Dk Migiro akabidhiwa ofisini akisema ‘tupo tayari kukitetea chama’

Dodoma. Katibu Mkuu mpya wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Asha-Rose Migiro ameanza rasmi kazi akisema, “tuko tayari kukitetea chama chetu ili kihakikishe wagombea wetu kinashinda.”

Dk Migiro amesema hayo leo Jumanne, Agosti 26, 2025 akiwa makao makuu ya CCM, ‘White House’ jijini Dodoma, alipofika kukabidhiwa ofisi na Dk Emmanuel Nchimbi.

Agosti 23, 2025, Halmashauri Kuu ya CCM chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mambo mengine, ilimteua Dk Migiro kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, kuchukua nafasi ya Dk Nchimbi.

Dk Nchimbi anaachia nafasi hiyo baada ya mkutano mkuu wa CCM wa Januari 18-19, 2025, kumteua kuwa mgombea mwenza wa urais. Ni baada ya jina lake kupendekezwa na mgombea urais wa chama hicho, Rais Samia.

Rais Samia na Dk Nchimbi na wagombea wa vyama vingine wanasubiri uteuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kesho Jumatano, Agosti 27, 2025 ili kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. 

Dk Migiro ambaye amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), baada ya kufika makao makuu ya chama hicho, amepokewa na mamia ya wanachama waliokuwa nje wakimsubiri.

Alikuwa ameongozana na Dk Nchimbi na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa. Akizungumza na umati huo wa wanachama, Dk Migiro amewametakiwa kudumisha mshikamano na upendo kuelekea kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu, ili kuhakikisha chama hicho kinaendelea kuaminiwa na wananchi.       


                      

Amesema msingi na mtaji mkubwa wa chama hicho ni wanachama, hivyo mshikamano wao ndiyo silaha ya ushindi.

Aidha, amewataka wanachama na wapenzi wa CCM kuhakikisha chama hicho kinashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao, kwa kufuata misingi, nidhamu na maadili yaliyoasisiwa na viongozi waasisi wa chama hicho.

Dk Migiro pia amesisitiza mshikamano wa wanachama ni nguzo imara inayoifanya CCM kuwa chama chenye nguvu na mshikamano wa kijamii, na kusisitiza kuwa ushindi wa chama hicho ni wa Watanzania wote.

Vilevile amewashukuru wanachama kwa mapokezi mazuri aliyoyapata, akisem ni kielelezo cha mshikamano, upendo na ushindi unaoendelea kudumu ndani ya chama hicho tawala.         

“Nichukue nafasi hii kuishukuru Halmashauri Kuu na Kamati Kuu kukubali, kuridhia mimi niwe mrithi wa kada mahiri na madhubuti anayejulikana kama Balozi Emmanuel Nchimbi,” amesema Dk Migiro.

‎‎Amesema Dk Nchimbi, aliyewahi kuwa waziri kwenye wizara mbalimbali ana uzoefu mkubwa, ameingia kwenye chama akiwa kijana mdogo hadi sasa ameendelea kuwa kada mahiri wa Chama cha Mapinduzi.

‎‎Dk Migiro amesema waswahili wanasema kidole kimoja hakivunii chawa, Dk Nchimbi amefanya kazi chini ya uongozi wa mwenyekiti, makamu mwenyekiti wawili wa Tanzania Bara na Zanzibar na amefanya kazi kwa kushirikiana na sektarieti ya chama ambayo ina manaibu katibu wakuu, wakuu wa idara na nyinyi pamoja na wanachama wenzake.

‎‎Amesema wanachama wa CCM ndio mtaji na rasilimali kubwa ya Chama cha Mapinduzi huku akiwapongeza wanachama hao kwa kazi nzuri waliyokuwa wakiifanya chini ya viongozi wa chama hicho.

‎Amesema kujitokeza kwa wanachama hao kwa wingi kumpokea ni dalili nzuri kwa chama hicho katika siku wanazoziendea kwa ajili ya kampeni na baadaye kwenda kukamata dola.

‎‎Amesema kuja kwake katika nafasi hiyo ni kutokana na wanachama hao walivyompa ushirikiano wakati wote akiwa sekretari huku akisema kuna kazi kadhaa wakiifanya wakiwa pamoja.

‎‎‎‎Kwa upande wake, Dk Nchimbi akimkaribisha Dk Migiro amempongeza Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan kwa kumteua katibu huyo mpya huku akisema wanaccm hawana mashaka katika nyadhifa mbalimbali alizowahi kuzishika katika chama, Serikali na kimataifa.


‎”Nashukuru Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa kuona uzito wa nafasi hii na kutambua aina ya mtu ya wanaccm na Watanzania wanakuwa tayari kufanyanaye kazi,” amesema.

‎‎Aidha, amemshukuru Rais Samia kwa kumuamini katika nafasi hiyo katika kipindi alichomalizia huku akisema kwa sasa wana kada mwingine ambaye yupo tayari kuendeleza na kwamba wanaimani nae.‎