SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limesema katika mageuzi ya Mashirika ya umma yanayoendelea kufanywa na Serikali, ni lazima TRC ihakikishe inafanya mabadiliko katika sekta ya biashara na ya uendeshaji kwa ushirikiano na sekta binafsi
Mkurugenzi mkuu wa TRC Mhandisi Machibya Shiwa, amebainisha hayo jijini Arusha pembezoni mwa kikao kazi cha Wenyeviti na watendaji wakuu wa taasisi za umma kilichoanza Agosti 23 na kufikia tamati yake Agosti 26, 2025, ambapo amesema sekta binafsi inaweza kuiwezesha TRC kupata mapato zaidi kuliko inavyojiendesha sasa.
Mhandisi Shiwa, ameishukuru serikali kwa kuruhusu sekta binafsi iweze kushiriki kwenye uendeshaji wa reli kufuatia marekebisho ya sheria nambari 10 ya reli ya mwaka 2017, yaliyofanyikwa mwaka 2023 na kusainiwa na Mheshimiwa Rais, hivyo kutoa fursa za kiuendeshaji kwa watu binafsi.
Aidha Mkurugenzi mkuu huyo wa TRC, amesema, moja ya changamoto iliyokuwa inaipata TRC ni kuwa na miundombinu mipana ambayo inatumia theluthi moja ya uwezo wake, hivyo inapoingizwa sekta binafsi inamaanisha ile sehemu ya miundombinu iliyopo TRC, sekta binafsi inaweza kushiriki na kuwezesha TRC kupata mapato zaidi kuliko inavvyojiendesha sasa.
Mabadiliko mengine amesema Mhandisi Shiwa, ni kwamba TRC inataka kuishirikisha sekta binafsi katika masuala yakiwemo ya ukarabati wa njia ya reli, vichwa na mabehewa na ikiwezekana tunakoekea TRC ibaki na jukumu la kiundeshaji tu.