Moshi. Mwili wa Askofu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Dk Martin Shao (86) unatarajiwa kuagwa Septemba 3, 2025, Usharika wa Moshi Mjini na kuzikwa Septemba 4, Usharika wa Lole Mwika, Wilaya ya Moshi.
Dk Shao ambaye alihudumu kama Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini kuanzia mwaka 2004 hadi 2014 alipostaafu, alifariki dunia asubuhi ya Agosti 25, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) Mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro.
Leo Jumanne, Agosti 26, 2025 nyumbani kwa marehemu, Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Fredrick Shoo amesema Dayosisi hiyo kwa kushirikiana na familia wanaendelea na mipango ya mazishi na wanatarajia kuulaza mwili wa Dk Shao Septemba 4, katika Usharika wake wa nyumbani Lole.
“Tunaendelea kuweka mipango kwa ajili ya kuulaza mwili wa baba yetu, tumepanga kwa kushirikiana na familia Septemba 3, mwaka huu tutafanya ibada ya kuaga mwili pale kanisa la KKKT Usharika wa Moshi Mjini ili watu wauage pale na pia kutakuwa na salamu mbalimbali za rambirambi,” amesema Askofu Shoo.
“Septemba 4, tutakwenda kuulaza mwili wa baba kule katika usharika wa nyumbani wa Lole, Mwika Wilaya ya Moshi,” amesema.
Aidha, Askofu Shoo amesema, Dk Shao ameugua kwa muda mrefu na msiba huo ni mkubwa na umewagusa wengi hususan waumini wa kanisa hilo Dayosisi ya Kaskazini ambako alikuwa kiongozi.
“Sote tunajua uhai wetu upo mikononi mwa Mungu, hatuna mamlaka na uhai wetu, kwa hiyo saa yake ilipofika ilimpendeza Mungu akamchukua mtu wake. Tunachopaswa kufanya ni kumwambia Mungu asante kwa kutupa baba huyu, asante kwa maisha yake, asante kwa utumishi wake akiwa kama kiongozi wetu na mlezi wetu wa kiroho, asante Mungu kwa kuwa ulitupa mtu huyu,” amesema Askofu Shoo.
“Tunafahamu baba aliugua kwa kipindi kirefu na wengi tulikuwa tunafanya maombi kwa ajili yake na tulimtembelea alipokuwa Hospitali. Tulikuwa tunawasiliana mara kwa mara na kijana wake kuhusu hali ya baba naye akawa ananipa taarifa na jana asubuhi nikiwa safarini niliwasiliana naye akaniambia ameamka ana nafuu kidogo, lakini saa tano akaniambia baba amelala.”
Askofu Shoo amesema: “Ni msiba mkubwa ambao umetugusa sisi sote, wa kuondokewa na baba yetu na kiongozi wetu, napenda kusema kwa watu wote, watoto, majirani na washarika wote wa dayosisi hii, tufarijike katika bwana na Mungu mwenyewe atutie nguvu tulipokee hili kama watu wa imani.”
Aidha amesema wameondokewa na kiongozi ambaye ameacha alama zisizofutika katika Dayosisi hiyo na hata kwa mtu mmojammoja.
“Tumeondokewa na kiongozi ambaye ameacha alama katika Dayosisi hii, ameacha alama nyingi za kukumbukwa kwa mtu mmojammoja na kwa ujumla wake akiwa kama kiongozi wetu, kipekee katika Usharika wa Moshi mjini tangu akiwa mchungaji katika usharika ule akiwa msaidizi wa Askofu, lakini alitangulia kuwa mkuu wa jimbo.”
“Tunafahamu unyenyekevu wake, utulivu wake na kujitoa kwake kwa ajili ya huduma hii, kibinadamu tulitamani kuendelea kuwa na baba huyu lakini tunafahamu tumewekewa mipaka, hatuna mamlaka ya kuamua mwisho wa mtu uweje,” amesema.
Kwa upande wake, Mchungaji wa usharika wa Moshi Mjini, Genoveva Ndimbwire amesema familia na washarika wote wa Dayosisi hiyo wanapaswa kumshukuru Mungu kwa maisha ya Dk Shao duniani.
“Tumshukuru Mungu kwa maisha ya baba yetu lakini pia tujifunze kwa unyenyekevu, upendo na utumishi wake,” amesema.