ya Taifa, wanatakiwa wawe wanachama wa ACT-Wazalendo kwa muda usiopungua mwezi mmoja kabla ya tarehe ya mwisho ya uteuzi ya wagombea wa chama.”

16(4)(iii) inasema, mgombea “awe tayari kutangaza mali binafsi na vyanzo vyake kabla ya kuteuliwa kugombea kwa kufuata utaratatibu ulioainishwa katika sehemu ya VI ya nyongeza ya Katiba ya ACT-Wazalendo.

Kifungu cha 16(4) (iv) kinataka mgombea “awe ni mtu aliyethibitika kuielewa itikadi, falsafa, misingi na sera za ACT-Wazalendo na aonyeshe utayari wa kuisimamia na kuiishi.”

Katika barua hiyo, Monalisa anadai Mpina anakosa sifa zote hizo, kwani alijiunga na chama hicho, Agosti 5 na Agosti 6, Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo ukampitisha kuwa mgombea wa urais.

Baada ya kusikiliza hoja za pende mbili, taarifa ambazo mwananchi imezipata kuwa ofisi ya msajili imekiandikia Chama cha ACT-Wazalendo kukiarifu uamuzi huo, kuwa Mpina hastahili kuwa mgombea wake wa urais.

Licha ya uamuzi huo, chama hicho kimesema ofisi hiyo haina mamlaka ya kubatilisha uteuzi wa mgombea, badala yake, msajili ana mamlaka ya kuweka pingamizi kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Mwananchi limetaarifiwa kuwa, uteuzi wa Mpina umebatilishwa na tayari barua ya taarifa hiyo imeshawasilishwa kwa pande zote mbili yaani ACT Wazalendo na kwa Monalisa. Pia, nakala imetumwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Alipotafutwa Msajili Jaji Francis Mutungi kuzungumzia hilo, simu yake iliita bila kupokewa.

Alipoulizwa Msajili msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amesema anachojua ni kuwa majibu ya suala hilo yangetolewa leo Jumanne na kwa taarifa zaidi atafutwe Jaji Mutungi.

“Majibu yatatolewa leo, lakini mpigie msajili ndiyo akueleze kwa kina,” amejibu Sisty.

Hata hivyo, Monalisa kwa upande wake, amekiri kupokea uamuzi wa ofisi ya msajili na kwamba anaandaa taarifa kwa umma kwa ajili ya kuisambaza.

Mwananchi pia, imemtafuta Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, simu yake ilikatika na akatuma ujumbe akiomba atumiwe ujumbe, ambao hata ulipotumwa haukupata majibu hadi taarifa hizo zinachapishwa.

Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita amesema hana taarifa ya kupokelewa kwa barua, lakini Msajili hana mamlaka ya kubatilisha uteuzi wa mgombea wa chama hicho.

Ameeleza msajili ana mamlaka ya kikanuni ya kuwasilisha pingamizi kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na si kubatilisha uteuzi wa mgombea ndani ya chama cha siasa, iwapo amefanya hivyo ni nje ya mamlaka yake.

“Kama ataamua ovyo ni sawa, lakini si mamlaka yake kubatilisha uteuzi wa mgombea ndani ya chama chetu. Hawezi kubatilisha wakati yeye ndiye amesikiliza malalamiko, yeye pia ndiye awe hakimu havieleweki,” amesema.

Mpina alitambulishwa kujiunga na ACT Wazalendo Agosti 5, 2025 akitokea Chama cha Mapinduzi (CCM), alikokuwa Mbunge wa Kisesa kwa miaka 20 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, kadhalika Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira.

Ushindani umepigwa nyundo

Uamuzi huo wa msajili dhidi ya Mpina na ACT Wazalendo umeelezwa ni sawa na kuupiga nyundo ushindani katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu, kama inavyoelezwa na mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk George Kahangwa.

“Kama Mpina atakuwa ameondoshwa, ushindani utakuwa mdogo sana. Ukiangalia wale waliosimama mwenye uwezo wa kusema ataleta ushindani kidogo alikuwa Mpina,” amesema mwanazuoni huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kwa hali ilivyo, Dk Kahangwa amesema CCM imepata “mchekea katika uchaguzi huu na itakuwa mara ya kwanza kwa chama hicho tawala kukosa mshindani wa kweli.”

“Kama hakutakuwa na mpinzani tofauti na Mpina, CCM kwa mara ya kwanza katika historia itaingia kwenye uchaguzi bila mshindani. Ukimwondoa Mpina, Tundu Lissu mazingira ndiyo hayo, hakuna ushindani. Kwa hiyo ni kama ushindani umepigwa nyundo,” amesema.

Hata hivyo, amesema kwa hatua hiyo, inaonekana dhahiri kunahitajika mazungumzo ya pamoja kama Taifa, ili kuwa na uchaguzi utakaokuwa na wagombea watakaopimwa kwa ushindani, uadilifu na uwezo wao.

“Tusipofanya hivyo, tutarudi enzi zile za mgombea hapa kivuli hapa na kivuli hakiwezi kushinda kwa sababu hakijielezi, hakina sera,” amesema Dk Kahangwa.

Baada ya juna lake kuengulia hatua za awali ndani ya CCM, aliibukia ACT-Wazalendo kisha kupitishwa kuwa mgombea wa chama hicho.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari siku kadhaa baada ya kupitishwa kuwa mgombea urais, Mpina aliahidi angewashughulikia wabadhilifu kuanzia siku ya kuapishwa, iwapo angeshinda urais.

Sambamba na hilo, alisema iwapo angechaguliwa kuwa rais wa Tanzania, siku ya kuapishwa angetangaza kuanza mchakato wa Katiba Mpya.

Kwa mujibu wa Mpina, suala la kukomesha ufisadi na mafisadi halitahitaji subira katika Serikali yake, atalishughulikia ndani ya saa 24 baada ya kuapishwa kuwa rais wa nchi.

“Mwenyezi Mungu atakaponijalia hiyo Oktoba nikipata hii nafasi, chama changu kimeelekeza kwamba ndani ya miezi sita mchakato (wa Katiba)  uwe umeanza. Mimi nitaagiza jukwaani pale baada ya kuapa mchakato uanze,” alieleza.

Hatua kama hizo, aliahidi kuzichukua dhidi ya wabadhilifu wa mali za umma na mafisadi, akisema kupitia hotuba yake baada ya kiapo, atatangaza kuwashughulikia.

Alisisitiza kazi ya rais ni kusimamia sheria na kuhimiza utekelezaji wake, hivyo haitakuwa taabu kwake kuelekeza hatua zichukuliwe dhidi ya yeyote atakayebainika kuhusika na ubadhilifu wa mali za umma.