TIMU ya taifa ya Madagascar imeweka historia kwa kutinga fainali ya michuano ya CHAN 2024 kufuatia kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ndani ya dakika 120 dhidi ya Sudan katika mechi ya nusu fainali iliyochezwa leo Jumanne Agosti 26, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Hii ni mara ya kwanza kwa Madagascar kutinga fainali ya mashindano hayo yanayohusisha wachezaji wa ligi za ndani, mafanikio yao makubwa walipata CHAN 2022 kwa kushika nafasi ya tatu.
Mechi hiyo ilianza kwa tahadhari kubwa huku kila upande ukionekana kutafuta bao la mapema jambo ambalo halikuonekana kuwa na matunda katika dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Katika kipindi hicho cha kwanza, Madagascar ambayo imetokea kundi B ambalo liliongozwa na Taifa Stars, ilipiga mashuti sita huku moja tu ndio likilenga lango, Sudan ilipiga mshuti matatu na yote yakilenga lango.
Mwamuzi wa mchezo huo, Mehrez Melki alionekana kufanya kazi kubwa huku akimwaga kadi za njano kwa wachezaji watatu wa Madagascar, Randriamanampsioa, Razafimahatana na Randriamanampisoa huku wawili wa Sudan, Tia Asad na Simbo nao wakionywa.
Kipindi cha pili kiliendelea kuwa cha kuvutia huku yakifanyika mabadiliko kadhaa kwa timu zote mbili.
Katika dakika ya 79, Madagascar ilijikuta ikipata pigo baada ya kiungo wao, Fenohasina Razafimaro kuonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyoambana na nyekundu ikiwa ni dakika nne tu tangu kuonyeshwa kadi ya kwanza.
Hata hivyo licha ya Madagascar kuwa pungufu, ilionesha kumudu dakika zilizosalia na kufanya mchezo huo kwenda dakika 30 za nyongeza baada ya kutoka suluhu katika dakika 90.
Wakati wengi wakiamini pengine mechi hiyo inaweza kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti, Madagascar ilipata bao katika dakika ya 116 kupitia kwa Toky Rakotondraibe aliyemalizia pasi ya Randrianirina.
Licha ya juhudi ambazo zilifanywa na Sudan, Madagascar ikiwa pungufu ilikuwa imara na kuandika historia kwa kutinga fainali ya michuano hiyo ambayo kwa mara ya kwanza inafanyika ukanda wa Afrika Mashariki.
Madagascar inasubiri mshindi wa nusu fainali itakayochezwa kuanzia saa 2:30 usiku wa leo kati ya Senegal dhidi ya Morocco ili kucheza nayo fainali Agosti 30 mwaka huu kwenye Uwanja wa Moi nchini Kenya.